Wednesday, February 25, 2015

SIMU ZA OBI MOBILES ZAINGIA TANZANIA

S550-Crane-1
Simu ya Obi aina ya S550-Crane.
Na Mwandishi Wetu
MWANZILISHI mwenza wa kampuni ya kimataifa ya teknolojia ya mawasiliano ya Obi Mobiles, yenye makao makuu yake Singapore, John Sculley amesema ujio wa kampuni hiyo nchini Tanzania, utaongeza wigo wa utumiaji wa tehama na hasa matumizi ya zana za kisasa za mawasiliano.
Obi Mobile inatumia teknolojia iliyobuniwa mjini Toronto, Canada na kampuni ya Inflexionpoint.
John Sculley, ambaye alishawahi kuwa ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Apple amesema teknolojia hiyo mpya ambayo ilizinduliwa India na Mashariki ya Kati mwaka 2014 imelenga kuwanufaisha vijana ambao ndio watumiaji wa kubwa wa simu za kisasa.
Amesema kwa kuingiza bidhaa za Obi nchini Tanzania wanatarajia kuwawezesha vijana kuwa na simu ambazo zinawatumikia wao kwa maarifa na umaridadi zaidi.
S550-Hornbill-2
S550-Hornbill.
“Simu hizi zimepokewa vyema zilikozinduliwa na tunararajia Tanzania nazo watazipokea kwa kasi hiyo hiyo” alisema Sculley .
Kwa mujibu wa ofisa huyo, simu za Mobile nchini Tanzania zinauzwa kati ya sh 50,000 na bei ya juu ni 350,000.
Alizitaja aina hizo za simu kuwa ni Hornbill S551; Falcon S451; Crane S550; Wolverine S501; Fox S453 ; Racoon S401 na Power GO F240 simu ambayo ina betri yenye uwezo wa 2,800mAH na yenye uwezo wa kuchaji simu nyingine.
Amesema watu wa Obi Mobiles wanaamini kwamba teknolojia ni kwa ajili ya watu wote na ndio maana mauzo ya teknolojia zao ni rahisi kwa ajili ya watu wote.
Alisema kwa kuwa na vifaa vya teknolojia ya Obi, vijana watakuwa na nafasi ya kutumia fursa zilizopo za kiuchumi na kijamii.
S453-Fox-1
S453-Fox
Sculley amesema kwa muono wake teknolojia haitakiwi kuwa ngumu kuitumia wala kutengeneza changamoto kwa watumiaji wake kwa kuiwekea vikwazo.
Teknolojia za Obi Mobile zinazotumia mfumo wa Android ni za daraja la juu na wkamba simu zote za Obi zilizoingizwa nchini zina uwezo wa kuwa na intaneti.
Kampuni hiyo inatarajia kuzindua simu hizo nchini Tanzania mwezi ujao .
Akizungumzia mkakati wa kampuni hiyo kwa bara la Afrika , Mkurugenzi Mtendaji wa Obi Mobile MENA, Amit Rupchandani: “Walaji wengi wanataka kujiondoa katika simu za kawaida kwenda katika simu za kisasa. Hata hivyo,gharama za uwekezaji katika teknolojia ya kisasa ni kikwazo kikubwa kwa watu wengi.”
Obi Mobiles, wamesema kwamba kwa kuelewa hilo, wamewezesha kuwa na simu zenye uwezo mkubwa na kwa bei nafuu ili kufikia kila kundi katika bara la Afrika.
Simu hizi ambazo vijana watazipenda zimeelezwa kutengenezwa kumudu maisha yao na kuwapendezesha.

No comments: