Tuesday, July 22, 2008

IJUE PIRAMIDI YAKO YA CHAKULA

Katika zama tuliyonayo, hali ya maradhi inatisha, kila kukicha watu wanakufa kutokana na maradhi karibu yanayofanana, kama vile shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo, kisukari, saratani, figo kufeli, ini kuharibika, n.k. Hata tulio hai, kila mmoja wetu anasumbuliwa na ugonjwa huo mmoja au zaidi na kwa hakika magonjwa hayo yote yanaepukika.

Katika kuugua, kila mtu anaweza kuwa na mtizamo wake. Wapo wanaoamini kuwa maradhi hayaepukiki na wapo wanaoamini kuwa maradhi yanaepukika. Kiimani ya dini, inaaminika kuwa ni Mungu pekee ndiye mwenye uwezo wa kumnusuru binadamu na maradhi yote na wala hakuna binadamu anayeweza kusema hawezi kuugua.

Imani hiyo ina ukweli, kwa sababu binadamu kwa uwezo wake hawezi kuepuka maradhi yote yaliyopo duniani, kwani ukiwa unajikinga na ugonjwa mmoja, utakabiliwa na ugonjwa mwingine, hiyo inabaki kuwa ishara nyingine ya uwezo wa kipekee alionao Mungu, Muumba wa vitu vyote hapa duniani.

Lakini pamoja na ukweli huo, Mungu ni mwema sana kwetu sisi, kwani ametupa neema ya vyakula vya kila aina, ambavyo ndani yake tunapata tiba na kinga ya maradhi yote, iwapo tu tutaweza kufuata utaratibu aliotuwekea katika kutumia neema hiyo.

Kwa bahati mbaya sana, wengi wetu hatujui njia sahihi ya kutumia neema hiyo, matokeo yake neema hiyo imegeuka kuwa balaa na zana ya kutuangamizi kila siku. Chakula, ambacho kilipaswa kuwa kinga na tiba ya maradhi mwilini, imegeuka kuwa sumu na chanzo cha maradhi mengi yanayotukabili sasa.

Hali hii inatokea bila wenyewe kujua, wala hakuna anayeonekana kujali, si serikali wala wananchi wenyewe. Hili ndiyo tatizo la msingi ambalo hatuna budi kulishughulikia kikamilifu kwa kukumbushana na kupeana elimu kuhusu ulaji sahihi na kwamba wajibu wa kujiepusha na maradhi unaanza na mtu mwenyewe.

Kila mtu anapaswa kujujitambua kuwa mwili wake unahitaji nini, kama vile dereva navyopaswa kuelewa kuwa ili gari litembee linahitaji mafuta, maji, upepo kwenye magurudumu, n.k. anapoendesha gari huku likiwa halina maji, injini ‘itanoki’ na likiwa halina mafuta, haliwezi kuwaka.

Chakula tunachokula kila siku, kimewekwa katika makundi makuu manne. Kila kundi moja linatofautiana na kundi jingine kwa upande kiwango cha kula. Kundi moja la chakula linapokosekana au linapozidi mwilini, husababisha upungufu wa virutubisho na matokeo yake huwa ni kujitokeza kwa tatizo moja au zaid la kiafya (ugonjwa).

Makundi hayo manne yanajulikana kwa lugha ya kiingereza kama FOOD PYRAMID ambayo ndiyo dira inayopaswa kufuatwa na kila mmoja wetu. Wiki ijayo tutaichambua na kuieleza kwa kina dira hiyo.

Itaendelea wiki ijayo..

No comments: