Saturday, February 7, 2015

MAHAKAMA: MACHA MNUNUZI HALALI NYUMBA YA BALENGA


NA MWANDISHI WETU
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imethibitisha kwamba mfanyabiashara Hans Macha alinunua nyumba kwa kufuata utaratibu na kihalali kutoka kwa Ramadhani Balenga.

Hayo yalithibitishwa kupitia hukumu iliyosomwa na Hakimu Mkazi Frank Moshi kwa niaba ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka, ambaye alisikiliza kesi ya kughushi inayomkabili Macha.

Katika kesi hiyo, Macha alikuwa akikabiliwa na mashitaka matatu ya kughushi hati ya umiliki wa kiwanja kilichopo eneo ya Kigogo, Dar es Salaam, kinachodaiwa kuwa mmiliki wake ni Ramadhani Balenga.

Pia alikuwa anadaiwa  kughushi mkataba wa mauziano wa eneo hilo kuonyesha kwamba Balenga alihamisha umiliki wa kiwanja hicho kwenda kwake na kuwasilisha nyaraka ya kughushi.

"Mahakama imepata muda wa kutosha wa kupitia ushahidi na vielelezo vyote. Makosa yote matatu hayajathibitishwa ipasavyo. Mlalamikaji  (Balenga), alimuuzia mshitakiwa eneo hilo kwa kufuata utaratibu na kihalali," alisema Hakimu huyo.

Alisema mahakama inamuachia mshitakiwa kwa mashitaka yote matatu na mlalamikaji ana nafasi ya kukata rufani.

Baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Nassoro Katunga, aliuliza iwapo nakala ya hukumu ipo tayari, ambapo Hakimu Moshi alimwambia haipo tayari na kama wanaitaka wafuate taratibu kwa kuwasilisha maombi mahakamani hapo.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliita mashahidi na upande wa utetezi ulileta mashahidi takriban 10 akiwemo mshitakiwa mwenyewe na aliyekuwa mke wa mlalamikaji Balenga, Nury Ahmadi.

Baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wao, Novemba, mwaka jana, mahakama hiyo ilimuona Macha ana kesi ya kujibu nahivyo kutakiwa kuwasilisha utetezi wake.

Wakati akijitetea mfanyabiashara Macha alidai tuhuma zinazomkabili ni za uongo na kuiomba mahakama kumuachia huru.

Katika utetezi wake, mfanyabiashara Macha aliiomba mahakama huyo kutupilia mbali mashitaka hayo kwa kuwa tuhuma hizo ni za uongo na Balenga anajua wazi kwamba alimuuzia hiyo nyumba namba 183 kitalu A iliyoko Kigogo.

Akiongozwa na Wakili Deo Ringia, Macha alidai alikuwa akimkopesha Balenga fedha huku akiweka dhamana hati za nyumba, hadi deni lilipofikia sh. milioni 879  ambalo hakuwahi kulilipa.

"Baada ya kushindwa kulilipa nilipomuuliza aliniambia makontena yake yalikamatwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hivyo hakuwa na fedha ya kunilipa tena.

"Alinijulisha ana hati nyingine ya nyumba ya ghorofa tano iliyoko Kigogo, hivyo aniuzie na nyumb nyingine ya Manzese ambayo hati yake nilikuwa nayo na nimuongeze na sh. milioni 20," alidai

Macha alidai Balenga alimuambia  nyumba ya Kigogo,  amekopea mkopo benki ya Azania, hivvyo hati ipo huko na kumwahidi ataenda kuitoa ili wabadilishane kwa kumuuzia hiyo nyumba na kumuongezea sh. milioni 20  na baada ya hapo amrudishie hati nyingine nne alizokuwa amezishikilia.

"Makubaliano hayo tuliweka maandishi ya mauziano baada ya kuletya hati yake ya Kigogo. Hiyo ilikuwa mwaka 2011, nyaraka ya mauziano nakumbuka ilikuwa mkataba wa mauziano na pande zote mbili mimi na Balenga tulitia saini ofisini kwangu katika hoteli ya Rick Hill, iliyoko mtaa wa Kipata, Mnazi Mmoja, Dar es Salaam," alidai

Alidai wakati wanatiliana saini kulikuwa na mashahidi ambao ni Mashaka (mjomba wa Balenga), David (rafiki wa Balenga) na John Mboya na mkataba huo ulishuhudiwa na wakili Henry Mkumbi  ambaye aligonga mhuri baada ya kumueleza makubaliano yao  na alimkabidhi Balenga sh. milioni 20 mbele ya wakili huyo.

Macha alidai baada ya mauziano walitia saini hati ya kubadilisha umiliki na Balenga alimkabidhi nyaraka nyingine zinazohusiano na jengo hilo zikiwemo kibali halisi cha ujenzi, ofa ya jengo, michoro halisi ya jengo inayotoka Manispaa, mkataba alioingia na mjenzi na risiti mbalimbali.

Alipoulizwa na wakili anaielezeaje mahakama kuhusu madai ya Balenga kwamba hajamuuzia nyumba hiyo, Macha alidai ni ya uongo kwa kuwa alimuuzia na Balenga anajua kwamba alimuuzua hiyo nyumba.

Shahidi mwingine alikuwa aliyekuwa mke wa Balenga, Nury Ahmadi ambaye aliieleza mahakama kuwa mlalamikaji alimtamkia kwamba amemuuzia nyumba Macha.

Mashahidi wengine wa upande wa utetezi walikuwa mawakili wa kujitegemea Henry Mkumbi na Castro Rweikiza, ambao walidai walishuhudia utiliaji saini wa mkataba wa mauziano  baina ya Balenga akiwa muuzaji na Macha mununuzi na hati ya kuhamisha umiliki. Walidai katika nyaraka hizo, wao walitia saini na kugonga mihuri ya ofisi zao.

No comments: