Saturday, November 7, 2015

BARUA KALI KWA CCM NA WATANZANIA WOTE

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi.
Ndugu zangu. Watanzania wenzangu,
Kwanza kabisa nawapongezeni kwa amani na utulivu mliouonyesha katika mchakato wote wa Uchaguzi Mkuu ambao ulimalizika salama na hatimaye jana Rais wa Awamu wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli aliapishwa mbele ya macho yangu na ya Watanzania wengine wengi.

Hakika tumeuthibitishia ulimwengu kwamba, sisi Watanzania ni tofauti na wao, tunao uwezo wa kuvuka kwenye nyakati ngumu lakini bado tukabaki wamoja tukiishi pamoja kwa upendo kama ndugu, msingi uliojengwa na wazee wetu wa mwanzo ambao kuubomoa si kazi rahisi, kwa hili nawapongeza Watanzania wote na ninamwomba Mungu awasaidie wenzetu wa Zanzibar waweze kufikia muafaka utakaoleta utulivu wa taifa zima.


Baada ya kusema hayo niendeleze barua yangu niliyoianza wiki iliyopita kwa Chama Cha Mapinduzi na Watanzania wote, hilo ndilo dhumuni la barua hii, kuendeleza pale nilipokomea! Leo nataka kuongea baadhi ya mambo niliyoyaona kama udhaifu mkubwa kwa Chama Cha Mapinduzi kwenye mchakato mzima uliohitimishwa Oktoba 25, 2015 kwa wananchi kupiga kura. Naomba nianze na suala zima la moyo wa kujitolea katika chama, ndugu zangu hili ni jambo la kusikitisha mno katika Chama Cha Mapinduzi, nina imani wengi wamelishuhudia! Moyo wa kujitolea ndani ya Chama Cha Mapinduzi umekufa kabisa, kama haujafa basi upo chumba cha huduma kwa wagonjwa mahututi (ICU), kila kitu ndani ya chama hiki kikubwa kimekuwa POSHO, POSHO, POSHO! Bila posho ndani ya Chama Cha Mapinduzi hakuna kinachofanyika, moyo wa kujitolea ambao waasisi wa chama hiki waliupandikiza wakati wa kutafuta uhuru umekufa.

Wakati katika muungano wa vyama vya upinzani, vijana walikuwa wamehamasika, wakifanya kazi kwa kujitolea, lengo lao likiwa ni moja tu; kuing’oa CCM madarakani, mimi nilishuhudia wanaCCM, wengine viongozi kabisa wamekaa chini bila kufanya chochote wakisema “Tufanye nini sasa hakuna posho?”

Kwangu mimi hii ilikuwa ni aibu, mwanaCCM anashindwa kuondoka nyumbani kwake na kwenda kuhamasisha nyumba kwa nyumba akishawishi wapiga kura eti hawajaletewa fedha kutoka wilayani au makao makuu, bila posho ndani ya CCM hakuna kinachofanyika, jambo hili inabidi lishughulikiwe, moyo wa kujitolea na uzalendo kwa chama ni lazima ufufuliwe, hii ni kazi ya Mwenyekiti wa CCM. Inawezakanaje vijana wa 4U Movement (marafiki wa Lowassa) waliojiunga nchi nzima eti wafanye kazi kubwa za kututisha kuliko jumuia za Chama Cha Mapinduzi kama ya wazazi, UWT na vijana ambazo zina mitandao mpaka vijijini kabisa? 4U Movement wanawezaje kufanya kazi kubwa ya kutetemesha kama jumuiya zetu hizi zina moyo wa kujitolea? Jibu ni moja tu hapa, moyo huo umekufa sababu ya posho, vijana wetu hawafanyi chochote mpaka wapewe posho na chama au mgombea.

Simaanishi kwamba watu wote katika jumuiya hizi hawakufanya kazi, lakini hata wewe msomaji kama ni mwanachama wa CCM, unaelewa kabisa ninachokizungumzia hapa ni nini na iko sababu kubwa sana ya kufufua moyo wa uzalendo na kujitolea ndani ya chama hiki badala ya kuacha jambo hilo lifanywe na vyama vya upinzani. Jambo jingine ni UNAFIKI na HUJUMA ndani ya chama, hakika tabia hizi mbili zimekiathiri sana Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi huu. Nasema bila kupindisha, zimepunguza mno kura za chama hiki. Kuna unafiki mno ndani ya CCM, watu sio wa kweli, wanavaa shati la kijani mchana lakini wanavaa ngwanda la khaki usiku! Hii ni aibu, wengine ni viongozi wa chama ngazi za wilaya, walishindwa hata kumuombea kura mgombea urais wa chama chao kwa sababu walishajiunganisha na kambi ya pili.

Hawa ndiyo walioendesha hujuma kukikwamisha chama kisipate ushindi lakini ashinde mtu waliyemtaka hata kama ni wa chama pinzani, tukubali tukatae, jambo hili lipo na ni lazima lishughulikiwe haraka iwezekanavyo kwa usalama na ustawi wa chama, kuendelea kuwafumbia macho watu wa aina hii itakigharimu chama kwenye uchaguzi utakaofuata. Inawezekanaje kiongozi wa chama akapelekewa kofia na tisheti za Chama Cha Mapinduzi halafu akaacha kuzigawa wakati anazo stoo? Inawezekanaje akapewa posho za mabalozi halafu akaamua kutowagawia au kukata nusu ya kiwango alichopewa? Wakati akifayafanya haya anajua kabisa kwamba kambi ya pili ya upinzani inagawa tisheti na kofia zake na kubandika bendera kila mahali jimboni. Je, hii si hujuma?
Ndugu zangu,

Niongelee mikakati, tumejitahidi sana kupambana kwenye uchaguzi huu, naomba niwasifu watu waliokuwa kwenye kitengo cha teknohama (IT) wamefanya kazi kubwa mno kupambana na vijana wa 4U Movement, kampeni za safari hii ziliendeshwa kisasa na zilikuwa na nguvu kubwa sana kwenye mitandao ya kijamii, kazi kubwa imefanywa na vijana wetu. Lakini jambo lililonisikitisha ni kwa nini tulikuwa mara nyingi tunakuwa wafuasi, badala ya kuwa viongozi kwenye mikakati? Mfano Ukawa wakibandika bendera zao nyingi mitaani ndiyo na sisi tunafuata nyuma yao, kwa nini hatukuwa watu wa kwanza na Ukawa wakafuata nyuma? Naamini sana kwenye msemo wa Steve Jobs usemao “Be a leader, not a follower!” daima uwe kiongozi siyo mfuasi. Ilifika mahali ikaanza kuonekana kama timu ya Ukawa ilikuwa na watu hatari katika mikakati kuliko sisi, jambo ambalo kwangu mimi halikunifurahisha na ninadhani halikuwafurahisha wengi, kuna jambo la kujifunza hapa, siku zote tuwapo katika mapambano tusiwe watu wa kusitasita, bali tuwe watu wa kuchukua hatua za kutekeleza mawazo yetu mara moja.

Ndugu zangu,
Sitaweza kumaliza barua hii bila kukikumbusha Chama Cha Mapinduzi juu ya kubadilisha taswira yake kwa jamii, kisitishe mara moja tafsiri ya kwamba ni chama cha matajiri na kurejea kwenye chama cha wakulima na wafanyakazi ili kila Mtanzania mwenye sifa aweze kujitokeza na atakapofanya hivyo na watu wanamkubali, apewe nafasi ya kutumikia nchi yake, asilazimishwe tu mtu kugombea hata kama hakubaliki, sababu tu ni mkongwe katika chama au ni waziri, hili limeigharimu CCM majimbo mengi safari hii, kosa hili halitakiwi kuendelea kutendwa. Katika hili ni mpango mzima wa kutayarisha viongozi wa kesho, waliopo leo ni lazima wataondoka, nafasi zao zitachukuliwa na akina nani? Lazima kuwe na ‘succession plan’ ya kwamba kizazi hiki kikiondoka, kitaingia hiki! Nionavyo mimi jambo hili halifanyiki na kama linafanyika basi si kwa kiwango kisichotarajiwa.

Lazima kuwe na “First in, first out!” yaani wa kwanza kuingia awe wa kwanza kutoka ili kupisha wengine, ningefurahi na nitafurahi sana kuona vijana wengi wanachukua nafasi za waliotangulia katika chama chetu ili kuingiza mawazo ya kizazi cha sasa, badala ya chama chetu kuendelea kutafsiriwa kama chama cha wazee kama ilivyo leo. Yapo mengi nitakayoyaongea kwa kirefu kwenye kitabu nitakachotoa cha kuirekebisha CCM kwa lengo la kuijenga si kuibomoa, bado chama hiki ni chama chenye nguvu na kinaaminiwa na watu wengi, tukikiacha kiende kama kinavyokwenda sasa mwisho wa siku watu watakuja kupoteza imani nacho na kitakufa kama vilivyokufa vyama vingine vilivyoleta uhuru katika nchi nyingine Afrika, jambo hili sipendi litokee ndiyo maana nitaandika kitabu hicho.

Baada ya kusema haya, nimalizie barua yangu kwa kumpongeza Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuapishwa kuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimtakie utendaji mwema wa kazi katika kuhakikisha anazitimiza ahadi alizotoa, Watanzania wanatarajia kutoka kwake; huduma bora za afya, upatikanaji wa maji safi na salama, elimu bora kwa kila Mtanzania, kutokomeza ufisadi,Tanzania yenye viwanda, miundombinu bora, amani na umoja wao kuendelea kuwepo.
Haya na mengine mengi yakifanyika, Watanzania wakafaidi utajiri ambao Mungu amewapa, naomba nimhakikishie mheshimiwa rais ya kwamba miaka mitano ijayo atachaguliwa tena, lakini hayo yasipofanyika, NINA MASHAKA.
Ahsanteni.
Wasalaam,
Eric Shigongo James

No comments: