Mwandaaji wa Shindano la Bongo Star Search
(BSS) Ritha Paulsen akisisitiza jambo wakati wa kikao cha tathimini cha
shindano hilo kilichofanyika mwishoni mwa wiki hii makao makuu ya BASATA. Kulia
ni Mratibu wa shindano hilo kutoka BASATA, Vick Temu.
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Muziki
Tanzania Che Mundugwao akitoa mchango wake kuhusu shindano la BSS wakati wa
kikao hicho cha Tathimini ya shindano hilo.
Che Mundugwao akiwa katika picha ya pamoja
na washindi wa BSS kwa mwaka 2011 Hadj Ramadhan (Kushoto) na Waziri Salum.
Na
Mwandishi Wetu
BARAZA la Sanaa la Taifa
(BASATA) limewataka wasanii waliotoka katika programu ya kusaka vipaji vya
muziki ya Bongo Star Search kuwa na mikakati ya kujiendeleza wenyewe ili
kufikia kilele cha mafanikio.
Wito huo ulitolewa jana na mratibu
wa BSS kutoka BASATA Vicky Temu wakati akichangia katika kikao cha tathimini ya
shindano hilo kilichofanyika Ukumbi wa BASATA mapema wiki hii.
Vicky alisema kuwa, wasanii
hao wanatakiwa kutambua kuwa uhusiano kati yao na shindano la BSS unalindwa na
kusimamiwa na mikataba wanayotiliana saini toka wanapoingia kwenye shindano
hilo hivyo inapofikia ukomo hawana budi kujipanga kwa ajili ya kujiendeleza
kisanaa.
“Wasanii wanaoshiriki BSS
wanapaswa kuwa na mikakati ya kujiendeleza baada kuwa wametambuliwa.Shindano
hili linawaibua kutoka chini hivyo lazima kuwe na daraja linalowafanya
wajiendeleze kisanaa” alisisitiza Bi. Temu.
Hata hivyo, wadau
waliochangia kwenye tathimini hiyo walimtaka mwandaaji wa shindano hilo Ritha
Paulsen kuangalia namna ya kujenga daraja la kuendeleza vipaji vinavyokuwa
vimepatikana kwani wengi wao wanatoka mikoani na hivyo kukosa mbinu za kuingia
kwenye soko la muziki.
Walimshauri awe na
utaratibu wa kuwaandalia semina na kozi fupifupi washiriki wa shindano hilo
zitakazolenga kuwaandaa kuingia kwenye soko la muziki lakini pia kuwa
wajasiliamali wazuri katika Sanaa.
“Washiriki wa BSS wanapokuwa kwenye kambi waandaliwe vema
kuingia kwenye soko la muziki. Wengi wao wanakosa mbinu na mikakati ya kuliteka
soko kutokana na kutoka mikoani hivyo wasaidiwe na wapewe mafunzo au elimu
katika eneo hili” alishauri Mjumbe.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu
wa Kitengo cha Matukio kutoka BASATA, Malimi Mashili aliwataka waandaaji wa BSS
kuhakikisha wanatekeleza maagizo mbalimbali waliyopewa kwa ajili ya kupatiwa
kibali cha kuendesha shindano hilo mwaka huu.
Maagizo waliyopewa
waandaaji hao ni pamoja na; kuwa na bajeti kamili ya shindano hilo, kuwekwa
wazi kwa zawadi za washindi, kuwepo kwa mikataba baina ya washiriki na BSS,
kuwasilisha majina ya majaji wa shindano hilo, uwezo wa BSS kuendesha shindano
hilo na maagizo mengine.
Akizungumza kwenye
tathimini hiyo, Mwandaaji wa shindano hilo Ritha Paulsen alisema kuwa, shindano
hilo limekuwa likimgharimu fedha nyingi lakini kwa kuwa limejikita kwenye
kuinua vipaji vya wasanii wachanga na anapenda kusaidia analazimika kufanya.
“Shindano hili tunalifanya
kwa gharama kubwa sana lakini tunajitahidi kusaidia wasanii wetu ili wafahamike
na baadaye wajisimamie katika kazi zao” alisisitiza Ritha.
Aliongeza kuwa, BSS imekuwa
ikijitahidi kusaidia wasanii katika kurekodi na kujiendeleza lakini changamoto
kubwa imekuwa kwa vyombo vya habari na wakuzaji sanaa (mapromota) kuwapokea
wasanii hawa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa na mtizamo hasi kuwa,
wasanii wanaotoka BSS wanakuwa na fedha nyingi.
Kuhusu maagizo aliyopewa na
BASATA aliahidi kuyafanyia kazi ilil kupewa kibali cha mwaka huu kwa ajili ya
mchakato wa shindano hilo kuanza mapema wiki hii.
No comments:
Post a Comment