Wednesday, March 17, 2010

YAKULA TUNAVYOKULA NA UGALI

Hebu tupeane uzoefu wa vyakula tunavyokula,kwa nini tunaona hivyo ni
vitamu na sababu ya kuendelea kuvitumia.Kwa upande mwengine ni
vyakula gani wanavyotumia wenzetu ambavyo tungependa wawachane navyo
na kujiunga katika mlo wetu au wa wenzetu.
Kwa uzoefu nimegundua ya kuwa kile chakula mtu anachokula wakati wa
utoto wake kuelekea ukubwa katika hali ya raha,yaani katika hali ya
kupata na kuridhika kimazingira alipo ,hicho ndicho chakula
atakachokiona ni kitamu kuliko vyote duniani.Hata ukimpeleka nchi gani
basi bado atakitamani chakula hicho.
Watu huweza kuzoea vyakula kama viwili hivi kimoja zaidi na kingine
chini yake.Wale waliozoea wali na kuku wataendelea hivyo mpaka
uzeeni.Wa ndizi na muhogo nao ni hivyo hivyo,na kadhalika.Wazungu
hakuna chakula bora kama viazi mbatata.Waarabu ni jamii ya mikate na
nyama.
Wengi wetu katika Afrika tunapenda ugali hasa wa mahindi,wengine
huita ugali wa sembe na majina mengineyo.Hata wakiwa maraisi na
mawaziri wakifika ugenini huuweweseka ugali.
TUWACHANE NA CHAKULA CHA UGALI
Mimi ndio wale wa wali kwa kuku kama chakula kikuu cha
siku.Inapokuwa si wakati wa njaa na ukame, huna cha kuniambia mbele ya
chakula hiki.Upishi wake huweza kutofautiana.Kwa bahati niko karibu na
mafundi wa upishi wake.Ningependa watu wote wajizoeshe chakula changu
cha wali,hata ikiwa ni kwa samaki. Ushauri huu,hasa naomba uzingatiwe
na wale wanaopendelea kula ugali
Vyakula vyengine ninavyopendelea kula kwa ajili ya kifungua kinywa
na chai ya usiku, ni jamii ya mikate na mboga mboga za majani
zilizotiwa viungo mbali mbali.Nikijiweza zaidi ni supu ya mbuzi
inayonukia viungo vya kiasili vya kiEshia.
Ufanisi wa sera ya KILIMO KWANZA ni wa mashaka iwapo hatutobadili
vipaumbele vya vyakula tunavyokula.Bahati mbaya sera hiyo katika
nguzo yake ya 4 ya mpango wa utekelezaji, bado inataja mahindi ambayo
hutoa ugali, kama zao la mwanzo katika mazao muhimu ya chakula.
Naomba tuanze kuchangia na utangulizi huu.Nikirudi nitaleta sababu
zangu za kupinga chakula cha ugali kuwa chakula muhimu kwa watu kiasi
cha kuhimizwa katika Kilimo kwanza.Kwa upande mwengine nitataja
vyakula ambavyo mimi sijavizowea lakini ningependa watakaoachana na
ugali wavichaguwe iwapo hawatopendelea wali.

(NA mwana BIDII Uongofu)

No comments: