Friday, July 31, 2009

IJUMAA SHOWBIZ!

kanumba
Mercy
Femi
France

Kanumba kuingiza kitaani The Director na Wanigeria
Msanii maarufu wa filamu nchini, Steven Kanumba anatarajia kutoa filamu mpya inayokwenda kwa jina la The director ambayo inaelezwa kuwa itakuwa ni moto wa kuotea mbali.

Kanumba ameitonya safu hii kuwa, katika filamu hiyo ya Kiswahili itakayofichua kinachofanywa nyuma ya pazia wakati wa kurekodi filamu za kibongo, amewashirikisha wasanii wakali kutoka Nigeria ambao ni Nkiru Sylvanus, Mercy Johnson ‘Ble Ble’, Emmanuel Francis na Femi Ogdebe.

Mbali na wanaijeria hao pia yumo Elizabeth Chijumba ‘Nikita’, Halfan Ahmed ‘Kevin’ na Suzan Lewis ‘Natasha’.

“Kwa kweli itakuwa ni filamu ya aina yake ambayo huenda ikafunika zote nilizowahi kuzitoa na naamini mashabiki wangu wataifurahia,”alisema Kanumba.
Kwa mujibu wa Kanumba, Filamu hiyo imeandaliwa chini ya Kampuni ya The Game 1st Quality itakuwa mtaani siku chache zijazo.

Wakati huo huo, Kanumba anasubiriwa katika mazoezi ya filamu ya Tears on Valentines inayoandaliwa chini ya Kampuni ya Tollywood Movies yaliyoanza mwanzoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam.

**********************************


Madhila-2
Kuteka soko la filamu Nchini
Kwa mara nyingine Kampuni ya Usambazaji wa filamu nchini, Tollywood Movies, inakuletea ‘movi’ ya kusikitisha na kusisimua, Madhila Part II, ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu na wapenzi wa Bongo Movies, hasa wale waliobahatika kuiona Part One.

Filamu hiyo, ambayo ni muendelezo wa hadithi ya unyanyasaji aliofanyiwa kijana Salu kutokana na ulemavu wake, imeigizwa kwa kiwango cha hali ya juu na wahusika wamebeba uhalisia wa hadithi nzima na itakapodondoka mtaani siku chache zijazo bila shaka itateka kwa muda soko la filamu nchini.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Meneja Mradi wa Kampuni hiyo, Abdallah Mrisho, alisema kuwa baada ya mashabiki kufaidi uhondo wa filamu ya Roho Sita, ni wakati mwingine wa kufaidi uhondo wa Madhila -II ambayo imechukuliwa na kampuni yake baada ya kuridhika na ubora wake.

“Baada ya mashabiki wa Bongo Movie kufaidi uhondo wa Roho Sita, sasa tunawaletea Madhila -II ambayo nayo ni nzuri sana,” alisema.

Baadhi ya mastaa wa filamu hiyo ni pamoja na Salum Mbwana (Salu), Richard Mshanga (Masinde) Riyama Ally na wengine wengi
*********

Battlefield yazidi kumng’arisha
Staa wa Marekani, Jordin Brianna Sparks yupo juu ya mstari baada ya albamu yake mpya inayokwenda kwa jina la Battlefield kuzidi kumweka matawi ya juu.


Kabla ya Battlefield, Jordin alikuwa akisumbua na albamu yake ya pili iliyopatikana kwa jina la Jordin Sparks ambayo ilitoka Novemba 20, 2007 ikiwa na nyimbo zilizotamba vibaya kama vile One Step at a Time na No Air ambayo alikamua ‘ojino’ mwenyewe kabla ya kumpa featuring Criss Brown katika remix.

Agosti 29, 2006, Jordin alitoa albamu yake ya kwanza aliyoisimamia mwenyewe, iliyokwenda kwa jina la For You lakini haikuvuma kihivyo.

Jordin Sparks na Battlefield ambayo ilitoka tangu Julai 7, mwaka huu zipo kwenye lebo kongwe katika muziki ya Jive.

“Nilifarijika sana kukamilika kwa albamu ya Battlefield, mashairi yake ni funga kazi, nimelitambua hilo, kwani siku zote nimekuwa nikipenda kuandaa mashahiri mazuri,” Sparks aliiambia televisheni ya MTV.
Khalid Chokaraa Kizimbani kwa madai ya kumtusi Afande!
Mwimbaji nguli wa Bendi ya African Stars ‘Wana wa kutwanga na kupepeta’ Khalidi Chokoraa juzi kati alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Magomeni kwa madai kwamba, Julai 27, maeneo ya Magomeni Mikumi, jamaa alisimamishwa na askari, WP 3022 Koplo Janeth na kukataa huku akimrushia matusi.

Hata hivyo, katika shitaka hilo mashahidi wa mshtakiwa ambaye ni Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka a.k.a Iron Lady alidai mahakamani hapo kuwa, kitendo hicho hakikufanywa na msanii wake.

“Askari wengine waliokuwa na askari huyo aliyemsimamisha walimshika Chokoraa huku wakimshinikiza mwenzao kumpeleka kituoni, lakini Chokoraa hakutoa matusi yoyote,” alieleza Baraka.

Kufuatia msanii huyo kukana shitaka lililokuwa linamkabili, hakimu Mwanaidi Madeni aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 11, mwaka huu na Chokoraa kuachiwa kwa dhamana aliyowekewa na Asha Baraka, Halima Kimwana pamoja na mke wake.
**********
COMPILED BY WALTER & LUQMAN

No comments: