HAYA ni moja ya maandiko yangu muhimu katika kazi yangu ya uandishi na uelimishaji jamii.
Ni kwa kutambua ukweli, kuwa nchi yetu imepatwa na
shambulizi la kigaidi. Imetokea Arusha, ingeweza kutokea popote pale katika
ardhi ya nchi yetu. Tunawapa pole wahanga wa tukio hili. Ni msiba wetu sote. Tuwe sasa na mioyo ya ustahamilivu. Tusikimbile kunyosheana vidole. Tuwaache
tuliowapa dhamana ya kuchunguza waifanye kazi yao. Wajibu wetu wa kizalendo ni
kutoa ushirikiano.
Naam, kama nchi, tunapitia sasa kwenye kipindi cha majaribu
makubwa. Huu ni wakati wa kuizunguka bendera yetu ya taifa. Ni wakati wa
kuonyesha umoja, uzalendo na mshikamano
wetu kama taifa. Umoja, uzalendo na
mshikamano wetu ni silaha muhimu na kubwa kabisa Watanzania tumeendelea
kuimiliki tangu enzi na enzi. Ndio silaha tunayoendelea kuimiliki hadi sasa.
Tuna lazima ya kupambana hadi risasi ya mwisho kuhakikisha adui hatupokonyi
silaha hii.
Ndugu zangu,
Hii ni Nchi Yetu. Ni nchi yetu sote, Watanzania wa
imani zote. Tutambue sasa, kuwa kwenye safari tunayokwenda kama taifa, mbele
yetu kuna mawimbi makubwa. Kwa pamoja
tutavuka, kwa kugawanyika tutazama.
Wahenga wetu walisema; kamba
hukatikia pabovu. Watanzania wa imani tofauti tuna historia ya kuchanganyika na
kuishi kwa amani na upendo. Hatuna hulka ya kubaguana. Tukianza sasa dhambi ya
kubaguana, basi, itaendelea kututafuna.
Na siku zote, uzoefu ni mwalimu mzuri .
Mathalan, uzoefu unatufundisha, kuwa kuwasha moto ni jambo jepesi sana, lakini,
kuuzima moto, ni kazi ngumu sana.
Ona, moto ulioanza kwenye
nyumba moja ya nyasi kijijini, waweza kusambaa haraka na hata kuteketeza kijiji
kizima. Na tangu utotoni tumetahadharishwa hatari ya kucheza na moto.
Naam, binadamu usicheze na moto, labda
iwe kwenye mazingaombwe.
Na ningependa hapa tuyakumbuke maneno ya busara na hekima nyingi
kutoka kwa Bi. Joy Mukanyange ( Pichani). Huyu alikuwa Balozi wa zamani wa
Rwanda nchini Tanzania. Mama huyu aliyatamka maneno haya miaka 13 iliyopita,
takribani miezi sita kabla ya kifo cha Baba wa Taifa. Bi. Joy Mukanyange
alikiona kile ambacho Watanzania hatukukiona. Ni kama vile alikuwa mtabiri,
maana, alichokisema mama yule leo ndio tunaanza kukiona. Siku ile ya Aprili 6,
1999, katika iliyokuwa Kilimanjaro Hotel, Bi Joy Mukanyanga aliyatamka haya;
” Naogopa, kwani nimeanza kuona
dalili zinazojengeka za mgawanyiko wa kidini nchini Tanzania na eneo lote la
Maziwa Makuu, hali ambayo inaweza kusababisha maauji ya halaiki kama yale
yaliyotokea nchini mwetu mwaka 1994.” Alisema Balozi yule wa Rwanda kabla ya
kuendelea kutoa ufafanuzi wa historia ya Rwanda na matukio yaliyosababisha
mauaji yale ya Wanyarwanda ya wao kwa wao. Ndio, Bi Joy Mukanyange alikiona
kile ambacho Watanzania hatukukiona.
Na tutafanya makosa makubwa, kama hata
sasa, tutajifanya kuwa hatukioni kile ambacho Balozi Joy Mukanyange alikiona .
Watanzania tukubali sasa kuwa tumepatwa na bahati mbaya sana ya baadhi ya
Watanzania wenzetu kuanza kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu. Kuna
wanaotaka tuanze kubaguana kwa misingi ya kidini.
Hili ni jambo la hatari sana. Ni
hulka ya mwanadamu, anapokuwa matatizoni kumtafuta kondoo wa kafara. Mtu
mwingine wa kummyooshea kidole kwa matatizo yake. Hali duni ya uchumi wa nchi,
hali duni za maisha na umasikini wa watu wetu isiwe chachu ya kuanzisha vurugu
za kijamii.
Maana, taratibu tumeanza kuizoea
misamiati ya sisi na wao. Mathalan, sisi Wakristo na wao Waislamu. Sisi
Wachagga na wao Wazaramo. Tunasahau, kuwa katika nchi yetu hii hakuna Sisi na
Wao, kuna SISI tu.Tutakapokumbwa na maafa ya kitaifa watakaoathirika ni SISI,
hakutakuwapo na WAO.
Hatari kubwa ninayoiona ni tatizo la
wengi wetu kuwa na ufahamu mdogo juu ya dunia tunayoishi sasa, kibaya zaidi,
ufahamu mdogo wa historia yetu. Hivyo basi, kupelekea hali ya kutojitambua kama
taifa.
Ndio, uelewa wa historia ya jamii husika
ni jambo muhimu sana. Kiumbe huwezi kuelewa ya leo, kesho na kesho kutwa kama
huelewi ya jana. Kuielewa historia yako ni kuelewa ulipo na unakokwenda.
Historia ni kama maji ya mto, yakipita hayarudi. Historia ni wakati, ni muda. Kihistoria
jana ni sawa na zamani.
Karne nyingi zilizopita wahenga wetu
walitafsiri muda kama mkusanyiko wa matukio ya zamani na sasa. Waliamini kuwa
yaliyotokea zamani na yanayotokea sasa ndiyo yenye kusaidia kubashiri
yatakayotea kesho, yataamua mustakabali wetu.
Dalili tunazoziona sasa za
kupandikiza mbegu za chuki kwa misingi ya udini si dalili njema. Haya
yatatupelekea kwenye maafa. Tuliopata bahati ya kutumia
kalamu zetu hatuna budi kuliweka hili hadharani. Ni wajibu wetu wa kizalendo.
Narudia, Hii ni Nchi Yetu. Katika ulimwengu
tunamoishi kuna mamilioni ya watu ambao hawana nchi. Wahenga wetu walishiriki
katika kuijenga nchi hii, wametutarajia sisi tuendelee kuijenga na kuilinda heshima
na hadhi ya nchi yetu. Mengine yanayofanyika sasa sio tu yanaitia doa nchi
yetu, bali, yanaiaibisha nchi yetu.
Ndugu zangu,
Hatuna haja ya kubaguana kwa misingi ya dini,
ukabila na rangi. Sisi wote ni Watanzania. Tuna historia ya kujivunia. Ni
historia yetu wenyewe. Kinyume na baadhi yetu wanavyofikiri au wanavyotutaka
tufikiri, historia yetu haikuanzia enzi za Mwarabu , Mjerumani au Mwingereza.
Historia yetu haikuanzia enzi za TANU wala Afro Shiraz.
Na dini hizi za kimapokeo
zinazotufanya sasa tufarakane zimekuja na kuzikuta dini zetu za asili, na bado
tunazo. Na hakika, Afrika hatugombanii matambiko. Afrika kila ukoo una tambiko
lake, hivyo basi, dini yake. Kamwe hutasikia Waafrika wanagombania matambiko.
Hutasikia Waafrika wakigombana kwa tofauti za matambiko yao.
Na sisi ni Waafrika. Hii leo mahala
ambapo unaweza kuwagawa Watanzania na hata kufanikiwa kuwafanya wachinjane ni kwenye kwenye tofauti zao za imani hizi
za kimapokeo; Uislamu na Ukristo.
Naam; kamba hukatikia
pabovu. Tusikubali dini iwe ndiyo penye ubovu kwenye kamba inayotuunganisha Watanzania.
Nahitimisha.
Maggid Mjengwa,
Msamvu, Morogoro.
0754 678 252, http://mjengwablog.co.tz
No comments:
Post a Comment