Dk. Mzige, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya IMTU na Mtaalamu wa Afya ya Jamii , alisema kuwa magonjwa yatokanayo na tabia za binadamu yanaongezeka nchini kwa kasi na inakadiriwa ifikapo mwaka 2020, magonjwa hayo yatachukua zaidi ya ailimia 70 ya magonjwa yote.
Aidha, katika habari hiyo, Dk. Mzige alisema kuwa magonjwa hayo hujulikana pia kama ‘magonjwa ya kusendeka’ (chronic disease) ambayo hutokana na ulaji mwingi wa vyakula vya kusindika (processed food) na kuacha kula vyakula vya asili.
Kwa kawaida, vyakula hivyo vya kusindika, au vya kwenye makopo kama vinavyojulikana, mara nyingi huwa na mafuta mengi, chumvi na sukari nyingi, kemikali nyingi na viungo bandia vingi.
Ulaji wa vyakula hivyo, humuweka mtu katika hatari ya kupatwa na magonjwa sugu kama vile kisukari, shinikizo la damu na saratani. Magonjwa haya hayampati mtu hadi pale anapoanza kuyatengeneza mwenywe kutokana na tabia yake ya ulaji. Leo tulizungumze hili kwa mara nyingine.
Unajitengenezeaje magonjwa?
Nimependa kauli aliyoitumia Dk. Mzige isemayo ‘magonjwa yatokanayo na tabia za binadamu’. Kwa wasioelewa usemi huu ningeomba kuwafafanulia kwani una maana sana. Tabia yako ya ulaji ndiyo inayozungumziwa hapa. Tangu unapoamka asubuhi unafanya nini na unakula nini, una kulaje, unalalaje, ndiko kunakoamua afya yako.
Kumbuka pia ule msemo wetu maarufu usemao, jinsi ulivyo kunatokana na unavyokula. Ukiwa na kitambi au kiribatumbo kunatokana na ulaji wako, ukiwa mnene, mwembamba, kumetokana na ulaji wako, ukiwa na ‘presha’ imetokana na ulaji wako, ukiwa na saratani imetokana na ulaji wako, n.k.
Lakini matatizo yote ya kiafya yanayotukabili, hayaji ghafla, bali huanza taratibu tena kwa kutoa ishara mbalimbali mwilini. Bahati mbaya sana wengi wetu hatuzijui ishara hizo. Hivyo huendelea nazo hadi pale ugonjwa unaporipuka ndiyo tunaanza kuhangaika na tiba.
Mwili wa binadamu hauna tofauti sana na gari. Gari linapokaribia kuishiwa mafuta, huwasha taa nyekundu kuashiria mafuta yamebaki kidogo, ukiendelea na safari kwa muda mrefu bila kuongeza mafuta litazimika na huweza kushangaa kwanini limezimika. Gari likiishiwa maji, mshale wa ‘temperature’ utapanda, ukipuuzia utaunguza injini.
Aidha, gari linapotoa moshi mwingi ni dalili kwamba injini haiko sawa, kuna kifaa kimeisha kinahitaji kubadilishwa, ukiendelea kuliendesha katika hali hiyo, unahatarisha usalama wa vifaa vingine na gari lako kwa ujumla.
Unywaji maji
Mwili wa binadamu nao una kanuni zake, ambazo zikikiukwa, mwili huanza kutuonesha ishara. Kwa mfano, kanuni moja wapo ya mwili inakutaka unywe maji mengi kila siku, kulingana na kazi unayoifanya, kwa siku unatakiwa unywe maji ‘angalau’ glasi sita na kama kazi zako ni nzito, kunywa hata lita 5.
Itaendelea wiki ijayo...
2 comments:
Oh, I real like hii mada, ni kweli tatizo la ulaji vyakula vya kusindikwa umekithiri sana hapa nchini, nimeiona hii hatari tangu ushindani wa kibiashara ulipopanda, utakuta mtu anaacha kununua machungwa akatengeneza juice yake mwenyewe ili awape watoto wake, na badala yake utakuta ananunua juice ya kopo au pakiti ambazo mimi binafsi naziona siyo salama kwa kuwa packing process quality pengine ilikuwa ni ya chini sana, isitoshe hata raw materials zake hatuzijui na nini alichanganya, na ni kiazi gani cha kemikali kimefanikisha utengenezaji wa juice hiyo.
Na si vyakula tu hata vipodozi na dawa za meno hakika zinatoka ktk mazingira yasiyo salama ya utengenezaji,..
Nami nawasihi sana Watanzania wenzangu wapende sana kula vyakula vya asili, i mean vile vinavyotoka ktk mashamba yetu, na hiyo si kwa faida ya afya tu bali hata kipato cha wakulima wetu kitaongezeka na kuweza kulinda thamani ya shilingi ambayo inazidi kushuka kila siku kwa vigezo hivyo vya kuagiza hata vyakula kutoka nje
WATANZANIA WENZANGU, NI KWELI TUNAHATARISHA AFYA ZETU WENYEWE
nakubaliana na wewe! last month nilikwenda kufanya kipimo kimoja kizuri sana, matokeo yake nilipewa ushauri mzuri sana na doctor na unaendana na maneno yako.
Asante sana kaka.
Post a Comment