Tuesday, August 5, 2008

Ubuyu una kinga kubwa ya mwili!

YOU ARE WHAT YOU EAT!
Inaaminika na baadhi ya watu kuwa ubuyu ni tunda lisilokuwa na thamani sana, kwani hata mtu akiwa anafanya biashara ya kuuza ubuyu hudharaulika, pengine ni kutokana na watoto na watu wa hali ya chini kupenda kutumia.

Lakini habari za hivi karibuni zinatoa taswira tofauti kuhusu tunda hili. Taswira hii inaweza kabisa kubadilisha mtazamo wa baadhi ya watu waliokua wakilidharau tunda hili. Hivi karibuni Jumuiya ya Ulaya (EU) imeidhinisha kuingizwa kwa tunda hili barani humo kama tunda la kibiashara baada ya kampuni ya PhytoTrade Africa kupewa kibali cha kuingiza tunda hilo kutoka Afrika.

Kampuni hiyo hivi sasa imeruhusiwa kuingiza ubuyu katika bara hilo na kutumiwa na wananchi wake kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuchanganya na vyakula mbalimbali vya nafaka ili kuongeza virutubisho.

Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi, Ubuyu una kiwango kikubwa cha Vitamin C kuliko chungwa. Imegundulika kuwa kiasi cha gramu 100 ya ubuyu ina miligramu 300 za vitamin C, kiasi ambacho ni mara sita zaidi ya kile kinachopatikana kwenye tunda kama chungwa ambalo ndilo linaaminika kuwa na kiwango kikubwa cha vitamin hiyo.

Kama inavyojulikana, Vitamini C ni muhimu sana mwilini kwani ndiyo inayotukinga dhidi ya magonjwa nyemelezi mbalimbali yanayoweza kutupata pale mwili unapokuwa hauna kinga ya kutosha, ndiyo maana hata hapa nchini imekuwa ikisisitizwa na wataalamu wetu wa lishe kuwa wagonjwa wenye upungufu wa kinga mwilini au wenye virusi vinavyosababisha Ukimwi, wapende kutumia ubuyu ili kuongeza kinga zao.

Hii inatokana na ukweli kwamba ubuyu una virutubisho vingi vya kulinda mwili. Inaelezwa pia na watafiti kuwa ubuyu una vitamini muhimu inayojulikana kama Vitamini B2 ambayo huimarisha ukuwaji wa nyama, ngozi na wa nuru ya macho. Halikadhalika kuna vitamini B3 ambayo ni muhimu kwa uimarishaji wa mchakato wa umeng’enyaji wa chakula mwilini.

Mbali ya vitamini, ubuyu pia una madini na mafuta aina ya ‘fatty acids’. Gramu 100 za ubuyu ina kiasi cha miligramu 293 za madini aina ya kashiamu, miligramu 2.31 za potasiamu na miligramu hadi 118 za fosforasi (phosphorus). Hivyo utaona ubuyu ni muhimu kiasi gani kwa mwili wa binadamu kutokana na kusheheni vitamini na madini hayo kwa wingi.

Aidha, ubuyu unatibu pia ugonjwa wa kuharisha kama vile ambavyo umekuwa ukitumiwa enzi na enzi na mababu zetu walipokutwa na tatizo la Kipindupindu au mfumko wa magonjwa ya kuharisha na kutapika.

Kwa mujibu wa habari za hivi karibuni, biashara ya ubuyu inatarajiwa kuongezeka barani Afrika, hasa nchini au mikoa inayolima tunda hili kwa wingi, kama vile Mkoa wa Dodoma na mingine.

Kampuni hiyo iliyoomba na hatimaye kukubaliwa kupewa kibali cha kuingiza ubuyu barani Ulaya, imesema kuwa inatarajia kufanya biashara ya Paundi za Uingereza milioni 500, ambazo ni zaidi ya shilingi za Kitanzania Bilioni 1000 kwa mwaka, hii ina maana kwamba ubuyu utakuwa ni zao linalowaingizia fedha nyingi sana wakulima wake pamoja na taifa kwa ujumla.

Kwa ujumla ubuyu siyo tunda la kudharau kama ambavyo baadhi ya watu hujaribu kuonesha, anza sasa kupenda matumizi ya ubuyu kwa faida ya afya yako, kwani utafiti umeshathibitisha zao hili lina virutubisho vingi na muhimu kwa afya ya binadamu.

No comments: