Tuesday, October 21, 2008

Matatizo ya kibofu cha mkojo kwa wanaume


Ni safari ndefu kwa mwanaume kufikisha umri wa miaka 50, lakini katika umri huo pia ndiyo matatizo mengi ya kiafya huanza kujitokeza, likiwemo tatizo la kibofu cha mkojo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, watu wanne kati ya watano hupatwa na matatizo ya kibofu cha mkojo wanapofikisha umri wa miaka 50. Inaelezwa pia kuwa karibu asilimia 80 ya watu wenye umri wa miaka 60 hupatwa na tatizo la kibofu.

Kuna aina nyingi za matatizo ya kibofu cha mkojo ambayo mtu anaweza kuyapata, mengi ya matatizo hayo yanaweza yasiwe na maumivu sana lakini hutoa usumbufu wakati wa kutoa haja ndogo ambayo mwanzoni hutoka kwa shida.

Tatizo la kibofu linapoanza kukomaa kwa mgonjwa, huweza kusababisha maumivu fulani hata kwa viungo vingine kama vile mgongo na ‘hips’, miguu na kwenye nyayo ikiwa ni dalili ya kuanza kukomaa kwa ugonjwa.

SABABU
Zinaweza zikawepo sababu nyingine, lakini sababu zinazojulikana zaidi kusababisha matatizo ya kibofu cha mkojo kwa wanaume wengi ni kama ifutavyo:

Kukaa sehemu kwa muda mrefu mkao wa aina moja. Hali hii huweza kuwapata baadhi ya watu maofisini wenye kazi za kukaa kwa muda mrefu na ambao hawapendi kufanya mazoezi mara kwa mara. Hivyo jiepushe na kazi za kukaa mkao mmoja kwa muda mrefu, ni hatari kwa afya yako ya uzeeni.

Matatizo sugu ya kibofu cha mkojo wakati mwingine husababishwa na hali ya hewa, hasa mtu anapopigwa baridi kali kwa muda mrefu. Aidha mtu pia anaweza kupatwa na matatizo haya kutokana na kuugua magonjwa ya kuambukiza.

Vile vile inaelezwa kwamba kadri umri unavyosonga mbele, ndivyo mtu anavyoongezeka uzito na hupoteza ulaini wa viungo, hivyo kufanya sehemu za nyonga kuelemewa na mzigo wote kuangukia kwenye kibofu.

Sababu nyingine inayoweza kusababisha mtu kupatwa na matatizo ya kibofu uzeeni, ni kuwa na tatizo la kukosa choo kwa siku kadhaa mara kwa mara.

KINGA
Jiepushe na unywaji wa ‘kafeni’ kwa wingi ambayo hupatikana zaidi kwenye chai, kahawa na chokoleti. Japo chai ina faida nyingine nyingi mwilini, lakini ikizidi sana huchangia kubana njia ya mkojo hivyo kuifanya hali ya mtu mwenye tatizo hili kusikia maumivu zaidi wakati wa kukojoa.

Aidha, inaelezwa pia kuwa unyaji wa kilevi uepukwe kwani huchangia kuziba kwa njia ya mkojo, ingawa hoja hii inapingwa na baadhi ya watu, hasa wale wanaotetea kilevi, wanasema kuwa watu wengi wanaokunywa bia huwa hawasumbuliwi na matatizo ya kibofu cha mkojo.

Vile vile, ili kujiepusha na uwezekano wa kupatwa na matatizo ya kibofu cha mkojo uzeeni, jiepushe na ulaji wa viungo vingi (spices), hasa pilipili, kupitia vyakula unavyokula kila siku.

Jiepushe na kuishi maisha yenye mawazo, hasira na ghadhabu, kwani hali hii huongeza uvimbe kwenye kibofu kutoka na kuzalishwa kwa wingi kwa homoni za kibofu pale mtu anapokuwa kwenye mfadhaiko wa akili, hii ni kwa mujibu wa wanasayansi wetu.

Penda kujisaidia haja ndogo kabla ya kwenda kulala ili kusafisha kibofu chako na inalezwa pia kuwa njia bora zaidi ya kusafisha kibofu cha mkojo ni kufanya tendo la ndoa kwani manii huondoa vizuizi vinavyozuia mkojo kupita kwenye kibofu.

Mwisho, inashauriwa kuwahi hospitali mapema pale unapoona dalili za kusumbuliwa na kibofu ili kupata tiba mapema kabla ya hali kuwa mbaya. Asanteni.

No comments: