Wednesday, May 31, 2017

TBS YAWASHAURI WAZALISHAJI WADOGO WADOGO WA BIDHAA KUTUMIA FURSA YA BURE YA UKAGUZI

Wazalishaji wadogo wadogo wa bidhaa nchini wameshauriwa kutumia fursa ya bure ya ukaguzi wa bidhaa zao inayotolewa na Shirika la Viwango Tanzania TBS.

Hayo yamesemwa na Afisa Masoko Mwandamizi kutoka katika shirika hilo,Gladnes Kaseka( pichani kushoto juu) wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye
maonyesho ya tano ya biashara ya Mkoa wa Tanga .

Alisema kuwa licha ya TBS kutoa fursa hiyo lakini bado wazalishaji wadogo na wakati wameshindwa kuitumia fursa hiyo kwa ukamilifu wake na kusababisha kuendelea kuwepo kwa bidhaa ambazo hazina nembo ya ubora.

"Bado wazalishaji wetu wengi hawajaweza kuifikia fursa hiyo ambayo itaweza kuwasaidia kuhakikisha wanazalisha bidhaa zenye ubora lakini wataweza kuingiza bidhaa zao kwa urahisi katika masoko ya ushindani tofauti na sasa" alisema Kaseka.

Aidha alisema kuwa bado wanaendelea na jitihada za kuhakikisha wanaziondosha katika soko bidhaa ambazo ni hafifu kwa kufanya ukaguzi wa Mara kwa Mara katika masoko na maeneo yote yanayohusika na shughuli za uuzaji wa bidhaa.

Nae Mfanyabiashara Aisha Kisoki alisema kuwa changamoto kubwa ni muingiliano wa bidhaa kutoka nje ambazo kwa hapa nchini zinauzwa kwa bei rahisi tofauti na wanazozizalisha.

Alisema kuwa iwapo TBS wataweza kudhibiti uingiaji usio rasmi wa bidhaa kutoka nje utasaidia sana wafanyabiashara wa ndani ya nchi kuona umuhimu wa kuweka nembo bidhaa zao.
Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha.

No comments: