Miaka miwili iliyopita, katika kuadhimisha kumbukumbu ya kuzama Meli ya Mv.Bukoba, kwa msaada wa mtandao, niliandaa makala haya hivyo nimehariri kidogo ili kuendana na wakati, japo uhalisia wake uko pale pale.
Na George Binagi
Mei 21 Mwaka 1996 Taifa la Tanzania
liligubikwa na Msiba Mkubwa ambapo kila mmoja kwa nanma yake aliguswa na Msiba
huo ambao uliyagharimu Maisha ya Mamia ya Wapendwa Wetu, baada ya Meli ya
MV.Bukoba Kuzama hatua chache kabla ya kutua Nanga Mkoani Mwanza ikitokea
Mkoani Kagera.
Meli ya Mv.Bukoba iliyoundwa mwaka
1979 ikiwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 850 na abiria 430 ilizama katika Maji
ya Ziwa Victoria Mkoani Mwanza yapata umbali wa kilomita zipatazo 30 kutoka
ufukweni mwa maji na kusababisha zaidi ya watu 1,000 kupoteza maisha katika
Meli hiyo ambayo tangu kuundwa kwake hadi kuzama kwake ilikuwa na umri wa miaka
17. Jambo la butwaa hapa ni Idadi ya vifo na idadi ya abiria waliookolewa
ukilinganisha na Uwezo uwezo wa Meli hiyo wa kubeba abiria 430).
Pengine tumezoea kuita kwamba Mei 21
Watanzania tunaadhimisha kumbukumbu ya kuzama kwa Meli hiyo ambayo iliigeuza
taswira ya Mji wa Mwanza, kwani kwa waliokuwa Mwanza Mwaka huo walipigwa na
Butwaa baada ya Uwanja Mkongwe wa Nyamagana ambao mara nyingi hutumika kwa
shughuli za Kimichezo, pale ulipogeuka na ghafla na kutapakaa Maiti za wapendwa
wetu, ama hakika inauma sana.
Wakati leo tunakumbuka tukio hili
ambalo limeacha simanzi mioyoni mwetu, hebu tujiulize kwa pamoja; Kama ilivyo
imani ya watalaamu wa masuala ya usafiri kwamba Usafiri wa Majini ndio usafiri
salama kuliko aina nyingine ya usafiri, Je Kwa Tanzania imani hiyo ina mantiki
yoyote kwamba vyombo vyetu vya usafiri wa majini ni salama?.
Lakini wakati tunatafakari suala hilo,
pia tukumbuke kujiuliza sisi wenyewe bila kusubiri kusukumwa na mtu hususani
wale wenye mamlaka ya kuleta matokeo chanya katika kuboresha hali ya usafiri
majini Ikiwemo Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu na Majini SUMATRA kwamba tulijifunza jambo lolote kutokana na
ajali hiyo ya Mv.Bukoba?
Na Kama kuna jambo tulijifunza, je
tumefanikiwa kulifanyia kazi ipasavyo jambo hilo? Je kuna hali yoyote ya
uwajibikaji (kwa waliopewa dhana ya kusimamia sheria) katika kuzingatia sheria
za usafiri na usafirishaji wa majini na nchi kavu? Je, tumekwisha jijengea hali
ya kuchukua hatua za uokoaji pale tunapopatwa na majanga ya majini au nchi
kavu?.
Lakini pia wapo waliohoji na bado
wanaendelea kuhoji juu ya taarifa ama ripoti ya uchunguzi wa ajari hiyo ya
Mv.Bukoba kama ulifanyiwa kazi ipasavyo? Lakini pia wakiwa bado wanaendelea
kujiuliza ni ajari ngapi za vyombo vya majini zimetokea tangu kuzama kwa meli
hiyo? Hapo nadhani nawe unazikumbuka ajali kadhaa ambazo tayari zimekwisha
kutokea na kuyagharimu maisha ya Watanzania ikiwemo ile ya mv Spice Ireland
iliyotokea Septemba 10 mwaka 2011 katika Mkondo wa Nungwi kaskazini Unguja
Zanzibar.
Lakini yote Tisa, Kumi ni stofahamu
iliyoibuka juu ya Chanzo cha ajali hiyo mbaya kuwahi kutokea hapa nchini.Wapo
waliosema ilikuwa ni Uzembe wa Wakaguzi wa na Waangalizi kwa maana ya Mamlaka
husika, Wapo waliosema ilikuwa ni Uzembe wa Nahodha na Timu yake na wapo waliosema
Chombo kilikuwa kibovu.
Wapo waliodai chombo hicho
kilikuwa kimebeba Mizigo na abiria kuzidi uwezo wake na wapo waliodai kuwa
abiria wenyewe walisababisha ajali hiyo kwani walilazimisha kupanda Melini
ilihali chombo kilikuwa kimejaa huku mlolongo huo ukihitimishwa na wale
waliohusisha ajali hiyo na Imani za Kishirikina.
Mimi nasema sina nia ya kuandika hayo
yote kwa lengo la kumtafuta mchawi ila lengo langu ni kuyaweka wazi hayo yote
ili kila mmoja kwa namna anavyohusika na anavyoweza kusaidia namna ya kufanya
ili kuepukana na ajali kama hiyo ama kama ambavyo wengine husema tusiangalie
tulipoanguka bali tuangalie tulipojikwaa.
Wapo wengi waliowapoteza ndugu, jamaa
na marafiki zao na mmoja wao ambae alimpoteza mpendwa wake katika maisha yake
ni Mwanamitindo maarufu hapa nchini ambae pia anafanya shughuli zake barani
Ulaya Flavian Matata ambae yeye alimpoteza Mama yake mzazi pamoja na binamu
yake.
Pamoja na watu wengine, Matata amekuwa
na desturi ya kukumbuka tukio hilo kwa kufika Mkoani Mwanza katika eneo la
Igoma walikohifadhiwa watu waliopeza maisha katika ajali hiyo ya Mv.Bukoba
ambapo pia maadhimisho ya kuwakumbuka hufanyiia kila mwaka, huku akibainisha
kuwa ilimchukua miaka mingi hadi kuamini kuwa ni kweli hayuko na mama yake
mzazi, kwa kusema kuwa ni miaka michache iliyopita ndiyo ameweza kuamini kama
ni kweli hayuko na mama yake tena.Hakina inauma sana.
Yapo mengi ya kuzungumza na kuandika
lakini swali la kujiuliza ni moja tu, miaka 21 mwaka huu 2016 tangu kuzama meli
ya Mv.Bukoba Mei 21 mwaka 1996, Je usafiri wa majini ni salama hapa nchini ama
tunasafiri kwa kudra za Mwenyezi Mungu? Mimi nihitimishe kwa kusema ni jukumu
la kila mmoja wetu kwa kushirikiana na Mamlaka husika ikiwemo SUMATRA kuhakikisha
kuwa usafiri wa Majini Unakuwa usafiri salama hapa nchini.
No comments:
Post a Comment