Saturday, June 9, 2018

MWENYEKITI CCM IRINGA KUNYANG’ANYA KADI WANACHAMA WANAOVUNJA KANUNI,SHERIA NA KATIBA YA CHAMA

 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Albert Chalamila ametoa onyo kali kwa wana CCM wanaokiuka kanuni na katiba ya chama cha mapinduzi kwa kuanza kampeni za chini kuwania ubunge na udiwani katika majimbo matatu ya wilaya ya Mufindi akisema wanakwenda kinyume na kanuni za uongozi na maadili.
Baadhi ya viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) wa wilaya ya Mufindi wakimusikiliza kwa umakini mkubwa
mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Albert Chalamila wakati wa ziara yake ya kwanza ya kikazi 
Baadhi ya wanahabari wa mkoa wa Iringa wakiwa kazini kupata habari kutoka kwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Albert Chalamila
 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Albert Chalamila akipokelewa na green gard wa wilaya ya Mufindi na kupewa heshima anayostahili
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Albert Chalamila akivishwa skafu nagreen gard wa wilaya ya Mufindi 

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Albert Chalamila ametoa onyo kali kwa wana CCM wanaokiuka kanuni na katiba ya chama cha mapinduzi kwa kuanza kampeni za chini kuwania ubunge na udiwani katika majimbo matatu ya wilaya ya Mufindi akisema wanakwenda kinyume na kanuni za uongozi na maadili.

Akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya wilaya hiyo mjini Mafinga,Chalamila alisema kuwa amesikia kuwa kuna wanachama wameanza kupita pita kuanza kufanya kampeni za chini chini na kusababisha wapunge wa majimbo hayo kutofanya kazi zao kwa ufanisi. 

Chalamila aliyataja Majimbo ambayo wananchama hao hao wameanza kupita ni jimbo Mafinga Mji linaloongozwa na Mbunge Cosato Chumi, jimbo la Mufindi Kaskazini Mahamudu Mgimwa na Mufindi Kusini Meldrad Kigolla.

Alisema kuwa anafanyakazi kwa ukaribu na vyombo ya usalama wa taifa ili kupata taarifa ambazo ni sahihi na kuwabaini baadhi ya wana CCM walioanza kujitengenezea mazingira kwa ajili ya kupata uteuzi katika uchaguzi mkuu ujao kinyume na kanuni hizo za chama.
  
Chalamila aliwataka viongozi waliochaguliwa na wananchi kufanya kazi kwa kujituma na kukitendea haki chama cha mapinduzi (CCM) ili kiendelee kuaminiwa na wananchi 

Aidha Chalamila alisema katika mazingira ya kusikitisha alisema wana CCM wengine wanaoshiriki kuhatarisha amani ndani ya chama hicho ni wale waliopewa dhamana ya kuwa wajumbe wa vikao vikubwa vya chama na katika onyo lake kwao aliwatahadharisha dhidi ya hatua zinazoweza kuchukuliwa kwao.

“Waacheni wabunge na madiwani waliopo wafanye kazi, wamalize miaka yao mitano kwa uhuru. Mliwachagua wenyewe, wapeni nafasi na kama mnataka kuamua vinginevyo subirini hadi pazia la uchaguzi litakapofunguliwa lakini sio sasa,” alisema Chalamila.

Mwenyekiti  huyo aliwataka wajumbe  hao,kuhakikisha wanaweka mikakati  ya ushindi katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa kuhakikisha wanazirudisha ndani ya ccm  kata  2 zilizochukuliwa na Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wilayani humo.

Chalamila alizungumzia visasi na mioyo ya kinyongo miongoni mwa wana CCM wakati na baada ya chaguzi za chama na jumuiya zake, na za serikali akisema; mambo hayo yamekuwa yakisabisha mpasuko wa muda mrefu ndani ya chama hivyo ni lazima yaachwe.

“Visasi na vinyongo vimevuka mipaka. Wapo pia wana CCM ambao kila kukicha kazi yao ni kuwazushia na kuwachafua wenzao kwamba ni wafuasi wa vyama vingine vya siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kwamba wana mienendo mibaya ndani ya chama mambo ambayo si ya kweli. Wana CCM tupendane na tutendeane mema,”alisema Chalamila.

Aliwataka wenye taarifa za wanachama wenye mienendo mibaya na inayotishia uhai wa chama waziwasilishe kwa kuzingatia taratibu, kanuni na katiba ya chama ili ziweze kufanyiwa kazi.

Mwenyekiti Chalamila alimalizia kwa kusema kuwa watawanyang’anya kadi wanachama wote ambao watakuwa wanaendelea kuvunja kanuni,sheria na katiba ya chama cha mapinduzi

“Kwakweli nitakuwa mkali sana na nitasimamia vilivyo kwa wale ambao watakuwa wanavunja kanuni,sheria na katiba ya chama cha mapinduzi kwa kuwa madaraka hayo ninayo kwa mujibu wa kanuni na sheria za chama chetu” alisema Chalamila

Baada ya kukutana na halmashauri kuu ya CCM ya wilaya ya Mufindi, Chalamila anatarajiwa pia kukutana na na wajumbe wa vikao hivyo wa wilaya ya Kilolo, Iringa Vijijini na Manispaa ya Iringa katika ziara yake anayofanya akiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Viti 15 Bara), Theresia Mtewele

No comments: