Friday, December 14, 2007

IJUMAA SHOWBIZ

Mastaa kibao kupotezato

Lile tamasha la aina yake lililobatizwa jina la Usiku wa Mwanza, litachukua nafasi leo, Desemba 14, 2007 kwenye Ukumbi wa Lataverna uliopo Mikocheni, Dar es Salaam.

Usiku huo ambao utawakutanisha mastaa kibao wa muziki wenye asili ya Mwanza kama H. Baba, Fid Q, Dudubaya, Flora Mbasha, Rado, Costa Siboka na wengine kibao umeandaliwa na kampuni za MOFA na Baraka Entertainments ukiwa ni maalum kwa wenyeji wa mkoa huo wa Kanda ya Ziwa na wale waliowahi kuishi huko ambao hivi sasa wanaishi jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa usiku huo, Mohamed Magori alisema kwamba shoo itakuwa bab-kubwa, itaanza saa tatu usiku hadi majogoo. “Lengo la usiku huo ni kufahamiana, kubadilishana mawazo, pia kutakuwa na hotuba itakayoshushwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti UKIMWI ya UVCCM Taifa, Eric Shigongo ambayo itatoa tathmini na muelekeo wa watu wa Mwanza”.

Aidha, Magori alisema mbali na shoo kutoka kwa wasanii maarufu wa Mwanza, pia kutakuwa na mpambano mkali wa Ma-DJ, nawazungumzia John Dilinga ‘JD’, Paul James ‘PJ’ na DJ Juice ambapo kila mmoja ataonesha ubabe wake kwa kuchezea LP.

“Hatuna ubaguzi, tunamkaribisha yeyote. Kama kuna mtu ambaye hana asili ya Mwanza wala hajawahi kuishi Mwanza, lakini anatamani kujiunga na sisi katika kudumisha ushirikiano na umoja wetu, tunamkaribisha sana,” alisema Mratibu huyo.

Usiku huyo ambao unatarajiwa kuwa wa aina yake, huku kiingilio kikiwa ni shilingi 5000 kwa kila mtu, umedhaminiwa na Kampuni ya Global Publishers & General Enterprises LTD, Zizzou Fashion na TAI.
TMK Wanaume kutimiza ahadi leo

Kundi la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Family ambalo limejitoa muhanga kuwafuata mashabiki wao mpaka Uwaswahili, leo litatimiza ahadi hiyo pale litakapofanya shoo kali ndani ya Ukumbi wa Kongwa Bar uliyopo Vingunguti jijini Dar es Salaam.

Meneja wa kundi hilo, Said Fella alisema kuwa timu nzima ya Wanaume iko safi, kwani walikuwa wakijifua kimazoezi kwa muda mrefu wakijiandaa na shughuli hiyo ya utambulisho wa albamu zao tatu, yaani Kazi Ipo ya kundi, Katikati ya jiji ya Chegge na Bado Mapema ya Stiko.

“Mbali na albamu hizo, meneja huyo alisema kwamba vijana pia watatambulisha staili mpya kibao, tofauti na hiyo moja, Konzi moja manundu elfu kumi ambayo watu wanaifahamu.

“Pia kuna kazi mpya kutoka kwa KR, Temba na wengine ambazo kwa mara ya kwanza masela watapata fursa ya kuzisikiliza siku hiyo”.

Naye mauandaaji wa shughuli hiyo, George Alphonce alisema kwamba mashabiki wa Vingunguti watapata kuishuhudia shoo hiyo kwa shilingi elfu mbili mia tano tu, wale watakaopatia kucheza staili za kundi hilo wataondoka na zawadi mbalimbali zitakazotolewa ukumbini hapo.

BSS sasa tumbo Joto

Shindano la kumtafuta mkali wa kuimba nchini, Bongo Star Search (BSS 2007) linazidi kuelekea patamu ambapo mchujo kwa washiriki 20 waliobaki kundini unawapa wakati mgumu, Julius Kihampa alipiga stori na Madam Ritta.

Washiriki hao ambao wamepiga kambi katika Hoteli ya Giraffe Greenview iliyopo pembezoni mwa Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam, wanaendelea kujifua kwa mazoezi ya kuimba na kucheza chini ya wakufunzi wa muziki nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Benchmark Production ambao ndiyo waandaaji wa shindano hilo, Rita Paulsen amewataka washiriki hao kuzingatia mafunzo waliyopewa bila kusahau nidhamu.

“Wajifue ili waweze kuionesha jamii kitu gani wanafanya, kwani katika hatua hii watatolewa na watazamaji wa kituo cha televisheni cha ITV kwa kura zao, ila wasisahau nidhamu,” alisema Madam Ritta.



No comments: