Thursday, September 19, 2013

Happy Birthday Mjengwablog; Miaka Saba, Na Tunasonga Mbele..!

Ndugu zangu,
Kwa mwanadamu, hakupaswi kuwapo na ukomo wa kujitahidi kufanya yalo mema kwa jamii yako.
Na katika kujitahidi kuyafanya yalo mema, basi, mwanadamu uwe tayari kukumbana na changamoto nyingi. Na kama  ilivyo kwa maji ya mto, yanapokutana na mwamba, basi, kasi yake huongezeka maradufu.
Leo blogu yako hii ya Mjengwablog imetimiza miaka saba. Miaka saba si haba. Ni umri wa mtoto kuanza shule.
Kwa niaba ya timu nzima ya Mjengwablog nachukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati ’ WanaFamilia’ wote wa Mjengwablog kwa kuwa nasi katika hali zote. Hivyo basi, kutuunga mkono.
Naam, ni miaka saba ya kuwa mtandaoni karibu katika kila siku inayotujia na kupita. Ni miaka saba ya mapambano magumu ya kuitumikia jamii na kuhakikisha kuwa tunabaki hai.
Maana, unapoamua kuitumikia jamii bila kuegemea upande, basi,  ina maana pia ya kujiweka  katika mazingira ya hatari sana.  Yumkini kuna maua mengi ya upendo yanaweza kurushwa kwako, lakini, kuna mishale michache ya sumu ambayo pia itarushwa kwako. Kwamba kuna maadui pia.
Na ukimwona nyani ametimiza miaka saba , basi, ujue kuna mishale  kadhaa ameikwepa. Lakini, na anavyozidi kuendelea kuishi, yumkini kuna mishale mingine inaandaliwa. Na nyani hatakiwi kuishi kwa kuogopa mishale ya wanadamu. Vinginevyo, ajitundike mtini, afe.
Lililo jema na kutia faraja ni kutambua, kuwa kuna walio wengi wenye kufaidika na kazi hii ya kijamii ambayo Mjengwablog inaifanya.  Ni hawa ndio wenye kututia nguvu ya kuendelea kuifanya kazi hii pamoja na changamoto zake nyingi.
Ndugu zangu,
Ilikuwa ni Jumanne, Septemba 19, 2006. Ni siku hiyo ndipo kwa mara ya kwanza niliingiza picha ya kwanza kwenye mjengwablog na kuashiria uzinduzi wa blogu. Ni picha hiyo inayoonekana hapo juu. Niliipiga eneo la Kinondoni Shamba. Tangu siku ya kwanza, niliweka wazi kwenye fikra zangu, kuwa Mjengwablog iwe jukwaa litakalomtanguliza mtu wa kawaida. Iwe sauti ya wale ambao sauti zao hazisikiki.
Na Mjengwablog ikawa chachu ya kuanzishwa kwa gazeti la michezo na burudani la ’ Gozi Spoti’, ikawa chachu pia ya kuanzishwa gazeti la ’ Kwanza Jamii’.
Na kuna miongoni mwetu wenye kufikiri, kuwa mwenye kumiliki gazeti ni lazima awe Mhindi au Mtanzania ’ mweusi’ Mfanyabiashara tajiri. Nakumbuka kuna hata ambao hawakuwa tayari kuchangia kiuandishi kwenye ’ Gozi Spoti’ na ’ Kwanza Jamii’ kwa vile linamilikiwa na ’ Mswahili mwenzao!’Na hata kupata matangazo kukawa na ugumu mkubwa. Gozi Spoti lilisimama kuchapwa baada ya mwaka mmoja mitaani. Kwanza Jamii, nalo likasimama kuchapwa. Likarudi tena baada ya kuingia  ubia na Shirika la Daraja. Baada ya miaka miwili na baada ya aliyepelekea kuingia ubia  kuondoka nchini na kurudi kwao Uingereza, basi, Kwanza Jamii nalo ’ likaandaliwa’ mazingira ya kuondoka mitaani.
 Hata hivyo, Kwanza Jamii, gazeti dogo, ambalo  naamini ni muhimu kwa jamii, limerudi tena kupitia mtandaoni. Mipango iko mbioni kuliimarisha zaidi katika siku zijazo.
Ndugu zangu,
Changamoto zipo ili tukabiliane nazo, na si kukata tamaa. Mjengwablog inatimiza miaka saba leo kwa vile  tulishaamua, kuwa  tutapambana hadi risasi ya mwisho. Hivyo pia, tutapambana hadi pumzi ya mwisho.

Maana, tunaamini kuwa kazi tuifanyayo ni yenye manufaa kwa jamii pana. Na tuna haki ya kuifanya. Tunavumilia sauti zenye kutushutumu na kutukosoa. Kuna tunayojifunza kutoka kwa wakosoaji wetu. Tunawashukuru sana na tunawaomba waendelee kutukosoa kila wanapoziona kasoro.
 Lakini, kuna wachache pia wenye kuonyesha zaidi chuki kuliko kukosoa.  Hawaipendi kazi tuifanyao wala kuithamini, ni kawaida. Lakini, faraja ni kutambua kuna wenye kuipenda na kuithamini kazi yetu.
 Hapa chini ni mmoja wa watu hao;
Maggid,
Iringa.
Wow. Siamini kama ni miaka saba tu. Mjengwa Blog was the first TZ blog that really hooked me. And it is still hooking me. In a blogging world fixated with celebrity, gossip and slander, Mjengwa Blog is a rare and fresh piece of sanity with a window onto the real Tanzania. Bravo Mwenye Kiti, umefanya kazi kubwa hadi hapo ulipo. Na wala usipate wazo lolote lile la kustaafu. Wanakijiji wenzako bado tunakuhitaji na kukutegemea uendelee hivyo hivyo. Aluta continua...
 Jimmy Innes ( UK)
 Ahsanteni sana.
 Maggid Mjengwa.
Mwenyekiti Mtendaji.
Mjengwablog.com

No comments: