Watu wengi tunakula vyakula ambavyo baadae vinageuku kuwa sumu na kutudhuru bila sisi wenyewe kujijua kutokana na kutokuzingatia ile dira ya vyakula. Hili ndilo suala ambalo kila mmoja wetu anapaswa kulijua na kulizingatia kila inapokuja suala la kula. Kabla hujala chkula chochote, ni vyema ukajua kinafaida gani mwilini mwako na unatakiwa ukile kwa kiwango gani.
Kwa mujibu wa dira ya vyakula, (FOOD PYRAMID) ambayo imependekezwa na wanasayansi wetu maarufu duiniani, vyakula vinavyopaswa kuliwa kwa wingi ni vyakula vyote vitokanavyo na nafaka, kama vile ugali, mikate, wali, uji, tambi, n.k.
Katika kundi hili inasisitizwa sana kupenda kula vyakula hivyo kutokana na nafaka halisi ambazo hazijaondolewa virutubisho vyake vya halisi, ili kupata faida inayopatikana kwenye vyakula hivi. Mfano, ugali uliyo bora ni ule uliyotayarishwa kutokana na unga wa mahindi yasiyokobolewa, kwa maana nyingine ugali utokanao na unga mweupe sana hauna virutubisho vya kutosha.
Matayarisho ya vyakula vitokanavyo na nafaka hizo ni muhimu sana, kwani watu wengi huandaa nafaka hizo na katika mchakato hujikuta wanaondoa virutubisho muhimu na kubaki na chakula kisichokuwa na virutubisho muhimu. Kwa mafano kitendo cha kokoboa na kuloweka mahindi kwa muda mrefu huondoa virutubisho vyote muhimu.
Vyakula vinavyofuata kwa umuhimu ni matunda na mboga mboga. Vyakula hivi vinatakiwa kuliwa kwa wingi, hasa mboga za majani, wastani wa milo 3-5 kwa siku. (mlo mmoja ni sawa na kisahani kimoja cha chai) na matunda yaliwe wastani wa milo 2 – 4.
Orodha ya vyakula hivi ni muhimu sana katika mwili wa binadamu kwa sababu katika mboga na matunda tunapata kinga ya maradhi mbalimbali yanayoweza kujitokeza iwapo mwili hauna kinga ya kutosha. Hivyo ulaji wa mboga za majani na matunda si umasikini wala anasa, bali ni suala muhimu na ni la lazima katika mwili wa binadamu.
Kundi linalofuatia kwa umuhimu ni vyakula kama vile nyama, samaki, maziwa, mayai, karanga, maharage, n.k. Kundi hili nalo ni muhimu, lakini linahitaji tahadhari katika ulaji wake, hasa kwa upande wa nyama na maziwa. Nyama iliwe kwa kiasi kidogo na iwe ‘steki’ isiyokuwa na chembe ya mafuta (lean meat), kwani mafuta ya wanyama kwa ujumla yana madhara kiafya hivyo haishauriwi kula nyama zenye mafuta.
Kwa upande wa maziwa, tahadhari pia inapaswa kuchukuliwa kwani si maziwa yote ni mazuri kwa afya yako. Maziwa bora kwa afya ni yale yasiyokuwa na mafuta (skim milk) au fat free. Usipende kunywa maziwa aina ya full cream, kwani aina ya mafuta yaliyomo kwenye maziwa hayo si mazuri kwa afya. Kama unaandaa mwenyewe maziwa, engua utandu wa juu (malai) ndiyo unywe maziwa hayo, malai ndiyo kiini cha mafuta mabaya, hivyo yaepuke.
Fungu la mwisho ni vyakula vyenye sukari, mafuta aina zote (fats na Oils) na vyakula vingine vitamu vitamu kama vile soda, ice cream, pipi, n.k. Kundi hili la vyakula linapaswa kuliwa kwa uchache sana, kwani mahitaji yake mwilini ni madogo na virutubisho vyake vinaweza kupatikana kwenye makundi mengine ya vyakula, kama mboga na matunda.
Huo ndiyo mpangilio sahihi wa vyakula ambao ukizingatiwa ipasavyo mwili huwa salama na si rahisi kushambuliwa na maradhi. Lakini kwa bahati mbaya sana, ‘piramidi’ hiyo imegeuzwa. Vyakula vinavyotakiwa kuliwa kwa uchache ndiyo vinaliwa kwa wingi na vile vinavyotakiwa kuliwa kwa wingi, vinaliwa kwa uchache! Matokeo yake ni kuibuka kwa maradhi hatari kila siku!
No comments:
Post a Comment