Wednesday, August 12, 2009

Fungua kinywa na kilicho bora kiafya


KWa maisha ya watu wengi nchini mwetu, chakula cha kwanza kuingia mwilini huwa ni ama chai, maziwa au soda na kufuatiwa na vyakula vya kupika na mafuta kama maandazi vitumbua, n.k., vyakula ambavyo viko kwenye kundi la vyakula hatari na ambavyo hutakiwa kuliwa kwa tahadhari kubwa.

Hiyo siyo staili nzuri sana ya maisha, kwa kuanza siku yako nyingine aliyokujaalia Mungu kwa kula chakula kisichohitajika sana na mwili, siyo jambo zuri. Badala yake mwili unahitaji chakula asilia ili uweze kujijenga na kujiweka sawa kwa kupambana na maadui wapya wa siku hiyo.

Hivyo, wataalamu wetu wanatushauri kuanza siku vyema kwa kula tunda lolote salama, juisi ‘fresh’ ya aina yoyote au maji angalau tu. Vitu hivi ni bora na muhimu sana kuanza kuingia tumboni badala ya vyakula vingine vya kukaanga. Hata kama huna uwezo wa kununua matunda mengi, lakini angalau anza kwa kula hata chungwa moja au ndimu, ambayo faida yake mwilini ni kubwa kuliko sukari.

Unaweza kushindwa kununua matunda au kutengeneza juisi, lakini huwezi kushindwa kupata maji ya kunywa. Kama tunavyoambiwa kila siku, maji ni kitu muhimu sana katika mwili wa binadamu na kuanza kunywa maji asubuhi, hasa ya uvuguvugu, ni dawa kubwa sana ya maradhi mengi na ni ufagio mzuri wa kuondoa mafuta na mabaki mengine katika njia ya mfumo wa damu mwilini. Watu wengi huogopa kunywa maji asubuhi kwa kudhani wataumwa tumbo, ukweli ni kwamba huwezi kuumwa tumbo kwa kunywa maji, muhimu ni kuhakikisha yawe safi na salama.

Maji yanaweza kukutibu tumbo kwani hata kama una matatizo ya kupata choo, kwa kunywa maji mengi asubuhi choo hufunguka na kuwa laini. Hivyo baada ya kuanza siku yako kwa kutanguliza chakula asilia tumboni mwako, iwe tunda, juisi au maji, kaa angalau kwa muda wa nusu saa ndiyo ule mlo wako kamili wa asubuhi. Kama umezoea kunywa chai asubuhi, jaribu kunywa chai yenye mchanganyiko wa viungo vingine kama tangawizi au mdalasini.

Aidha, kinywaji bora zaidi kuanza nacho baada ya kufungua kinywa na matunda ni Uji, hasa wa ulezi uliotengenezwa kwa kuzingatia suala la virutubisho. Usianze kufungua kinywa asubuhi kwa kunywa soda, ambayo haiingizi kirutubisho chochote mwilini mwako, zaidi ya kukuongezea sukari ambayo inapokuwa nyingi huweza kunenepesha na kuwa chanzo cha magonjwa mengine hatari.

Aidha, unywaji supu ya nyama ya ngo’mbe au mbuzi asubuhi, nao siyo mzuri sana. Vyakula vitokanavyo na wanyama vingi huwa na mafuta, ambayo tumeshaona ni miongoni mwa vyakula hatari. Ieleweke kwamba si vyakula vyote vyenye ladha ya utamu mdomoni ni vizuri tumboni, chakula kinaweza kuonekana kizuri mdomoni, lakini tumboni kibaya.

Na ni wazi kwamba ukila vizuri utakuwa na afya njema na bila shaka ukila vibaya, utakuwa na afya mbaya, maradhi yatakuwa hayakuishi. Tunapaswa kujua kula vizuri ni kupi nakula kubaya ni kupi.

Kanuni ambayo unaweza kuitumia ni ile ya kupendelea kula sana chakula asilia na hai (natural and fresh), kama vile matunda, mboga, vyakula vitokanavyo na nafaka zisizokobolewa, (mahindi, ngano) au mchele wa rangi ya kijani (brown) na kujiepusha na ulaji mkubwa wa vyakula vya kukaanga na kupikwa na mafuta mengi.

No comments: