Mheshimiwa Spika;
Niko hapa leo
kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91
Ibara ndogo ya kwanza inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi Bunge hili.
Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na
kutuwezesha kuwepo hapa siku ya leo. Aidha nitumie fursa hii kuwakumbuka wenzetu
ambao, kwa namna na nafasi mbalimbali, walishiriki katika mchakato wa uchaguzi
huu na kwa bahati mbaya walipoteza maisha yao kabla ya mchakato haujakamilika.
Kwa hao wote waliotangulia mbele za haki ninamuomba Mwenyezi Mungu azirehemu
roho zao na awape pumziko la amani. Nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu na
jamaa ambao ndugu zao walifariki na wengine kupata ulemavu wakati wa mchakato
wa uchaguzi huu.
Pia natoa pongezi
kwako wewe Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Ackson
Tulia kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge letu la 11. Waheshimiwa Wabunge wamewapa
imani yao, na mimi kwa nafasi yangu nawahakikishia imani na matumaini yangu
makubwa kwenu. Sina shaka Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wako Bunge letu
limepata kiongozi mahiri, makini na mweledi.
Aidha, niwapongeze
Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge hili la 11. Aidha, nitumie
nafasi hii kuwapongeza wale wote waliochaguliwa katika nafasi za udiwani katika
kata mbalimbali kote nchini. Natoa pongezi hizi kwa dhati kabisa kabisa kwa
sababu kuu mbili:
·
Kwanza,
ni kwa sababu ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni mkubwa sana
kuanzia ndani ya vyama vyetu na baadae katika Uchaguzi Mkuu uliohusisha na
kushindanisha wagombea toka vyama tofauti.
·
Pili,
nawapongeza kwa sababu wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha
katika kipindi ambacho matarajio yao kwa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu
ni makubwa sana. Watatupima kwa namna tutakavyokidhi kiu na matarajio yao. Sote
tuliahidi kuwatumikia wananchi, na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze
kutatua matatizo yao mbalimbali, na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji,
usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali za taifa, na ugawaji wa
rasilimali hizo kwa haki. Mimi na Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais
tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na tutahakikisha kuwa katika utumishi wetu
tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida. Naamini wenzangu
pia ndicho mlichoahidi na daima tukumbuke kuwa kazi zetu na mipango yetu yote
tutakayoipanga na kuisimamia italenga katika kuwanufaisha watu wetu.
Mheshimiwa Spika;
Niwahakikishie tu
wananchi kuwa mambo tuliyowaahidi tutayatekeleza. Sikusudii kurejea mambo yote
niliyoahidi katika hotuba yangu hii ya leo, lakini nataka niwatoe wasiwasi kabisa
kwamba tuliyoahidi tumeahidi na ahadi ni deni. Nataka Wananchi mniamini kuwa
sikutoa ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi kuwatumikia na kuwafanyia kazi,
na hicho ndicho nitakachofanya. Ni imani yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge na
Madiwani pia watafanya hivyo hivyo kama tutakavyofanya sisi.
Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kabisa
kwa Watanzania wote. Tulijiandikisha kwa wingi sana kwa ajili ya kupiga kura,
tulishiriki na kufuatilia kwa karibu sana kampeni za uchaguzi, na tukajitokeza
kwa wingi siku ya kupiga kura. Kinyume na ilivyotabiriwa na wasio tutakia mema
hakuna siku iliyokuwa na utulivu mkubwa na amani kama siku ya tarehe 25 Oktoba
tulivyokwenda kupiga kura. Hata baada ya matokeo kuanza kutangazwa tulionyesha
utulivu mkubwa, na hata pale ambapo matokeo yalipotangazwa na yakawa sivyo
baadhi yetu walivyoyatarajia bado tuliyapokea kwa hali ya utulivu na uungwana
mkubwa.
Wale waliotarajia
kuwa tutafarakana wameondoka wakiwa wamefadhaika sana huku wakijiuliza hivi
hawa Watanzania ni Waafrika wa namna gani. Ndugu zangu Watanzania, kwa mara
nyingine tena tumedhihirisha, kwetu sisi wenyewe, kwa Afrika na dunia, kwamba
sisi ni kisiwa cha Amani katika bahari iliyochafuka. Tunayo haja ya kujipongeza
na kujiwekea nadhiri kuwa tuaendelea kuidumisha hali hii na kuilinda amani ya
nchi yetu. Ombi langu kwa vyama vya siasa, wanasiasa wa vyama vyote na viongozi
wa dini ni kutimiza wajibu wetu wa kuilea amani ya nchi yetu.
Aidha, napenda
niungane na ninyi pamoja na Watanzania wote kuvipongeza vyombo vyetu vya Ulinzi
na Usalama (Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji na
Usalama wa Taifa pamoja na mgambo) kwa jinsi walivyoshiriki katika kuhakikisha
nchi yetu inaendelea kuwa salama katika kipindi chote cha uchaguzi.
Nawapongeza pia Tume
ya Taifa ya Uchaguzi kwa namna walivyosimamia zoezi zima la uchaguzi toka hatua
za awali za kujiandikisha hadi siku ya kupiga kura na kutangaza matokeo.
Mmetimiza wajibu wenu kwa weledi na umahiri mkubwa katika mazingira magumu na
yenye changamoto nyingi. Hongereni, hongereni sana!
Mheshimiwa
Spika;
Naomba kwa namna ya pekee, niwashukuru
viongozi wakuu wa nchi yetu walionitangulia kwa kazi kubwa na nzuri
walioifanyia nchi yetu. Natambua mchango wa Waasisi wa taifa letu, Mwalimu
Nyerere na Mzee Karume kwa kujenga misingi imara wa umoja, mshikamano na amani
ya nchi yetu. Mzee Mwinyi (Mzee Ruksa) kwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na
kisiasa na kuijenga misingi yake. Mzee Mkapa (Mzee wa Ukweli na Uwazi) kwa kupanua
na kuimarisha misingi ya uchumi na siasa ya nchi yetu. Mzee Kikwete (Mzee wa
Maisha Bora) kwa kuendeleza misingi hiyo na kupanua fursa mbalimbali kwa
wananchi kujiletea maendeleo yao. Wamefanya kazi kubwa. Nawashukuru sana na
ninawatakia uzee mwema na maisha marefu ili tuzidi kuchuma busara zao.
Mhishimiwa
Spika;
Tumeingia kwenye uchaguzi wamoja, tumeshindana katika kampeni tukiwa
wamoja, na tumemaliza uchaguzi wetu tukiwa wamoja. Nataka niwahakikishie
Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali ya Awamu ya Tano
itaendelea kulinda kwa nguvu na uwezo wote Tunu hizi za Umoja na Amani.
Hatutakuwa na simile kwa mtu au kikundi chochote ambacho kitataka kuvuruga
umoja na amani yetu kwa misingi ya udini, rangi, ukabila, vyama au ukanda.
Mheshimiwa Spika;
Wakati wa kampeni, yako maeneo yaliyojitokeza
kwa kulalamikiwa sana na wananchi. Ningependa niyataje baadhi ya maeneo
yaliyolalamikiwa, maeneo hayo ni pamoja na:
·
Rushwa
-
Suala la rushwa limelalamikiwa sana takriban katika maeneo yote yanayogusa
wananchi.
·
TAMISEMI
- Upotevu wa mapato, kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya
fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi, uzembe, n.k.;
·
Ardhi
–
Migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza,
mipango miji, kujenga maeneo ya wazi, n.k.;
·
Bandari
- Rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu;
·
Maji
–
Kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma ya maji
kupatikana mbali na makazi, n.k.;
·
TRA
- Ukwepaji kodi, rushwa, ubadhirifu, urasimu na upotevu wa mapato kwa kushindwa
kukusanya kodi hasa kodi zinazotakiwa kulipwa na wafanyabishara wakubwa;
·
TANESCO
- Kukatika kwa umeme mara kwa mara na uwepo wa umeme wa mgao;
·
Maliasili
na Utalii - Ujangili ambao lazima Idara husika inashiriki,
Migogoro ya mipaka kati ya vijiji na Hifadhi, Upotevu wa mapato, n.k.;
·
Huduma
za Afya (Hospitali) - Huduma kuwa mbali na wahitaji,
Ukosefu wa madawa, hujuma kwenye vifaa vya vipimo, msongamano wa wagonjwa na
tozo zisizostahili, lugha mbaya za watumishi kwa wagonjwa, uhaba wa majengo,
vitendea kazi, rasilimali watu na fedha, kushindwa kukusanya mapato
yanayowahusu, n.k.;
·
Uhamiaji
na Ajira - Kutoa hovyo hati za uraia, Vibali vya kuishi
nchini kwa wageni, Kushindwa kusimamia ajira za wageni hususan kwa kazi
zinazoweza kufanywa na wazawa, n.k.;
·
Elimu
- Uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, michango mingi isiyo ya lazima,
malalamiko ya walimu yasiyoisha, mazingira ya kusomea ikiwa ni pamoja na
majengo, Madawati, Ukosefu wa nyumba za walimu, n.k.;
·
Polisi
-
Malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi, upendeleo, Madai ya askari, Ukosefu wa
nyumba za askari, Ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa, n.k.;
·
Zimamoto
– Kuchelewa kufika kwenye matukio, kufika kwenye matukio bila vitendea kazi
kama maji, n.k.;
·
Mizani
–
kucheleweshwa kwa magari yanayosafiri;
·
Mahakama
-
Natambua jitihada za Mahakama katika kushughulikia swala la mrundikano wa kesi.
Hata hivyo, bado kumekuwa na malalamiko mengi juu ya ucheleweshaji wa kesi.
·
Madini
–
Wenyeji kutofaidika, Vilio vya wachimbaji wadogowadogo kutengewa maeneo ya
uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu kulipa fidia,
n.k;
·
Kilimo
na Mifugo – Uhaba wa pembejeo za mifugo na kilimo, Tatizo la
masoko, Kukopwa mazao ya wakulima, Ukosefu wa Wataalamu wa Ugani, Upungufu wa
Maghala, Mabwawa, Malambo, Majosho, n.k.;
·
Uvuvi
–
Vifaa duni na masoko, Uvuvi haramu, Uwekezaji mdogo katika Sekta ya Uvuvi hususan
viwanda vya mazao ya uvuvi n.k., na hasa katika ukanda wetu wa bahari;
·
Reli
–
Uchakavu wa miundombinu ya nchi, Kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika wa reli, upungufu
wa bandari kavu, Mizigo mingi kusafirishwa kwa barabara, n.k.;
·
ATC
–
Shirika la Ndege lipo, Wafanyakazi wapo zaidi ya 200, na wanalipwa mishahara ila ndege ni moja (1);
·
Makundi
Maalum – Haki za wazee, Walemavu, Wanawake na watoto
zimekuwa zikikiukwa;
·
Wafanyakazi,
Wasanii na Wanamichezo – Mzigo wa kodi kwa wafanyakazi,
Haki na maslahi yao, n.k.;
Kero hizi tutazishughulikia
kwa nguvu zetu zote. Wizara, Ofisi na Taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua
kero hizi. Nimetaja baadhi ya kero hizi ili nanyi Waheshimiwa Wabunge mzitambue
na mshirikiane na Serikali na wadau wengine tuzitatue haraka.
Pamoja na kero hizo
tutashughulikia pia mambo yafuatayo.
Kuimarisha
Muungano
Mheshimiwa Spika;
Nilipoapa kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niliapa kuulinda Muungano wa nchi yetu.
Hata bila kiapo, mimi ni muumini wa dhati wa Muungano wetu wa kipekee,
uliounganisha nchi mbili zilizokuwa huru za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya
Watu wa Zanzibar, tena kwa hiari na kwa wino wa kalamu, na si mtutu kama
miungano mingine duniani. Naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa Muungano wetu
ndio umoja wetu, amani yetu na salama yetu. Ninayo kila sababu ya kuulinda na
kuuenzi Muungano wetu adhimu na adimu. Ni azma yangu kuwaona wananchi wa
Zanzibar na Bara wakifurahia matunda ya Muungano wetu badala ya kuwa kikwazo
kwa ustawi wao na ustawi wa nchi yetu.
Aidha, kwa
kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa siasa hususan
vyama vya CUF na CCM tutahakikisha kuwa majaribu ya kisiasa yanayoikabili
Zanzibar yanamalizika kwa salama na amani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie
busara na hekima tumalize kwa utulivu na amani.
Serikali
nitakayoiunda itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuendelea kuimarisha
Muungano wetu. Nina faraja kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais anao
uzoefu mkubwa kutokana na nafasi yake ya awali ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, na pia akiwa Makamu Mwenyekiti wa
Bunge la Katiba. Mimi pamoja na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar,
Dkt. Ali Mohamed Shein tutahakikisha tunasimamia na kuimarisha Muungano wetu.
Kuimarisha
Mihimili ya Serikali
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya
Tano itaheshimu na kuendeleza utamaduni mzuri uliojengeka nchini wa kuheshimu
mihimili ya dola. Tutafanya hivyo kwa kuhakikisha kuwa mihimili yetu ya Bunge na Mahakama inapata fedha za
kutosha kuendesha shughuli zake kwa uhuru kupitia Mfuko wa Bunge na Mfuko wa
Mahakama. Kwa upande wa Bunge, tutahakikisha fedha za Mfuko wa Maendeleo ya
Jimbo zinapatikana kwa wakati ili Waheshimiwa Wabunge mkashirikiane na wananchi
wenu kusukuma maendeleo. Kwa upande wa Mahakama, tutalipa uzito mkubwa suala la
uboreshaji wa Mahakama kwa kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi,
kuongeza kasi ya utoaji haki na kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama
zetu.
Mchakato
wa Katiba
Mheshimiwa Spika;
Serikali yangu
imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika Awamu
iliyopita kutokana na kutokukamilika kwa wakati kwa zoezi la uandikishaji
wapiga kura. Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya
kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa
maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba
lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu kama
ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba.
Uchumi
na Matarajio ya Wananchi
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya
Tano inaingia madarakani kukiwa na msingi imara wa kiuchumi uliojengwa katika
Awamu inayomaliza muda wake. Uchumi wa nchi yetu umekuwa ukiimarika na kukua
wastani wa asilimia 7. Katika
kipindi hicho fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini mwetu zimezidi
kufunguliwa. Hii ni kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali za Awamu
zilizopita za kujenga miundombinu ya kiuchumi kama vile barabara, uimarishaji
wa bandari, uimarishaji wa reli, na ukuzaji wa sekta za mawasiliano ya simu na
mitandao, ukuzaji na uongezaji wa uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme.
Napenda
kuwahakikishia kuwa tutaendeleza na kuimarisha ujenzi wa miundombinu mipya na
kuiimarisha iliyopo ili kuvutia na kushawishi wawekezaji wa ndani na wa nje.
Mheshimiwa Spika;
Nasema hivi kwa
sababu miongoni mwa ahadi tulizowaahidi Watanzania ni kuendeleza ujenzi wa
barabara mbalimbali za kuunganisha miji yetu mikuu ya mikoa na wilaya; barabara
ziendazo kwenye maeneo muhimu ya kimkakati na kiuchumi; na upanuaji wa barabara
za miji kama Dar es Salaam kwa kujenga flyovers,
barabara za pete (ring roads),
n.k. Uboreshaji wa barabara na njia nyingine za uchukuzi na usafirishaji
kuingia na kutoka Dar es Salaam ni muhimu sana kwa sababu bandari ya Dar es
salaam ni lango kuu la biashara kwa nchi yetu na nchi jirani.
Mheshimiwa Spika;
Katika
jitihada hizo hizo za kuboresha na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi Serikali
ya Awamu ya Tano, katika kipindi cha miaka mitano ijayo itaelekeza nguvu zake katika ujenzi wa
reli mpya katika kiwango cha kimataifa (yaani standard gauge). Reli ambazo
tunakusudia zianze kujengwa ni:
·
Dar es Salaam – Tabora – Kigoma/Mwanza
·
Uvinza – Msongati (Burundi) na Isaka –
Kigali (Rwanda)
·
Mtwara – Songea – Mbamba Bay na matawi
ya kwenda Mchuchuma na Liganga;
·
Tanga – Arusha – Musoma
·
Kaliua – Mpanda – Karema
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu pia
imejaliwa kuwa na madini na maliasili nyingi. Ugunduzi wa gesi asilia umeongeza
matumaini ya watu wetu wengi juu ya uwezo wetu wa kiuchumi katika miaka ijayo. Serikali
itahakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa
letu kwa kusimamia Sheria na Taratibu zilizopo. Aidha, napenda kuipongeza kwa
dhati kabisa Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Bunge la 10 kwa
kupitisha Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi yaani The
Oil and Gas Revenues Management Act, 2015. Serikali yangu itasimamia
utekelezaji wa sheria hiyo kwa uaminifu na umakini mkubwa.
Ujenzi
wa Viwanda
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya
Tano itaweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa Viwanda. Natambua kwamba sekta
binafsi ndiyo muhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Hatuna njia nyingine
kama kweli tunataka kujenga msingi wa uchumi endelevu katika nchi yetu
utakaopaisha uchumi na maisha ya watu wetu. Dira ya Maendeleo ya 2025 inatutaka
tuwe nchi ya watu wenye kipato cha kati. Tunaweza tukafika huko, na dalili
zipo, lakini pia tunaweza tukafika huko kitakwimu tu wakati ukweli na uhalisia
wa mambo ni tofauti. Utofauti ninaouzungumzia ni pale takwimu zitakapoonyesha
kwamba sisi ni nchi ya kipato cha kati wakati mapato halisi na hali za maisha
ya watu wengi hazifanani na takwimu hizo. Tamaa yangu na kwa kweli jitihada za Serikali
ya Awamu ya Tano, zitakuwa katika ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ambapo
sura na maisha ya Watanzania walio wengi yafanane fanane na nchi ya kipato cha
kati. Njia moja ya kutufikisha huko ni uendelezaji wa viwanda.
Mheshimiwa Spika;
Tutahakikisha suala
la viwanda linasimamiwa vizuri na tunafanikiwa. Matarajio yangu ni kuwa Bunge
lako Tukufu litatuunga mkono mimi na Serikali nitakayoiunda katika kufikia
lengo hili.
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema
wakati wa Kampeni, na nataka nirudie hapa, tutaanza na viwanda vilivyopo na
kuhakikisha vinafanya kazi. Wale wote ambao walibinafsishiwa viwanda
vilivyokuwa vya umma kwa makubaliano kwamba wataviendeleza niliwataka wafanye
hivyo mapema. Na hapa nataka nisisitize wito wangu huo kwao. Najua huko nyuma
ufuatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa mikataba ya aina hiyo umekuwa ukilegalega
na watu wamejifanyia mambo watakavyo. Wapo walioacha kabisa uzalishaji na
kufumua hata mitambo ya uzalishaji. Mimi niliahidi, na nataka niseme hapa kwa
wazi kabisa, kwamba wale waliobinafsishiwa viwanda hivyo waanze kazi, waanze
kazi mara moja. Wakishindwa basi tutavitwaa viwanda hivyo kwa kuzingatia sheria
na taratibu za nchi na kuwapa watu wengine wenye nia ya kuviendeleza. Hatuwezi
kuwa na watu wanajiita wawekezaji tunawapa viwanda vyetu halafu wanaviatamia
tu. Mimi hilo sitalikubali na wala sitalivumilia. Nimeielekeza Ofisi ya Msajili
wa Hazina kuanza kushughulikia suala hili mara moja. Naomba Bunge lako lituunge
mkono.
Mheshimiwa Spika;
Njia ya pili ya
kuendeleza viwanda ni kuhimiza na kushawishi wawekezaji kuwekeza katika maeneo
mbalimbali ya nchi yetu. Kama nilivyoeleza miundombinu ya kufanya hivyo tayari
ipo na baada ya muda itakuwa bora zaidi. Najua wapo watu wanaotaka kuwekeza
Tanzania sasa, katika viwanda, na wamekuwepo hata miaka ya nyuma kidogo, lakini
wakati mwingine sisi humu humu – tukiwemo sisi viongozi kwa kushirikiana na
wafanyabiashara matapeli na laghai – tumehujumu mipango na shauku ya wawekezaji
wa nanma hiyo. Pamoja na shauku na utayari wao wa kuwekeza Tanzania tumewawekea
vikwazo na kuwapiga vita na hivyo kuwalazimisha kwenda kuwekeza katika nchi
jirani. Sisi katika Serikali ya Awamu ya Tano tutajitahidi sana kuondoa
usumbufu na urasimu wa aina hiyo na kuongeza bidii ya kuwashawishi wawekezaji
wa ndani na wa nje kuja kuwekeza viwanda hapa nchini. Kwa watendaji wa Serikali
watakaokwamisha jitihada za uwekezaji na ujenzi wa viwanda hapa nchini
hatutawavumilia.
Mheshimiwa Spika;
Ni
viwanda vya aina ipi hasa tunavyovikusudia? Sura ya
kwanza ya viwanda tunavyovikusudia ni vile ambavyo sehemu kubwa ya malighafi
yake itatoka ndani, hususan kweye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, na madini –
na maliasili nyingine. Viwanda vya aina hii vitatupa fursa ya kujenga mfumo wa
uzalishaji ndani ya nchi uliofungamana na kushikamana. Viwanda vya aina hii
vitahitaji na kutegemea malighafi toka kwa wazalishaji wa sekta nilizozitaja,
na kwa kufanya hivyo wazalishaji hao watakuwa na soko la uhakika humu humu
ndani ya nchi. Sura ya pili ya viwanda hivi ni kuzalisha bidhaa ambazo
zinatumiwa na watu wengi humu nchini (mass consumption) – yaani bidhaa kama
vile nguo, viatu, mafuta ya kupikia, n.k. kwa hivyo viwanda hivi vitakuwa na
uhakika wa soko la ndani kabla ya kufikiria soko la nje. Viwanda hivi
vitatarajiwa kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje. Yote mawili yakitokea,
yaani kuzalisha kwa ajili ya soko la ndani na nje, itatuongezea akiba yetu ya
fedha za kigeni na kutuwezesha kutekeleza na kuendeleza mipango mingine kwa
ajili ya ustawi wa uchumi wetu. Sura ya tatu ya viwanda tunavyovikusudia ni
kuzalisha ajira nyingi. Shabaha yetu ni kuwa ifikapo mwaka 2020 idadi ya ajira
itokanayo na viwanda ifikie asilimia 40
ya ajira zote zitakazokuwepo nchini wakati huo.
Mheshimiwa Spika;
Nimeamua kulisema
hili kwa kirefu sana kwa sababu ili tufanikiwe lazima tuelewane na tusaidiane
kulisukuma kwa pamoja jambo hili.
Kilimo,
Mifugo na Uvuvi
Mheshimiwa Spika;
Sekta nyingine ambazo
lazima tutazitilia mkazo mkubwa na kuziendeleza ni kilimo, mifugo na uvuvi.
Tutaziangalia sekta hizi kwa mtazamo wa kibiashara na viwanda kwa lengo la kuwa
na viwanda vya kisasa vya kuongeza thamani mazao yatokanayo na kilimo, mifugo
na uvuvi. Nchi yetu kwa kiasi
kikubwa ni nchi ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Hii inatokana na ukweli kwamba
sehemu kubwa ya watu wetu wapatao asilimia
75 wanaishi vijijini na wanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya maisha
yao. Wakulima, wafugaji na wavuvi wanatumia zana na mbinu duni katika shughuli
zao na wanazalisha zaidi ya asilimia 95
ya chakula chote kinacholiwa hapa nchini, na kutoa mchango wa asilimia 25 kwenye pato la taifa yaani
GDP, na asilimia 30 ya mapato yetu
ya fedha za kigeni. Kwa takwimu hizi chache ni wazi kwamba mchango wa sekta ya
kilimo, mifugo na uvuvi katika uchumi wetu
na maisha yetu ni mkubwa sana. Nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru
wakulima, wafugaji na wavuvi wote wa Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika
maisha yetu na uchumi wa nchi yetu. Nataka kuahidi kwao sitawaangusha.
Mheshimiwa
Spika;
Pamoja na
umuhimu wa kilimo, mifugo na uvuvi katika uchumi wetu
wakulima, wafugaji na wavuvi wetu wengi bado ni watu maskini. Mapato yao yako
chini na wanaishi maisha duni. Lengo letu ni kuuimarisha sekta hizi ili ziweze
kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi lakini pia ziweze kuwanufaisha
wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuyabadili maisha yao. Tukiweza kuboresha
sekta hizi vijana wengi zaidi watavutiwa kujiunga nazo na hivyo kupunguza
tatizo la upatikanaji wa ajira. Nataka
niwahakikishie wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kwamba ahadi zetu kwao
tutahakikisha zinatekelezwa. Serikali ya Awamu ya Tano itazisimamia kwa dhati
ahadi hizo ili kuhakikisha kwamba kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa wa kisasa
zaidi na wenye tija. Baadhi ya mambo tuliyowaahidi kuyatekeleza ni pamoja na
haya yafuatayo:
1. Kuwapatia mafunzo ya kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa ikiwa pamoja na
ufugaji wa samaki,
2. Kuwapatia pembejeo,
3. Kuwapatia zana za kisasa za kilimo, ufugaji na uvuvi,
4. Kuwapatia wataalamu wa ugani,
5. Kuwawezesha kupata masoko ya uhakika ya mazao yao,
6. Kuwapatia mikopo, na kwa hili Benki ya Kilimo itasaidia sana kufikia
lengo hili,
7. Kuondoa ushuru, kodi na kero mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na
uvuvi zinazosababisha bei ya mazao hayo kuwa chini (mfano. Kahawa, kule Kagera
ina kodi 26 ambazo husababisha wananchi kuuza kahawa yao Uganda ambako bei iko
juu, tutapunguza kama sio kuondoa kabisa ushuru hizo ili wakulima wapate bei
nzuri. Tutafanya hivyo pia kwa mazao
mengine kama mahindi, chai, pamba, korosho, mkonge, ngozi, nyama, maziwa, samaki,
n.k.),
8. Kuwahakikishia umiliki wa ardhi na kuwaondolea usumbufu wa wao
kuondolewa kwenye ardhi zao kupisha
wawekezaji,
9. Kuhakikisha kwamba migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji
tunaitatua na kuikomesha kwa kuhakikisha kuwa vyanzo vya msingi vya migogoro
hiyo tunaviondosha haraka,
10. Kuhakikisha kwamba tatizo la
wavuvi kuvamiwa na majambazi na uvuvi
haramu linashughulikiwa kikamilifu.
Tatizo la Umaskini na Ajira
Mheshimiwa
Spika;
Nimezungumzia
umuhimu wa kuendeleza viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi kwa sababu ya matatizo
makubwa mawili yanayoikabili nchi yetu kwa sasa. Kwanza, ni tatizo la UMASIKINI na pili ni tatizo la AJIRA. Ni kweli uchumi wetu umekuwa
ukikua kwa kasi ya kuridhisha, lakini kasi hiyo haijawiana na kasi ya kuondoa
umasikini na uzalishaji wa ajira za kutosha kwa vijana wetu wanaoingia kwenye
soko la ajira kila mwaka.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa
mujibu wa takwimu zilizopo zaidi ya asilimia 28.2 ya Watanzania ni maskini. Na kwamba kwa namna na
kadri uchumi wetu unavyokuwa pengo baina ya matajiri (walionacho) na maskini
(wasionacho) linazidi kukua. Tukiendelea hivi tunavyoendelea sasa hatutakuwa
tunaitakia mema nchi yetu kwa sababu mgawanyiko mkubwa wa kimapato na tofauti
kubwa za kimaisha baina ya matajiri na maskini ukiachiwa uendelee na kuzidi
kukua utachochea chuki na uhasama baina ya walionacho na wasionacho. Lazima
tujizatiti na kutumia akili, maarifa na nguvu zetu zote kukabiliana na
kuibadilisha hali hii. Kwanza, lazima tushughulike na UMASIKINI wa watu wetu. Na njia moja kama nilivyokwisha eleza ni
uendelezaji wa sekta ya viwanda na uboreshaji wa sekta za kilimo, mifugo na
uvuvi.
Mheshimiwa Spika;
Tatizo la pili ni AJIRA. Kama nilivyokwisha kugusia, ukuaji wa uchumi wetu haujaenda
sambamba na kasi ya watu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka. Tatizo la
ajira ni kwa vijana wote waliosoma viwango mbalimbali vya elimu na wasio na
ujuzi. Hii inamaana kwamba sekta zinazochangia kukua kwa uchumi wa nchi yetu
sizo zinazozalisha ajira kwa wingi. Ndio maana ya kuweka msisitizo kwenye sekta
ya viwanda hasa vile vinavyoajiri watu wengi, na sekta ya kilimo, uvuvi na
mifugo ambavyo ndio mwajiri mkubwa hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuweka
msisitizo katika Viwanda, Kilimo, Mifugo na Uvuvi hatuna budi kuwawezesha vijana
wetu kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa viwango mbalimbali. Ili
hili liwezekane, na sisi tutalifanya, linahitaji mambo mawili makubwa.
Kwanza,
kuwaandaa vijana wetu vizuri kielimu na kiujuzi. Hatuna budi kuweka mkazo
katika viwango vya ubora vya elimu na stadi za kazi wanazopata vijana wetu. Nalisema
hili kwa sababu hatuwezi kuzungumzia uendelezaji wa viwanda ikiwa hatujaandaa
vijana wenye uwezo, ujuzi, na stadi za kufanya kazi hizo kwa ubora na ufanisi
wa hali ya juu; hatuwezi kutaka kuwekeza katika viwanda vya nguo au samani
ikiwa hatuna wahandisi wa mitambo wazuri, wabunifu wa zuri na wenye viwango vinavyotakiwa na
kukubalika. Aidha hatuwezi kuwa na vijana wenye uthubutu wa kuanzisha shughuli
za uzalishaji kama hawana elimu na maarifa ya kubuni miradi na kuiendeleza. Kwa
hivyo tutaelekeza nguvu zetu katika kuhakikisha kuwa shule na vyuo vyetu katika
ngazi mbalimbali vinafundisha na kutoa vijana wenye viwango vya hali ya juu vya
elimu, maarifa, ujuzi na ufundi.
Mheshimiwa Spika;
Pili,
ni
suala la uwezeshaji wa vijana hasa wale watakaotaka kujiajiri. Katika
kutekeleza lengo hili Serikali ya Awamu ya Tano itachukua na kutekeleza hatua
mbalimbali ikiwemo:
·
Kuwawezesha vijana wanaohitimu Elimu
ya Juu na Vyuo vya Ufundi kupata mitaji ya kuwasaidia kuanzisha makampuni yao
kulingana na fani walizosomea;
·
Kuwawezesha vijana kuanzisha SACCOS zao na kupitia SACCOS hizo kuwawezesha
kupata mikopo;
·
Kuwawezesha vijana wajasiriamali
kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili waweze kupata mikopo na kunufaika na
mafao mengine katika mifuko hiyo.
Mheshimiwa Spika;
Tatu,
ni kuzitambua na kuziheshimu kazi na shughuli mbalimbali zinazofanywa na
makundi mbalimbali ya kinamama na vijana. Hapa namaanisha shughuli za kina Mama
lishe, wachuuzi mbalimbali, Machinga, waendesha Boda Boda na Maguta, na vijana
wa kike na wa kiume wanaojitafutia kazi mbalimbali halali za kujipatia mapato
kwa ajili ya kuendesha maisha yao, n.k. Shughuli za makundi haya zinatusaidia
sana katika kupunguza makundi ya vijana wetu ambao wangekaa tu na kuzurura
zurura ovyo bila shughuli ya kufanya. Na kwa kuwa kwa sasa uwezo wetu wa
kuwapatia ajira tofauti ni mdogo ni jukumu letu kuwasaidia na kuwawezesha
kufanya shughuli zao kwa utilivu bila bugudha. Niliahidi, na nataka nirudie
hapa, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ikishirikiana na Halmashauri zetu,
pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya itaweka mipango na taratibu nzuri na rafiki
kwa aina ya shughuli ambazo baadhi nimezigusia. Aidha, ushuru usio wa lazima na
wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo utokanao na shughuli
nilizozitaja tutauondoa. Tunaamini ikiwa tutaweza kuongeza ukusanyaji mapato,
na kuziba mianya ya wakwepaji wakubwa wa kodi ambao huipotezea Serikali mabilioni
ya fedha tutakuwa hatuna sababu ya kufukuzana na kina mama na vijana mitaani. Viongozi
na watendaji wa Serikali na hasa wa Halmashauri watenge maeneo kwa ajili ya
wafanyabishara wadogo na waandae mipango ya kupunguza ushuru usio wa lazima.
Afya
Mheshimiwa Spika;
Dhamira ya kujenga
uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umasikini linakwenda sambamba na kuwa
na wananchi wenye afya bora. Kwa kutambua ukweli huu na mahitaji ya huduma bora
za wananchi wetu Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba wananchi
wanapata huduma bora za afya kwa kufanya baadhi ya mambo yafuatayo:
·
Kwanza,
kuimarisha huduma za afya pale zilipo na kuanzisha pale ambapo hazipo. Lengo ni
kuhakisha kwamba kila kijiji kinakuwa na Zahanati, kila Kata inakuwa na Kituo
cha Afya, kila wilaya inakuwa na Hospitali, na kila Mkoa unakuwa na hospitali
ya Rufaa.
·
Pili,
tutaimarisha na kuboresha huduma za afya kwa kuongeza utaalamu katika Nyanja za
afya kwa kuwapatia mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi; kwa kuzipatia
vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Lengo la
kufanya hivyo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma mahsusi hapa hapa nchini na
hivyo kutolazimika kupeleka watu wetu kutibiwa nchi za nje.
·
Tatu,
tutaongeza
bajeti ya dawa na kuboresha mfumo wa upatikanaji ili kuhakikisha dawa
zinapatikana katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Aidha,
tutahamasisha wananchi wajiunge na Bima ya Afya.
Elimu
Mheshimiwa Spika;
Natambua juhudi kubwa zimefanyika
katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu. Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika
kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika
masomo ya sayansi. Aidha, tutahakikisha
kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na
maabara, vitabu, madawati, n.k. Tutahakikisha kuanzia Januari mwakani elimu
kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure, kama tulivyoahidi
kwenye kampeni. Tutahakikisha kwamba
wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati. Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa
ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu vijijini na kuiunga
mkono Benki ya walimu ili iweze kuwanufaisha zaidi.
Maji
Mheshimiwa
Spika;
Wakati wa kampeni nimekutana na
malalamiko mengi sana ya ukosefu wa maji. Serikali ya Awamu ya Tano
itahakikisha kwamba inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 95 kwa maeneo ya mijini
ifikapo 2020. Tutakamilisha miradi iliyokwishaanza na kuanzisha miradi mipya
mikubwa na midogo ya maji kutoka katika mito, maziwa na vyanzo vingine vya
uhakika vya maji ikiwa pamoja na kuvuna maji ya mvua. Tunataka
tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umaskini hauwezi kuondoka nchini
kama wananchi hawapati maji safi na salama.
Umeme
Mheshimiwa
Spika;
Suala la
upatikanaji wa umeme limeendelea kuwa tatizo katika nchi yetu pamoja na
jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali zilizopita. Hatuwezi kuzungumzia suala
la kujenga viwanda wakati umeme hautoshi. Serikali yangu itahakikisha kwamba
umeme unapatikana wa kutosha na wa uhakika. Tutakamilisha miradi ya umeme
iliyopo na kujenga mingine mingi mipya ili wananchi wengi zaidi wanufaike na
nishati ya umeme na viwanda vingi zaidi vidogo vidogo, vya kati na vikubwa
vianzishwe.
Madawa ya Kulevya
Mheshimiwa
Spika;
Madawa ya kulevya yamekuwa ni janga
kubwa kwa taifa letu na kundi linaloathirika zaidi ni vijana wa kiume na kike.
Familia nyingi zimeathirika na nguvu kazi ya taifa imepotea. Tutaushughulikia mtandao huo hususan
wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na madawa ya kulevya bila ajizi.
Mheshimiwa
Spika;
Masuala mengine
tutakayoyawekea mkazo katika utawala wa Awamu ya Tano ambayo ninaamini
yatasaidia katika kujenga uchumi wetu ni pamoja na masuala ya Utalii,
Mawasiliano, Madini, Ardhi na Makazi, Ujenzi na Miundombinu, Bandari, Barabara,
Ulinzi na Usalama, utunzaji wa mazingira, Vijana, Wanawake, Watu wenye Ulemavu
na Ualbino, Wazee, Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo, wanahabari,
wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali, sekta binafsi, n.k. Utekelezaji wa
masuala haya umefafanuliwa vizuri katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015.
Tutayatekeleza ipasavyo.
Mapambano
Dhidi ya Rushwa na Ufisadi
Mheshimiwa Spika;
Jambo moja
nililolisemea kwa nguvu kubwa wakati wa kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na
ufisadi. Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe
kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati kabisa,
na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa nilichokikusudia.
Mheshimiwa Spika;
Wananchi wanachukia
sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo. Mimi pia ninachukia
rushwa na ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo vya rushwa na ufisadi
vinavyoendelea hapa nchini. Vitendo vya rushwa na ufisadi vinawanyima haki wananchi
na kuitia hasara serikali kwa mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kwa
ajili ya kujenga miradi ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu.
Mheshimiwa Spika;
Chama changu, Chama
cha Mapinduzi, kimejengwa katika misingi ya kukataa rushwa na ufisadi. Ndio
maana moja ya Imani kuu za CCM ni ile isemayo: “Rushwa ni adui wa haki, sitatoa
wala kupokea rushwa”
Kwa Mtanzania
mwaminifu kwa imani yake hatakuwa na kigugumizi katika kuwa mstari wa mbele
katika kupambana na rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa Spika;
Mmoja wa waasisi wa
Taifa letu, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi
kuifananisha rushwa na ufisadi ‘Kama Adui
Mkubwa wa Watu’. Akiongea Bungeni
Mei 1960, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo kuhusu rushwa:
“Rushwa [na ufisadi] havina budi
kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini wakati wa Amani rushwa na ufisadi
ni adui mkubwa kwa ustawi wa watu kuliko vita.”
Mheshimiwa Spika;
Haya ni maneno makali
ya mtu na kiongozi aliyeichukia na kuikemea rushwa katika maisha yake yote ya
uongozi. Ni maneno yanayotukumbusha tu nini kinaweza kikatutokea kama taifa
endapo tutaendekeza rushwa na ufisadi. Chuki za wananchi dhidi ya rushwa na
ufisadi ni dhahiri, wamechoka kabisa, wamechoka sana, hawako tayari kuvumilia
upuuzi wa serikali itayoonea haya rushwa na kulea mafisadi.
Mheshimiwa Spika;
Mimi nimewaahidi
wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu,
kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote.
Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua
kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine. Hivyo
ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na muniunge mkono
wakati natumbua majipu haya.
Mheshimiwa Spika;
Ninafahamu ugumu wa
vita niliyoamua kuipigana. Nasema nafahamu ugumu na changamoto zake kwa sababu
wanaojihusisha na rushwa sio watu wadogo wadogo. Vitendo vya rushwa na ufisadi
vyenye madhara makubwa kwa nchi na ustawi wa nchi yetu hutendwa na watu wenye
dhamana kubwa za uongozi na utumishi ambazo wamezipata kutokana na ridhaa ya
watu. Kwa hivyo ili niweze kufanikiwa
lazima nipate ushirikiano mkubwa toka kwa Bunge lako tukufu na vyombo vingine
vilivyopo na vyenye majukumu ya kupambana na vitendo hivi.
Aidha, tutashinda
vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina mashaka kuwa kwa vile wao,
kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano
wao katika mapambano haya dhidi ya rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa Spika;
Katika kushugulikia
tatizo hili nimeahidi kuunda mahakama ya Rushwa na Ufisadi. Ni matumaini yangu
vyombo husika katika jambo hili havitanikwamisha.
Aidha, nataka niahidi
mbele ya Bunge lako tukufu kwamba, kiongozi yeyote wa kuteuliwa, ambaye mimi
nitakuwa nimemteua kwa mamlaka niliyonayo kikatiba, na ninayo mamlaka ya
kumwajibisha, pindi tu nikibaini na kujiridhisha kuwa anajihusisha na vitendo
vya rushwa na ufisadi nitamtimua mara moja. Baada ya mimi kuchukua hatua hizo
hatua na taratibu zingine za kisheria zitafuata.
Mheshimiwa Spika;
Ninachotaka kusema ni
kuwa Serikali yangu itafuatilia kwa karibu mienendo ya viongozi na watendaji wake
ili kubaini kwa haraka nani anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi. Na
tukishajiridhisha hatutasubiri, tutachukua hatua. Ni imani yangu wengine pia
katika ngazi mbalimbali mtafanya hivyo. Kwa sababu bila kufanya hivyo rushwa na
ufisadi vitazoeleka na kuwa wimbo unaoburudisha badala ya kuudhi na kukera.
Muundo
wa Serikali na Utumishi
Mheshimiwa Spika;
Nilipokuwa nazunguka
na kuzungumza na wananchi wakati wa Kampeni za Uchaguzi, niliahidi kuwa
nitaunda serikali ndogo ya wachapa kazi.
Aidha, niliahidi pia
kuunda serikali ambayo itawatumikia watu na hasa wananchi wa kawaida. Serikali
nitakayounda, nataka iwe inawahudumia wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua
sumbua na kuwazungusha. Natoa rai kwa watumishi wa serikali, hasa ambao ni
wazembe na wavivu, kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu sasa basi. Kwa sababu
watumishi wa aina hiyo hawatavumuliwa katika serikali nitakayoiongoza. Lugha za
“hiyo
ni changamoto tutaishughulikia”, au “Mchakato unaendeela”
hazitavumiliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi nataka watu wa Kazi Tu. Hatuwezi kulea watu ambao
wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi wanazotakiwa kufanya, au wamegeuza
ofisi za umma kuwa ni mahala pa kuchuma bila kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuwataka
watumishi wa Serikali kufanya kazi hatuna budi kuyaangalia na kuboresha
mishahara na maslahi yao na mazingira yao ya kufanyia kazi kwa kuwapatia
vitendea kazi bora na vya kisasa. Na jambo moja tutakalolitekeleza ni kuangalia
namna ya kupunguza kodi ya mapato katika mishahara ya wafanyakazi yaani PAYE.
Pia tutajitahidi kuwatambua na kuwapa motisha wafanya kazi wachapa kazi.
Kuongeza
Mapato na Kupunguza Matumizi ya Serikali
Mheshimiwa Spika;
Kwa zaidi ya miaka
mitatu sasa ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio kwa sababu
mbalimbali. Serikali ya Awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa
kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Tutahakikisha kwamba kila
mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki. Hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote
atakaye kwepa kulipa kodi. Tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila
mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili
kulipa kodi alipe.
Aidha, tutahakikisha
kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika
kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za
Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa Spika;
Nitataja baadhi tu ya
maeneo ambayo tutayasimamia kwa lengo la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na
kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za Serikali:
Kwanza,
safari zote zisizo za lazima nje ya nchi Serikalini tutazidhibiti na badala
yake tutawatumia mabalozi wetu kutuwakilisha kwenye mikutano ya aina hiyo. Na
pale inapolazimu kiongozi au mtumishi mwandamizi kusafiri tutahakikisa kwamba
haandamani na msururu wa watu wengi ambao hawana umuhimu wala shughuli za
kufanya katika safari hizo.
Katika kusisitiza
hili napenda niwape takwimu za fedha zilizotumika ndani ya Serikali, Mashirika
ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14
na 2014//2015. Jumla ya shilingi
bilioni
356.324 zilitumika kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:
·
Tiketi za ndege (Air ticket) zilitumia
shilingi bilioni 183.160;
·
Mafunzo nje ya nchi (Training Foreign) zilitumia shilingi bilioni 68.612;
·
Posho za kujikimu (Per Diem Foreign) zilitumia shilingi bilioni 104.552;
Wizara na Taasisi
zinazoongoza kwa matumizi ya safari za nje ni pamoja na Bunge, Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi
ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT), Wizara ya Mambo ya Ndani,
n.k.
Hizi
fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya
chini, kama afya, maji, elimu, umeme n.k. Mfano; fedha hizi zingetosha
kutengeneza kilometa 400 za barabara
za lami, tujiulize zingeweza kutengeneza zahanati ngapi?, nyumba za walimu
ngapi?, madawati mangapi? n.k. Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba
Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.
Pili,
tutahakikisha tunadhibiti safari na ziara za mafunzo nje ya nchi
zinazogharamiwa na serikali ambayo yanapatikana hapa nchini.
Tatu,
tutadhibiti warsha, semina, makongamano, na matamasha ambayo kwa kweli
yanatumia fedha nyingi tu za serikali lakini hayana tija na wala hayaongezi
ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa sera na mipango ya Serikali.
Nne,
tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ili kuhakikisha kwamba
mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi hafifu tunaiziba. Ni
matarajio yangu kutakapoleta Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya
Umma Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono.
Tano,
tutasimamia na kudhibiti ukiukwaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali
yaliyokwisha kutolewa na Serikali siku za nyuma kuhusu ununuzi wa bidhaa kama
samani kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Samani zote kwa ajili ya matumizi ya
Serikali zinatakiwa ziwe zile zinazozalishwa hapa hapa nchini.
Sita,
Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia kwa karibu na kuthibiti ununuzi wa magari
ya gharama kwa ajili ya Viongozi na Watumishi waandamizi wa Serikali; na
Saba, tutaendelea
kuchunguza na kudhibiti matumizi ya Serikali na Taasisi zake zote yasiyo na
tija kwa uchumi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika;
Kwa ajili
hiyo, vipaumbele vya Serikali ninayotarajia kuiunda vitakuwa ni: kupunguza urasimu ili kuongeza kasi ya
utekelezaji wa maamuzi na miradi ya Serikali; kubana matumizi kwa kupunguza yale ambayo kutokana na hali yetu ya
uchumi kwa sasa yanaweza kuepukika;
na kurejesha nidhamu ya Serikali na
utumishi wa umma kwa kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Tutatekeleza
vipaumbele hivyo kwa kufanya pamoja na mambo mengine kupunguza ukubwa wa Baraza
la Mawaziri; kuongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na maduhuli
ya Serikali kwa kuziba mianya ya ukwepaji kodi, tutahakikisha kwamba wale wote
wanaotakiwa kulipa kodi wanalipa ipasavyo. Tutaongeza nidhamu ya matumizi ya
Serikali ili kuhakikisha fedha zinazookolewa zinakwenda kwenye miradi ya
maendeleo; na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa viongozi
na watumishi wa umma ili wawajibike kwa wananchi ambao ndio wateja na waajiri
wakuu wa watumishi wa umma. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kubainisha
maeneo mengine ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo yanaigharimu Serikali fedha
nyingi na kuyadhibiti. Aidha, nitoe wito kwa Watanzania wote kila mmoja wetu
afanye kazi iwe shambani, ofisini, kiwandani, sokoni, n.k. Badala ya tabia ya sasa iliyoanza kujengeka
kwa Watanzania kutokupenda kufanya kazi na hivyo kupoteza muda mwingi vijiweni,
muda ambao ungetumika kufanya kazi ndiyo maana kauli mbiu yangu ni HAPA KAZI TU!
Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa
Kikanda
na Kimataifa
Mheshimiwa Spika;
Nchi
yetu imepata mafanikio makubwa katika Nyanja ya diplomasia na ushirikiano wa
kimataifa katika awamu zilizotangulia za uongozi. Serikali yangu itaendeleza
sifa hiyo kwa kujenga juu ya msingi imara uliowekwa na awamu zilizotangulia na
awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Tutaendelea kuwa
waumini na tutaendeleza sera ya ujirani mwema na nchi zinazotuzunguka kwa lengo
la ustawi wa watu wetu na maslahi mapana ya nchi yetu. Tutaendelea kuwa
waaminifu wa utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na daima
tutatekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, itifaki zake na maamuzi ya vikao vya nchi wanachama.
Tutaendelea kutekeleza matakwa ya Mkataba huu wa kujenga utengamano wetu hatua
kwa hatua.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania itaendelea
kuwa mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
na kuendelea kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama ambao tunauhusiano wa
kihistoria na kidugu. Tutaendelea kuamini katika Umoja wa Afrika (AU) na azma
ya ndoto ya waasisi wetu ya kuunganisha bara la Afrika. Tutaendelea pia
kushiriki kikamilifu katika Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na
kushirikiana na nchi wenzetu wanachama kutafuta majawabu ya kudumu ya amani,
usalama na maendeleo katika eneo la maziwa makuu.
Tutaendeleza
na kustawisha mahusiano na marafiki zetu wote Magharibi, Mashariki ya Mbali na
Mashariki ya Kati kwa lengo la kushirikiana kwa maslahi ya nchi zetu na watu
wetu. Tutapenda kutumia fursa nzuri ya mahusiano yetu mazuri kisiasa kukuza
mahusiano yetu ya uchumi kwa kutumia diplomasia ya uchumi. Tutafanya hivyo pia
kwa ushirikiano wa kimataifa kwa kuendeleza mahusiano yetu na Umoja wa Mataifa
(UN) na taasisi zake, Jumuiya ya Madola, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha
Duniani (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), n.k.
Aidha, tutazitaka
Balozi zetu zionyeshe matunda yanayolingana na thamani ya fedha tunazowapelekea
hususan katika kuvutia uwekezaji, biashara, utalii na mchango wao katika
ukuzaji wa sekta ya viwanda. Tunataka kuona diplomasia yetu na Sera yetu ya nje
ikijibu changamoto zetu za ndani za ajira, miundombinu, masoko ya mazao ya
wakulima, viwanda n.k.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika;
Naomba kabla ya
kuhitimisha nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge, Bunge hili linalo nafasi ya
kuweka historia ya kuwa kitu kimoja na kuweka masilahi ya Taifa mbele. Kama
kuna kitu ambacho wananchi wanachukia ni lugha za vijembe, mipasho, na ushabiki
wa vyama bungeni. Kwanza, tukumbuke wote bila kujali itikadi za vyama vyetu sisi
ni kitu kimoja; na pili tumechaguliwa kuwawakilisha wenzetu. Baada ya miaka
mitano kila mmoja atarudi kwenye jimbo lake kuomba kura na huko atapimwa kwa
maendeleo aliyopeleka.
Tusimame pamoja,
Tanzania ni yetu sote tutangulize masilahi ya nchi mbele, na kwa mara ya kwanza
Watanzania waone Bunge tofauti na sio Bunge la kuzomea, kutoka nje, kutukanana,
mipasho, n.k. Tunaitwa Waheshimiwa kwa heshima ya dhamana tuliyopewa na Bunge
hili Tukufu, tutunze heshima hiyo ili tuzidi kuheshimiwa.
Aidha, napenda kusisitiza
kuwa kazi iliyoko mbele yetu ni kubwa. Matarajio na matumaini ya Watanzania
waliotuchagua na kutupa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano
ijayo ni makubwa. Wanachotaka kuona ni nchi yetu kupiga hatua kubwa za
maendeleo zitakazojibu matumaini yao na kutatua shida na kero zao. Nyie na
mimi, baada ya miaka mitano toka sasa, tutapimwa kwa namna tutakavyokuwa
tumetekeleza mambo ambayo tumewaahidi Watanzania wenzetu. Mimi nina amini
kabisa kwa ushirikiano wetu na kwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu tutaweza
kuzitimiza ndoto za Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa Spika;
Sasa natamka kwamba
nimelifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Asanteni kwa
kunisikiliza!
Mungu libariki Bunge letu na
Wabunge wake!
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment