Wednesday, February 4, 2015

OLOLOSOKWAN WAPIGWA MSASA KUKITUMIA VYEMA KIJIJI CHA DIJITALI

DSC_0022
Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Bw. Al Amin Yusuph akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues (aliyeipa mgongo kamera) wakati wa ukaguzi wa mwisho wa eneo la mradi wa kijiji cha digitali wa Samsung unaoendeshwa na UNESCO lilitolewa na serikali ya kijiji. Katikati ni Mwenyekiti wa kijiji cha Ololosokwan wilaya ya Ngorongoro, Kerry Dukunyi .(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog)
Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
SHIRIKA la Elimu ,sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, limeanza maandalizi ya kuumilikisha mradi wa kijiji cha digitali cha Ololosokwan kwa wananchi wa kijiji hicho kwa kuendesha warsha ya siku mbili ya kutambua vipaumbele vya wananchi vitakavyoingizwa katika mradi huo.
Vipaumbele hivyo ni katika elimu, afya na uchumi.
Warsha hiyo ilishikirikisha wanakijiji wa Ololosokwan na vijiji vingine vinavyozunguka kijiji hicho,viongozi wa halmashauri, viongozi wa kimila, viongozi wa vijiji na wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya, elimu na uchumi.
Katika majadiliano yao wananchi walitambua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na mazingira na mfumo wa utamaduni walionao wakazi wa eneo hilo.
DSC_0042
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akikagua eneo la mradi wa kijiji cha kidigitali Ololosokwani wilayani Ngorongro. Kushoto ni Mwenyekiti wa kijiji cha Ololosokwan, Kerry Dukunyi na Mratibu wa miradi wa Taasisi ya Irkiramat, Salanga Mako.
Wakazi hao ambao ni wafugaji wenye kuheshimu mila na utamaduni wa kimasai na mfumo wa maisha wamesema kwamba lugha inayotumika katika kufundishia ni tatizo na ingawa wana shule mbili za msingi na sekondari lugha ya Kiswahili ni tatizo na wakifika sekondari lugha ya kiingereza nayo inakuwa tatizo.
Aidha walisema kutokana na wazazi kutokuwa na elimu hawaoni sababu ya kuwafanya watoto wao wenye maarifa makubwa kwenda shule na badala yake hao wanaoelewa vitu hupelekwa kuchunga au wale wenye umri mdogo wa kike huolewa.
Warsha hiyo pia ilibainisha tatizo la afya ya wanawake na watoto, ndoa za utotoni na magonjwa ya zinaa ya kuambukiza.
DSC_0047
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akiteta jambo na ujumbe wake aliombatana nao kwenye kijiji cha Ololosokwan kwa ajili ya kuwapiga msasa wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni maadalizi ya kupokea mradi wa kijiji cha kidigitali hivi karibuni.
Kijiji hicho cha digitali ambacho ni nadharia ya Samsung katika kurejesha faida kwa umma kitakuwa na huduma mbalimbali ambazo zikiunganishwa na haja ya wananchi zitasaidia kubadili maisha ya wamasai na kuondokana na utegemezi wa mifugo pekee na kutambua thamani yao katika rasilimali zilizopo katika maeneo yao.
Warsha hiyo ambayo imesimiwa na wataalamu kutoka UNESCO imelenga kuwafungua macho na kuwashirikisha wananchi kuhusu mradi huo mkubwa wa aina yake nchini na duniani.
Kijiji cha dijitali nchini Tanzania ni cha nne cha kwanza kikiwa nchini Afrika Kusini, kingine Gabon na Ethiopia.
DSC_0060
Baadhi ya wanakijiji wa Ololosokwan na vijiji vingine vinavyozunguka kijiji hicho,viongozi wa halmashauri, viongozi wa kimila, viongozi wa vijiji na wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya, elimu na uchumi wakimsikiliza Mkurugenzi mkazi wa UNESCO, Zulmira Rodrigues (hayupo pichani).
Kijiji hicho ili kiwe endelevu wananchi wanaohusika wanatakiwa kuelewa mradi huo kuweka vipaumbele vyao na kuangalia jinsi ya kutumia mradi huo katika kukabili changamoto zinazowakabili kwa sasa.
Katika majadiliano kwenye ngazi za elimu wananchi walielezea haja ya kushawishi wamasai kuanza kujifunza Kiswahili na Kiingereza ili kuweza kufuatilia kwa karibu masomo na pia kuwepo kwa sheria ndogo ili kuzuia utoro wa wanafunzi kwa ajili ya kwenda kuchunga mifugo na pia kuolewa mapema kwa mabinti.
Mathias Herman, mratibu wa program za Afya , UNESCO, alisema kwamba pamoja na kwamba kijiji hicho kitakuwa na zahanati na huduma za mawasiliano ya tiba (telemedicine) hamasa kubwa inatakiwa kutolewa ili wananchi waweze kutumia huduma hizo kwani kwa sasa wamejikita zaidi huduma za waganga wa jadi.
DSC_0066
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akiendesha mjadala kwa wanakijiji wa Ololosokwan na vijiji vingine vinavyozunguka kijiji hicho,viongozi wa halmashauri, viongozi wa kimila, viongozi wa vijiji na wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya, elimu na uchumi ikiwa ni maandalizi ya kuupokea mradi wa kijiji cha kidigitali Ololosokwani wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.
Alisema katika warsha kulielezwa kuwa kukosekana kwa madaktari katika zahanati zilizopo kijijini hapo kumefanya watu wengi kuendelea kuamini waganga wa jadi na kujifungulia huko hali ambayo imezaa kuwapo kwa idadi kubwa ya wanawake wanaokufa wakati wa uzazi na pia watoto wasiopata chanjo.
“Wakifika hakuna madaktari hawawezi kuamini huduma hii wakati kuna waganga wa kienyeji na wakunga wa kienyeji” alisema Mathias na kuongeza kuwa katika warsha ilihimizwa kwamba watu watambue tatizo lililopo la kiafya linalosababishwa na mfumo wa mazingira na maisha ya wafugaji na kuhakikisha kwamba huduma zinazoletwa zinatumiwa vyema.
Aidha alisema kuwapo kwa kiwango kikubwa cha maambukizi ya magonjwa ya zinaa, ndoa za utotoni na mimba katika umri mdogo ni sehemu ya matatizo ambayo yanaaminika kwamba yanaweza kutanzuliwa kwa kutolewa elimu na kushawishi wakubwa wa mila kutambua nafasi zao na elimu ya kisasa katika kushughulikia changamoto za kiafya.
DSC_0095
Afisa mipango ya Elimu wa Shirika la UNESCO, Bi. Jennifer Kotta (kulia) akiwa kwenye majadiliano na baadhi ya wanakijiji wa Ololosokwan kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu na nini kifanyike kuboresha sekta ya elimu kwa ujumla katika kijiji hicho na kuishirikisha halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro katika maandalizi ya kupokea mradi wa kijiji cha kidigitali.
“mila na heshima kwa wakubwa wa mila kumefanya wamasai kutegemea tiba za asili na mfumo wa asili wa kuendesha maisha bila kujua athari kwao ziwe hasi au chanya” alisema Mathias kauli iliyoungwa mkono na Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO, Zulmira Rodrigues ambaye alisema kunahitajika sana ushirikiano wa jamii, viongozi, wazazi kuhakikisha kwamba kijiji kinafanikiwa na kuwa cha kupigiwa mfano.
Kijiji cha Ololosokwan kilichopo Loliondo, wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kikiwa na watu 9000 kupitia mradi huo kitapewa pia mbinu za kuimarisha soko la utalii, kulitambua na kulitumia kwa manufaa yao na pia elimu ya ubunifu ambayo itawafanya wanawake wanaotengeneza urembo mbalimbali kuweza kumudu soko la utalii na la kawaida.
DSC_0103
Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Bw. Al Amin Yusuph akiendesha mjadala na baadhi ya wanakijiji wa Ololosokwan kuhusiana mradi wa kijiji cha kidigitali na kuuboresha ili kutatua matatizo ya wananchi pamoja na kuwapata taarifa za maendeleo kupitia redio jamii ya Loliondo FM inayofadhiliwa na UNESCO ikiwa ni katika maandalizi ya kuupokea mradi huo wa kijiji hicho unaotarajiwa kuwasili hivi karibuni kijijini hapo.
Aidha mradi huo utafikisha umeme na elimu kwa njia ya Tehama huku, elimu hiyo ya Tehama ikikusudiwa kutumika kutoa elimu ya darasani kwa wanafunzi ambao wapo machungani.
Mfumo wa wamasai ambao umejengwa katika utamaduni na kuthamini mifugo unatakiwa kubadilishwa kwa wazazi kupewa elimu ya kuwawezesha kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wao.
DSC_0163
DSC_0145
Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias akiongoza mjadala wa nini kifanyike katika kuboresha sekta ya afya na changamoto zinazowakabili wanakijiji wa Ololosokwan kwa ajili ya maandalizi ya kuupokea mradi wa kijiji cha Kidigitali unaoendeshwa na UNESCO kwa kushirikiana na kampuni ya Ki-elektroniki ya Samsung unaotarajiwa kuwasili mapema mwezi februari kijijini hapo. Wa pili kushoto ni Mratibu wa Taifa wa tiba asilia na mbadala katika Idara ya Tiba Wizara ya Afya na ustawi wa jamii. Dkt Liggy Vumilia.
DSC_0226
Afisa mipango ya Elimu wa Shirika la UNESCO, Bi. Jennifer Kotta akiwasilisha kazi ya kikundi chake baada ya kujadiliana na wanakijiji wa Ololosokwan katika kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni maandali ya kupokea mradi wa kijiji cha kidigitali kinachotarajiwa kuwasili hivi karibuni kijijini hapo.
DSC_0124
Mmoja wa washiriki wa kikundi kilichokuwa kikijadili masuala ya utamaduni na utalii akiandika changamato mbalimbali zinazowakabili wakinamama wakimasai wanaofanya biashara za urembo wa kimasai kwa watalii wanaotembelea hifadhi ya Ngorongoro.
DSC_0089
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akishiriki kwenye mjadala na wanakijiji wa kijiji cha Ololosokwan katika maandalizi ya kupokea mradi wa kijiji cha kidigitali unaotarajiwa kuwasili mapema mwezi februari kijiji hapo.
DSC_0231
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akisaini mkataba wa kukabidhiwa ardhi iliyotolewa na serikali ya kijiji kwa ajili ya mradi wa kijiji cha kidigitali huku tukio hilo likishishudiwa na uongozi wa juu wa serikali ya kijiji, wataalam kutoka UNESCO na halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro pamoja na wanakijiji.

No comments: