African
Stars Band ambao wanajulikana pia kwa jina la “Twanga Pepeta”
walikuwa kivutio cha sherehe za miaka 50 ya Uhuru London juzi
Jumamosi. Kikosi hiki cha watumbuizaji maarufu wa Kibongo kilikaribishwa
na Urban Pulse, Jestina George wakishirikiana na Ubalozi wa Tanzania
mjini hapa.
Watanzania wa kila rika, nasaba na taaluma walifurika toka miji ya
Leeds, Bristol, Birmingham, Northampton, Milton Keynes na vitongoji
mbalimbali kufurahia vigongo vya bendi hili lenye makao makuu Mango,
Kinondoni Dar es Salaam.
Ukumbi wa Club 2000 Banqueting Suite ulioko nyuma ya uwanja maarufu wa
Wembley ulishuhudia tafrija hiyo wakati viongozi rasmi wa serikali
walipofungua tafrija wakicheza nyimbo maarufu za Kitanzania kama ule wa
mwanamuziki Salum Abdallah (“Wanawake wa Tanzania” na “Tujenge Nchi
Yetu”) marehemu alizoimba mara baada ya Uhuru mwaka 1961.
Viongozi waliojumuika walikuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na serikali za mitaa, Mheshimiwa Aggrey Mwanri, Balozi
wetu Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe, naibu wake Mheshimiwa
Chabaka Kilumanga na Ofisa Habari ndani ya ubalozi,Mheshimiwa Amos
Msanjila aliyehamasisha wageni kwa kunyofoa kinywaji cha “champagne”
mahsusi kuzindua maadhimisho.
Akiwakaribisha wote Balozi Kallaghe alisema sherehe za miaka 50 ni
idhinisho kuwa Tanzania ni nchi ya amani inayostahili kuwa fahari yetu
sote.
“Waangalie Waingereza wanavyoorodhesha tarehe na mida ya majengo yao
muhimu. Kutambua na kusherehekea muda kamili wa matukio ya jamii ni
jambo muhimu na la kawaida,” alikumbusha kiongozi huyo na kupigiwa
makofi.
Kutokana na maombi mengi ya washabiki Twanga Pepeta itafanya Show ya
pili siku ijumaa Tarehe 2 Desemba 2011 katika mji wa Milton Keynes
kwenye ukumbi wa Golden Lounge, Unit 35 Barton Road, Bletchley Milton
Keynes. MK2 3UH
No comments:
Post a Comment