Ndugu zangu,
Nafuatilia kinachoendelea Zanzibar. Siioni namna nyingine ya kumaliza kadhia iliyotokea bali kwa pande mbili zinazokinzana kukubaliana kurudia uchaguzi. Walokosea wawajibishwe, lakini, hakuna namna nyingine yeyote ya kuhalalisha matokeo yatakayotangazwa baada ya uwepo wa kadhia, isipokuwa, kwa zoezi zima kurudiwa upya ikiwezekana chini ya uangalizi pia wa watu wa kutoka nje. Hivyo, kazi kubwa sasa na iwe kuyatafuta mariadhiano ili Zanzibar isonge mbele kutoka kwenye
hali ya 'political impasse' iliyopo sasa.
Na ni heri kuyatafuta maridhiano kwanza kabla ya kuingia kwenye majadiliano, kuliko kuyatafuta maridhiano baada ya kuingia kwenye kugombana. Na MARIDHIANO ndio msingi wa UHALALI wa SULUHU itakayopatikana baina ya CUF na CCM.
Maana, tusipotanguliza busara, hekima na maslahi ya taifa, yumkini yaweza ikawa kama yale aliyopata kuyasema miaka 60 iliyopita, mwandishi yule mahiri, Mtanzania mwenzetu Shaaban Robert, aliandika; ” Wasadikika wana desturi ya kutafuta fimbo baada ya kuumwa na nyoka. Tumekwisha umwa na nyoka wa matendo yetu mabaya ya zamani.
Nyoka mwenyewe amekwishakimbia. Hapatikani kwa kujilipiza kisasi, lakini, sumu yake imebakia katika jeraha tulilolipata. Sasa, shauri lililo jema ni kuzuia sumu hii isienee miilini mwetu ikaleta kifo.
Maovu yana hatari kubwa kukaa kati yetu. Tumedumu nayo kwa muda mrefu. Hayakutuletea faida ila hasara, huzuni na kilio siku zote.”- Shaaban Bin Robert.
Na Mwanafalsafa Aristotle alipata kuandika, kuwa sifa kuu ya Ufalme ni Mamlaka, maana, Ufalme huwa ni sawa na Umungu Mtu. Ufalme huzaa despotism. Na HEKIMA ni sifa kuu ya Aristocracy, kwa maana ya tabaka la Uongozi . Naam, kiongozi sharti awe ni mtu mwenye hekima.
Na viongozi wanapokosa hekima wanaingia kwenye hali ya kuwa Ma-Oligarchy. Hiki ni kikundi kidogo cha wateule lakini waliojaa ubinafsi na choyo kubwa. Ni watu wasiojali maslahi ya umma bali ya kwao binafsi na kikundi chao.
Na sifa kuu ya Demokrasia ni ridhaa ya jamii. Naam, Demokrasia hujengwa katika msingi wa mariadhiano. Ikikosekana hali hiyo, ndipo makundi ya kuhasimiana huzaliwa, na hupelekea kuzaliwa kwa kinachoitwa ' mob tyranny', yaweza kusemwa uharamia au uongozi wa kimabavu wa kikundi fulani katika jamii.
Hivyo basi, Mwanafalsafa Aristotle anapendelea zaidi uwepo wa kinachoitwa ' Polity' aina ya utawala wa mchanganyiko. Utawala wenye kuhakikisha makundi yenye kuhasimiana yanapata fursa ya kugawana madaraka ili kuwepo na ' checks and balances'- kwamba kuwepo na hali ya kudhibitiana. Ndio msingi pia wa mgawanyo wa madaraka. Nchi lazima isonge mbele.
Maggid,
Dar es Salaam.
0754 678 252
No comments:
Post a Comment