Saturday, November 21, 2015

Tukumbushane: Matatu Aliyoyasema Zitto Kabwe Angali Chadema..


Ndugu zangu,
Mimi bado nina kukumbukumbu ya nitakachokisema hapa; katikati ya tuhuma za usaliti wa Zitto Kabwe Chadema nakumbuka ndugu yangu Zitto Zuberi Kabwe alisema matatu haya kuhusu imani kwa mwanasiasa;

1. Mwamini mwanasiasa anapokutajia jina lake na salamu anayokupa.
2. Kwenye siasa hakuna adui wala rafiki wa kudumu
3. Muhimu ni kuweka ' akiba ya maneno'
Ndio, katika hayo kuna ukweli, tumepata kumsikia mwanasiasa wa kuheshimika akitamka hadharani kuwa atakuwa mtu wa mwisho kuhama chama chake. Tunajua kilichotokea baada ya kauli hiyo. Tukamsikia anayesema yeye na ubunge basi tena, akimaliza muda wake atakwenda kufundisha. Tunajua kilichotokea.
Mwanasheria nguli, Tundu Antipas Lissu, alipata kusikika bungeni akiwalaumu CUF kwa kuwa sehemu ya uwepo wa Katiba mpya ya Zanzibar inayotishia uwepo wa Muungano, naam, kwenye siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu!
Angalia hapa sehemu ya alichokiwakilisha Tundu Lissu Julai 4, 2012 kama Msemaji Mkuu wa kambi Rasmi ya Upinzani akichangia Makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano)
Mengine nawaachia wajumbe mjadili nyinyi...
Maggid.
"Mheshimiwa Spika,
Katiba mpya ya Zanzibar sio tu kwamba ‘imetangaza uhuru’ wa Zanzibar kwa kuhoji misingi muhimu ya Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano, bali pia imehakikisha kwamba uhuru huo utalindwa dhidi ya tishio lolote la Serikali ya Muungano. Hii imefanywa kwa kuweka utaratibu wa kuwepo kura ya maoni ya wananchi wa Zanzibar kuhusu mabadiliko ya vifungu kadhaa vya Katiba ya Zanzibar. Kwa mujibu wa ibara ya 80A(1) ya Katiba hiyo, “... Baraza la Wawakilishi halitaweza kufanya mabadiliko ya Katiba kuhusiana na sharti lolote lililomo katika kifungu chochote kilichoainishwa katika kijifungu cha (2) cha kifungu hiki, mpaka kwanza mabadiliko hayo yakubaliwe na wananchi kwa kura ya maoni.”
Vifungu vinavyohitaji kura ya maoni ni vifungu vyote vya Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Kwanza inayohusu Zanzibar kama nchi na/au dola; kifungu cha 9 kinachohusu Serikali na watu wa Zanzibar; vifungu vyote vya Sura ya Tatu inayohusu kinga ya haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi; na kifungu cha 26 kinachohusu Rais wa Zanzibar na mamlaka yake.
Vifungu vingine ni pamoja na kifungu cha 28 kinachohusu muda wa urais; Sehemu ya Pili na ya Tatu ya Sura ya Nne zinazohusu Makamu wawili wa Rais, Baraza la Mawaziri na Baraza la Mapinduzi; kifungu cha 80A kinachohifadhi haki ya kura ya maoni; na vifungu vya 121 na 123 vinavyohusu Idara Maalum na mambo yanayohusiana nayo.
Mheshimiwa Spika,
Kuweka masharti ya kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya vifungu tajwa vya Katiba mpya ya Zanzibar kuna athari ya moja kwa moja kwa uhai wa Muungano wetu. Hii ni kwa sababu hata vifungu ambavyo tumeonyesha kwamba vinakiuka misingi mikuu ya Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano haviwezi kubadilishwa bila kura ya maoni ya Wazanzibari.

Kwa maneno mengine, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, masuala ya kama Tanzania ni nchi moja au la, majeshi ya ulinzi, polisi, n.k. ambayo yamekuwa Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano sio Mambo ya Muungano tena hadi hapo wananchi wa Zanzibar watakapoamua – kwa kura ya maoni – kuyarudisha kwa mamlaka ya Muungano. Huku, Mheshimiwa Spika, ni kutangaza uhuru wa Zanzibar bila kutaja neno uhuru! Huku ni kuua Muungano bila kukiri hadharani!"- Tundu Lissu, Julai 4, 2012

No comments: