
UNASUMBULIWA NA UGONJWA WA MOYO? SOMA HAPA!-2
Wiki iliyopita tulianza makala haya kwa kuangalia tataizo la ugonjwa wa moyo na jinsi ya kukabiliana nao kwa kutumia matunda, mboga na vyakula vingine kwa mpangalio unaokubalika.
Aidha tuliona kuwa chanzo kikubwa cha matatizo ya moyo ni kuishi staili mbovu ya maisha na kula vyakula visivyofaa au kukosaha lishe stahili. Leo tunaendelea kwa kuangalia orodha ya vyakula vilivyobaki vinavyoaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na tatizo hili linaloua watu wengi duniani...
ASALI KAMA TIBA YA MOYO
Asali, kama inavyojulikana, ina faida nyingi mwilini na katika suala la kupambana na ugonjwa wa moyo, nayo haikubaki nyuma. Inaelezwa kuwa asali ina virutubisho vya ajabu katika kuzuia matatizo yote ya moyo. Asali ina wezo wa kuusafisha moyo na kuboresha mzunguko wake wa damu.
Aidha, asali ikitumika ipasavyo, huasaidia haraka kuondoa maumivu ya moyo na moyo kwenda mbio. Asali kijiko kimoja cha chakula, ikitumiwa kila siku baada ya mlo, inatosha kabisa kukupa kinga ya magonjwa yote ya moyo.
Kwa mtu anayejali afya yake, matumizi ya asali ndiyo yanayochukua nafasi ya sukari ya kawaida iliyozoeleka na kutumia na watu wengi. Asali hutumika kwenye chai, maziwa au kinywaji chochote kinachohitaji sukari, hivyo ili kujiweka katika afya bora wakati wote, anza sasa kunywa chai, maziwa au uji ulioungwa kwa asali; utamu utabaki palepale na hakuna madhara ya kiafya, bali utakuwa unajipa tiba au kinga ya mwili.
VITAMINI E KAMA TIBA YA MOYO
Wagonjwa wa moyo wanashauriwa kula kwa wingi vyakula vyenye kiwango kikubwa cha vitamini E, kwasababu huimarisha utendaji kazi wa moyo. Halikadhalika huimarisha mzunguruko wa damu na misuli. Vyakula visivyokobolewa na mboga za kijani, hasa majani ya nje ya kabichi, yana kiwango kikubwa cha Vitamini E.
Ili upate faida za virutubisho vilivyomo kwenye nafaka, saga mahindi bila kuyaloweka wala kuyakoboa ili kupata unga bora kwa ajili ya ugali na uji. Halikadhalika kwenye ngano, kula mikate ‘myeusi’ badala ya myeupe ambayo virutubisho vyake huwa vimeondolewa.
VITAMIN C KAMA TIBA YA MOYO
Nayo Vitamin C ni muhimu katika kutibu ugonjwa wa moyo, kwani huzuia nyufa kwenye kuta za mishipa ya damu ambazo husababisha mshituko wa moyo. Vile vile hutoa kinga dhidi ya kolestro.
Aidha, mgandamizo wa moyo unaosababishwa na hasira, wasiwasi, fadhaha na mawazo mengine, hupandisha shinikizo la damu mwilini, lakini panapokuwa na kiasi cha kutosha cha vitamin C mwilini, hali hiyo haiwezi kuleta madhara yoyote. Chanzo kizuri cha vitamin C ni matunda jamii ya machungwa, limau, n.k. (citrus fruits)
LISHE YA MGONJWA WA MOYO
Sharti la msingi kwa wagonjwa wote wa moyo ni lishe na hasa lishe ya mboga na matunda, kiwango kidogo cha chumvi na kalori. Chakula kiwe kiasi kikubwa ni cha asili na hai, huku mkazo ukitiliwa kwenye vyakula vitokanavyo na nafaka zisizo kobolewa. Vyakula vya kuepuka ni vile vinavyotengenezwa kwa unga wa ngano mweupe, chai, kahawa, tumbaku, pipi, mafuta ya wanyama, siagi na krimu. Sukari na chumvi zitumike kwa uchache sana.
TIBA NYINGINE ZA MOYO
Mgonjwa wa moyo hana budi kuzingatia kanuni za ulaji sahihi na kuishi, kama vile kufanya mazoezi ya viungo ya wastani mara kwa mara, kupata nafasi ya kutosha ya kupumzika, kupata usingizi na kuwa na mawazo chanya kuhusu maisha. Staili nzuri ya maisha ni tiba tosha pia.
Tiba zote mbadala zinaposhindikana, tiba pekee ya mwisho huwa ni upasuaji ambao ni ghali sana na mara nyingi hufanyika nje ya nchi, ambako watu wengi hushindwa kwenda na hivyo kupoteza maisha yao.
Okoa maisha yako sasa na gharama zisizo za lazima kwa kula vyakula sahihi na kuishi maisha yaliyombali na karaha, mashaka na uvivu. Kuwa mtu unayejali sana kile unachokula kina faida gani mwilini mwako. Tuache ili kasumba ya kupenda vitu vyenye ladha tamu mdomoni lakini isiyo na faida yoyote mwilini.
Mara nyingi watu wengi tunakosa virutubisho muhimu kwenye miili yetu kutokana na kupenda kula vyakula kwa kigezo cha utamu. Watu tunapenda kunywa soda zaidi kuliko maji kwa sababu soda ni tamu na maji hayana utamu. Tunapenda kula nyama badala ya mboga za majani kwa sababu tu nyama ni tamu kuliko mchicha au kabichi. Tabia hii hatuna budi kuiacha kama kweli tunataka kujiepusha na maradhi sugu, ikiwemo ugonywa wa moyo.
No comments:
Post a Comment