Monday, October 4, 2010

WIKIENDA SHOWBIZ!

JokateMiaka 16 ya Miss TanZania: Lundenga alivyotimuliwa na Mama Jokate
Miaka 16 kwa utaratibu wa kileo, unatosha kumfanya mtoto azaliwe na kumaliza kidato cha nne. Miss Tanzania imekua lakini kuna changamoto za kuangalia ili tukumbuke walipotoka.

Mwaka 1994, Hashim Lundenga kwa kushirikiana na Prashant Patel waliunda wazo la pamoja la kuanzisha Miss Tanzania. Wakafuata taratibu zinazofaa na mwaka huo huo wakapata usajili na kuanzisha mashindano.

Kabla ya hapo, miaka ya 60 kulikuwa na mashindano ya urembo ambayo yalipigwa marufuku na serikali baada ya kuonekana yanakwenda kinyume na utamaduni wa nchi.

Yaliporuhusiwa, Aina Maeda alishinda mwaka 1994, Emil Adolph (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basila Mwanukuzi (1998), Hoyce Temu (1999), Jacqueline Ntuyabaliwe (2000), Happiness Magesse (2001), Angela Damas (2002), Sylvia Bahame (2003), Faraja Kotta (2004), Nancy Sumari (2005) na Wema Sepetu (2006).

Wengine ni Richa Adhia (2007), Nasreen Karim (2008), Miriam Gerald (2009) na Genevieve Emanuel Mpangala (2010). Jumla ni warembo 17 katika miaka 16. Zipo changamoto nyingi ambazo Lundenga anazieleza kama alivyofanya mahojiano na safu hii hivi karibu.

CHANGAMOTO
Lundenga anasema: “Miss Tanzania tupo busy sana. Mwaka mzima ni kupanda na kushuka lakini kubwa ni jinsi ambavyo inakuwa ngumu kwa baadhi ya wazazi kuelewa thamani ya Miss Tanzania. Ni ukweli kwamba mashindano yamekua kwa kiasi kikubwa, ila changamoto hatuziepuki.

“Ni ngumu sana kupata warembo wenye sifa. Mawakala wanahangaika kutafuta warembo lakini kuna ugumu kutoka kwao wenyewe mpaka wazazi,” anasema Lundenga.

Anagusia kuwa mwaka 2006, alitimuliwa na mama wa Miss Tanzania namba 2 2006-07, Jokate Mwegelo alipokwenda kumuombea ruhusa ya kushiriki mashindano hayo Kanda ya Temeke, baada ya mratibu wake, Benny Kisaka kuvutiwa naye, mrembo mwenyewe kupenda fani lakini wazazi wakagoma.

Lundenga anasema, hata mwaka huu haikuwa rahisi kwa Kisaka kumnasa Genevieve Miss Temeke kwa sababu wazazi wake waligoma kumruhusu.

“Usione mambo yanaenda, hawa waandaaji wa kanda hasa Jackson Kalikumtima (Ilala), Yusuf George ‘Boy George’ na Kisaka wakati mwingine ni kama wehu, wakiona warembo hawatulii. Mwaka mzima wanasaka warembo, kwahiyo kazi inafanyika na muda si mrefu tutaona matunda Miss World,” anasema na kuongeza:

“Jacqueline Ntuyabaliwe (K-Lynn) tulimchukua kwa kulazimisha, Hoyce aligoma kushiriki eti kuna rushwa ya ngono, pia Happiness Magesse, kwahiyo ni kazi kubwa kuhakikisha warembo wenye sifa wanashiriki.

“Hata Nancy ilikuwa ngumu kushiriki, alipotoka namba tatu Dar Indian Ocean aligoma kwenda Miss Kinondoni. Nadya Mohamed, wazazi wake walisimama kidete kuhakikisha mtoto wao hashiriki Miss Tanzania.”

MATARAJIO CHANYA
“Kuna tatizo linatukabili, wakati mwingine tunapata warembo wazuri lakini uwezo wa kujieleza ni tatizo. Mfano, mwaka jana, kila mtu aliyemuona Miriam alikubali kwamba Tanzania tumepeleka mrembo sahihi lakini uwezo wake wa kujieleza ulikuwa mdogo. Vazi la ufukweni, alifanya vizuri na akawa mmoja wa warembo 40 waliochaguliwa kwenda kufanya shopping kabla ya kutua Afrika Kusini yalipofanyika mashindano.

“Tupate warembo kama Miriam wenye uwezo wa kujieleza na hapa wapo. Na dalili zipo wazi kwamba muda si mrefu tutafanikiwa hasa kutokana na msukumo wa sasa wa wazazi kupeleka watoto shule za kimataifa. Unajua watu hawajui kwamba Tanzania ndiyo nchi yenye wanawake wazuri zaidi duniani.”

KINACHOFANYIKA
“Tunajitahidi kupanua nafasi za warembo kutoka vyuo kushiriki. Hatuna maana kanda nyingine haziwezi kwa sababu Nancy alifanya vizuri na kutoka Miss World Africa wakati alikuwa anatokea kidato cha nne Kenya. Njia ambazo tunazifanyia kazi kwa sasa, bila shaka zitatuwezesha kupata warembo bora wenye uwezo wa kujieleza.

“Kikubwa ambacho tunakihofia ni kuwekeza nguvu kwenye kushawishi warembo kushiriki, maana yake ukimwambia miss aingie kwenye shindano maana yake umemuahidi ushindi, kitu ambacho kinaweza kusababisha kelele endapo atashindwa.”

MAANDALIZI YA WAREMBO HAYATOSHI
“Kwanza mrembo anakuwa na mwaka mzima wa kujiandaa kupitia mashindano yetu ngazi mbalimbali. Kwahiyo maandalizi yanatosha kwa sababu kinachofanywa Miss World ni kile kile kinachofanywa na Miss Tanzania.

“Pamoja na hivyo, kuna ukweli kwamba tunatakiwa kuwapata warembo wetu mapema kabla ya kwenda Miss World ili wapate maandalizi mazuri, lakini kilichopo ni kwamba makampuni ya udhamini yanakuwa na pesa katika kalenda yetu ya sasa, kwa maana bajeti zao hupitishwa baada ya Aprili.”

VIPI KUHUSU JULIET WILLIAM?
Alitoka Miss Tanzania namba tatu mwaka jana, lakini mwaka huu ameibuka na taji la dunia la Miss Progress International. Anaitwa Juliet William, je, Lundenga anamzungumziaje: “Amefanya vizuri sana, namfahamu Juliet ana uwezo mkubwa wa kujieleza na ana umbo zuri, alistahili ushindi kwa sababu alipata malezi bora Miss Tanzania.”

KAULI KUHUSU GENEVIEVE
“Apewe ushirikiano, anakwenda China kushiriki Miss World na kikubwa ni kwamba ataitangaza nchi yetu, kwahiyo hilo ni muhimu kwetu. Hamtangazi Lundenga, anaitangaza Tanzania na vivutio vyake.”

Mwaka 2007, Richa alicheleweshewa DVD inayoonesha kazi zake nchini, hivyo kumpunguzia maksi mwaka huu vipi? Lundenga anajibu: “Kilichotokea kipindi kile ni makosa ya Kamati ya Miss World, lakini utaratibu wa sasa ni kwamba mrembo mwenyewe anaondoka na DVD yake mkononi halafu akifika anakabidhi. Genevieve ameondoka nayo.”
**************************************

The Undertaker:
Undertaker: Mbabe anayeishi na maumivu ya kuporwa mke
Mchezo wa miereka umekuwa ukikua na kujizolea umaarufu kila kukicha, ingawa baadhi ya nchi kuna mashabiki wa mchezo huo wamekuwa na shaka juu ya uhalisi wa mchezo wenyewe.

Kinachowafanya wasiamini kuwa mchezo huo ni wa kweli ni jinsi unavyotawaliwa na matukio ya kutisha yanayoonekana ulingoni. Kuna wababe wengi wenye uwezo mkubwa ulingoni, wakiwa na rekodi ya kiwango cha juu lakini kati yao huwezi kumsahau Mark William Calaway ‘The Undertaker’.

Ni mkongwe lakini kiwango chake ulingoni hakina shaka. Ana umri wa miaka 45 lakini anavyowahenyesha vijana ambao inaaminika damu zao zinachemka ni kitu kinachosisimua kupita kiasi.

Staili yake ya kuibuka kutoka kwenye jeneza ni kitu ambacho siyo tu kwamba kinasisimua bali pia kinamfanya wa kipekee. Ana rekodi ya kupigana na watu wengi ulingoni na kuwashinda wote.

Anapopanda ulingoni mandhari hubadilika, sauti mfano wa king’ora husikika, hapo mashabiki wa miereka hasa wale wa WWE, hushangilia kwa nguvu kwa sababu wanajua ‘kifuatacho’ ni action za Undertaker. Msisimko Ulingoni Kamisheni ya World Wrestling Entertainment (WWE) imekiri kuwa inatumia kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kuandaa mbwembwe na vikorombwezo vya taa na vitu vingine wakati Undertaker anapokuwa anaingia ulingoni.

Kuwasili kwake ulingoni ni kitu ambacho kimekuwa kikiwashangaza mashabiki wa mchezo huo duniani. Manjonjo yake na jinsi anavyopambana na kushinda, ndivyo vinamfanya Undertaker kuwa mcheza mieleka mwenye mvuto wa aina yake. Uwezo ulingoni Hili ni jambo pekee ambalo limekuwa likimfanya kuonekana mtu wa ajabu, kwani uwezo wake na nguvu alizonazo zimemuwezesha kushinda mapambano yake mengi bila kupata upinzani mkali licha ya kwamba anaonekana umri umekwenda.

Wakati mwingine anacheza na watu zaidi ya sita na kuwapiga wote, na uwezo huo ndiyo unaowafanya wanamieleka wengine wagome kupanda naye ulingoni kupigana mmoja mmoja (one against one).

Kuingia na Jeneza Ni staili ambayo imemjengea umaarufu, kwani mara kadhaa imemsaidia kupata ushindi ‘kiulani’ kutokana na hofu inayowapata wapinzani wake pindi wanapoona jeneza limefunguliwa. Wengi huogopa na kutimua mbio, hivyo kumfanya aendelee kushikilia mkanda bila kutoka jasho. Undertaker anapendwa na anaheshimiwa na watu wengi.

Mbinu za Ushindi Ingawa siyo mtaalamu sana wa staili za mapigano lakini amekuwa anashinda mapambano yake kwa mbinu nyingi. Inapotokea mpinzani wake anatumia mtindo wa kujifanya kalegea kwa kipigo, yeye hutafuta njia ili amkamate kichwa chini miguu juu na kumpigiza kwenye sakafu na kumaliza pambano.

Kukaba Koo
Hii ni hatua ya mwisho ambayo Undertaker huitumia kumaliza pambano, hasa baada ya kuwa amemlainisha mpinzani wake kwa kipigo, humkaba koo kwa nguvu na kumtupa kwenye jeneza kisha kumfunika na mchezo kumalizika. Pambano la kifo Licha ya kuwa anamkubali Ray Mysterio Junior kama mwanamieleka mwenye mbinu za ajabu katika mchezo huo lakini bado pambano lake na mbabe Batista linabaki kuwa pambano kali linalobatizwa jina ‘pambano la kifo’ kila wakutanapo.

Batista anatajwa kuwa mwanamiereka pekee ambaye hajawahi kukabwa koo na Undertaker au kulainishwa na kutupiwa kwenye jeneza.
Rekodi aliyonayo Undertaker ni bingwa mara saba wa Dunia ikiwa ni pamoja na ubingwa mara nne wa WWF/E, ubingwa mara tatu wa uzito wa juu unaotambuliwa WCW, ubingwa wa dunia wa WWF Hardcore, pia akiweka kibindoni rekodi ya ubingwa mara saba wa World Tag Team Champion.

Undertaker pia ni bingwa mara sita wa WWF World Tag Team na ubingwa mara moja wa WCW World Tag Team. Kikubwa kikiwa ni ubingwa wa dunia wa Royal Rumble alioutwaa mwaka 2007 mbele ya wababe Big Show, Batista na Shawn Michael.
Chuki Ulingoni Mara nyingi Undertaker amekuwa akipambana na chuki nyingi ulingoni kutoka kwa wapinzani wake wanaohofia uwezo wake, mfano mzuri ukiwa ni tukio ambalo alimanusura lichukue uhai wake baada ya kufanyiwa unyama wa kupigwa na kiti kichwani na Shawn Michael.


Undertaker pia katika pambano hilo, alikalishwa kwenye kiti cha umeme kabla ya kuokolewa na bingwa wa wakati huo Lex Luger, hii ilikuwa ni mwaka 1997 kwenye mpambano wa WWF Summer Slam. Kuzushiwa kifo Mei 20, 2010, Undertaker alizushiwa kifo baada ya tukio la kupigwa mpaka kupoteza fahamu kabla ya kufukiwa kwenye shimo na wapinzani wake waliokuwa wakiongozwa na Big Show pamoja na Edge.

Baada ya kumaliza mpambano wa hatari wa ‘No Way Out’ ambao wababe wa uzito wa juu huingia ndani ya ulingo halafu unashushwa wavu mkubwa ikiwa na maana kuwa anayefanikiwa kumshinda mwenzake na kutoka ndiye mshindi.

Maisha yake ya kimapenzi Undertaker alifunga ndoa ya kwanza na Jodi Lynn mwaka 1989, miaka mitatu baadaye walifanikiwa kupata mtoto aitwaye Gunner, lakini waliachana mwaka 1999.

Julai 21, 2001 alifunga ndoa na Sara, St. Petersburg, Florida, Marekani na kufanikiwa kupata watoto wawili wa kike Chasey aliyezaliwa Novemba 21, 2002 na Gracie Mei 15, 2005.

Miaka miwili baadae yaani 2007, Undertaker alimuacha Sara akiwa bado anampenda baada ya kuvuja taarifa kwamba mkewe huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamieleka mwingine. Juni 26, 2010, Sara na Michelle walifunga ndoa.

Adui yake Kamisheni kubwa ya WWE pamoja na ile ya WWF zililazimika kupiga marufuku uwepo wa pambano linalomkutanisha Undertaker na Michelle.

Hiyo ni baada ya Michelle kumchukua mke wa Undertaker na kumuoa. Kamisheni hizo, ziliamua kufanya uamuzi huo kwa sababu kwa chuki iliyopo, kuna hofu kwamba ipo siku wanaweza kuuana ulingoni. Nje ya mchezo Undertaker ni mjasiriamali. Alishirikiana na mkewe wa zamani, Sara kuanzisha taasisi ya mafunzo ya kutibu wanyama inayoitwa Texas A&M College of Veterinary Medicine & Biomedical Sciences.

Amewekeza dola za Marekani milioni saba (shilingi bilioni 12) katika ujenzi wa nyumba maaalum za makazi, Loveland, Colorado, mradi unaoitwa “The Catahart”, ikiwa anashirikiana na swahibu wake Scott Everhart.

Undertaker pia ni shabiki wa masumbwi (boxing) na bondia anayemhusudu ni Mann Pacquiao wa Philippines, amekuwa akihudhuria mapambano yote ambayo Mfilipino huyo amecheza kama ambavyo alionekana akipeperusha bendera za Marekani na Phillippines wakati Pacquiao alipopambana na Velázquez mwaka 2005.
Kituko Wakiwa kwenye kipindi cha mahojino na kituo kimoja cha runinga, Manila Philippines mwaka jana, Undertaker na Batista walipigana studio kama wako ulingoni na kuvunja vitu vya thamani kubwa.

Baadaye, Undertaker na Batista walikubali kulipia gharama ya vitu walivyoharibu na mpaka leo ikitokea wanahojiwa, huwekwa vyumba tofauti kwa kuhofia yaliyotokea. Alikotoka Alizaliwa Machi 24, 1965. Ni mkali anayetambuliwa na kamisheni ya WWE katika Smack Down Brand.

Alianza kuingia kwenye mashindano ya kunyanyua vyuma vizito yaliyokuwa yanazihusha kambi kadhaa za mazoezi (Gyms), mwaka 1984 alijiunga na michuano midogo ya mieleka ya World Class Championship Wrestling (WCCW) .

Miaka mitano baadaye (1989), alijiunga rasmi na World Championship Wrestling (WCW) na baada ya mwaka mmoja yaani 1990 alijiunga na World Wrestling Federation (WWF) na kukaa hapo kwa miaka 12 kabla ya mwaka 2002 kutimkia World Wrestling Entertainment (WWE) ambapo anasumbua mpaka leo.
IMEANDALIWA NA HEMED KISANDA
********************************








No comments: