Friday, October 22, 2010

IJUMAA SHOWBIZ!

Fleva ya showbiz: Wasanii wanajua maana ya umaarufu?
Bado tupo katika safari ya kuzifanya sanaa zetu za Bongo zipenye mbali zaidi a.k.a kimataifa, tunachotafuta hapa ni mchawi anayetufanya tuendelee kubaki tulipo badala ya kwenda mbali zaidi kama walivyo wenzetu wa nchi nyingine za Afrika. Ndiyo maana tukakuomba wewe msomaji na mdau wa burudani utusaidie kutuambia nini hasa kinasababisha kushuka kwa sanaa zetu.

Leo tunaicheki ishu moja ambayo kwa kiasi kikubwa inaunganishwa na sababu nyingine kibao zinazozifanya sanaa zetu zibaki kuishia hapa hapa nyumbani. Kuna mdau mmoja wa safu hii alitutumia meseji akionesha kusikitishwa kwake na baadhi ya wanasanaa wa Bongo ambao wakipata kujulikana kidogo wanajiweka juu zaidi kuliko jamii inavyowatazama, sisi kama Flava ya ShowBiz tukaamua tuishushe kwako wewe msomaji na mpenzi wa burudani ili tuichangie kwa pamoja.

Kuna mwanasaikolojia mmoja aliwahi kusema kwamba umaarufu una nguvu ya ajabu na unaweza ukambadilisha mtu bila yeye kujijua, kitu ambacho nahisi kama kimeanza kuniingia akilini kwa sababu mimi ni mmoja kati ya watu waliopata bahati ya kuishi na baadhi ya watu ambao kabla hawajajulikana walikuwa tofauti na walivyo sasa. Wapo baadhi yao ambao hivi sasa wamekuwa ni walevi kupita kiasi na kusahau majukumu muhimu yaliyowaingiza kwenye sanaa zao.

Hawaishii kwenye ulevi wa pombe tu, kibaya zaidi hutumia hadi dawa za kulevya ambazo mwisho huwafanya waharibu kazi zao, ikiwemo kuwa na jeuri, kutoa maneno ya kashfa kwa jamii iliyowazunguka na kuwafanya wajulikane na inapotokea wakakosa ushirikiano kidogo kutoka kwa jamii hiyo kutokana na tabia zao hushindwa kuendelea na safari ya sanaa kisha hubaki wakijuta na kumuona kila mtu mbaya, wakati wamejiroga wao wenyewe na mwisho sanaa husika inaonekana haina maana tena.

Mbali na kundi hilo wapo baadhi ya wasanii wetu wanapopata kujulikana kidogo tu, inakua ni tiketi ya kuchukulia mademu au wanaume kwa ajili ya kufanya nao ngono tu na kusahau kwamba sanaa ni moja kati ya ajira muhimu ambayo wanatakiwa waiheshimu. Siku moja niliwahi kushikwa sikio na kuambiwa kwamba, kuna msanii mmoja wa kiume (jina ninalo) kila anapokwenda mikoani kufanya shoo baada ya kazi hulala na wasichana wawili au watatu kwa usiku moja, hebu tujiulize hiyo ndiyo maana ya umaarufu?

Kwa mifano hiyo michache inawezekana kabisa wapo baadhi ya wasanii wanaoingia kwenye tasnia hizo wakiwa hawajui wanakwenda kufanya nini au wakiwa na lengo moja tu la kutafuta majina ili wayatumie kufanya uzinzi na uasherati ikiwemo kwa wasanii wa kike kujiuza kwa mapedeshee ambapo mwisho wanawafanya hata wanaopiga kazi ‘siriasi’ waonekane wababaishaji.

Ili tuzipeleke sanaa zetu mbele zaidi umefikia wakati sasa wa kuangalia nani ana nia ya dhati kutuinua na yupi anataka kutupeleka shimoni na tunapombaini tumuondoe kundini kwa kutompa ushirikiano.

Naamini mtu yeyote atakayeingia kwenye sanaa akiamini kwamba ndiyo kazi aliyoichagua kama ajira yake ya kudumu hawezi kutembea bega moja chini lingine juu au kutoa maneno ya kashfa mbele za watu pale anaposikika na wimbo mmoja tu redioni bali atakaa chini na kuumiza kichwa zaidi tena akisikia uchungu kwanini na yeye siku moja asipate mwaliko wa kwenda kufanya shoo Marekani kwa kina 50 Cent kama wao wanavyokuja Bongo. Vivyo hivyo kwa upande wa tasnia ya muvi siamini kama mtu huyo anaweza kujiita yeye ni supastaa kwa kushiriki kwenye filamu moja tu, tena akiwa amechezeshwa kama mhusika wa kazi na siyo ‘stelingi’.

Mwisho namaliza kwa kusema kwamba, wasanii wetu wanatakiwa kufahamu kuwa umaarufu siyo tiketi ya kufanya mambo maovu na kujiona wako juu ya jamii ambayo imewakubali kuwa vioo vyao, wanatakiwa wajione wao ni sawa na watu wengine kwa kushiriki kikamilifu kwenye matatizo ya kijamii pale wanapotakiwa kufanya hivyo ,inawezekana jamii hiyo ikawashauri na kuwapa mawazo mazuri yatakayowafanya wafike mbali zaidi badala ya kujiona wao ndiyo wao wakati hata ukienda kijijini kwetu ‘Nsemulwa’ hawajulikani. Tubadilike.
********************************
Ali Kiba Kusepa Marekani leo, kupiga kolabo na R.Kelly
Kutoka ndani ya mradi wa muziki wa kizazi kipya, msanii Ali Kiba anatarajia kuondoka leo kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya kugonga ngoma ya pamoja na baadhi ya mastaa wa Afrika, kabla ya kufanya kolabo na staa wa kimataifa, Robert Kelly wa pande hizo.

Kwa mujibu wa msemaji wa ishu hiyo, Christine Mosha ‘Seven’, Ali Kiba ataungana na mastaa wengine kutoka Afrika wakiwemo Navio (Uganda), Amani (Kenya), 2Face (Nigeria), Fally Ipupa (Congo), JK (Zambia), 4x4 (Ghana) na wengine waliopata nafasi hiyo kupitia utafiti uliofanywa na Kituo cha Televisheni cha MTV Base wa kutafuta wasanii wakali kwa nchi za Afrika.

Kabla ya safari hiyo, mwanzoni mwa wiki hii, Kiba anayeendelea kufanya vizuri na video ya wimbo wake wa Hadithi iliyoandaliwa na Mtayarishaji, Malcom akiwa katika mchakato huo wa kusepa kwa Obama alijikuta akidondokea kwenye vikwazo pale aliposhindwa kupata Viza ndani ya Ubalozi wa Marekani.

Staa huyo wa ngoma ya Usiniseme alifika katika Ubalozi huo uliopo pande za Drive In, Dar Jumatatu asubuhi kwa ajili ya kushughulikia ishu hiyo lakini aliambiwa na mmoja wa maafisa wa ubalozi huo kuwa hawezi kupata Viza kwa sababu pasipoti yake ilikuwa inakaribia kwisha muda na kwamba alitakiwa ‘kuirinyuu’ kitu ambacho alikitekeleza na kufanikiwa kuendelea na safari yake leo. ShowBiz inamtakia Kiba Kolabo njema na aiwakilishe vyema Bongo huko ughaibuni.
**************************************
Angelina Jolie Amaliza bifu na Serikali ya Bosnia
Nyota wa filamu nchini Marekani mwanadada Angelina Jolie ameshinda mzozo ulioibuka wiki iliyopita kati yake na serikali ya Bosnia iliyokuwa imempiga stop kufanya kazi ya kurekodi muvi yake mpya katika ardhi ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa habari kutoka Zimbio.Com, Jolie ameshinda vita hiyo baada ya kupata mbeleko ya mashirika mbalimabli ya kimataifa yanayojishughulisha na haki za wanawake yaliyoibuka na kupinga hatua ya serikali hiyo kumzuia mwigizaji huyo kufanya kazi yake ya kurekodi filamu kwenye Jiji la Sarajevo.

Muda mfupi baada ya kuondolewa kwa pingamizi, mtayarishaji mahiri wa filamu huko Marekani, Edin Sarkic alisema; “Ni furaha kubwa kwa Jolie na watu wake kukubaliwa kuendelea na kazi yao, hii ina maana kuwa sasa Bosnia itatapata mapato kutokana na upigwaji picha huo ndani ya ardhi yake.
*********************************
Huyu ndiye ‘mchawi’ wa Inspector Haroun
Waswahili husema, jambo usilolijua ni kama usiku wa giza. Kumbe wakati staa wa Muziki wa Kizazi Kipya, Haruna Kahena ‘Inspector Haroun’ anafanya maajabu na ngoma yenye jina la ‘Mtoto wa geti kali’ nyuma ya pazia alikuwepo mtu aliyefanikisha zoezi hilo.

Namzungumzia msanii Cool Boy ambaye alizaliwa kwa jina la Amily Ally anayesikika hivi sasa na ngoma yenye jina la Ajira. Jamaa alisema na ShowBiz kwamba, kuchelewa kwake kutoka ilikuwa neema kwa wengine kama Inspector ambaye alimuandikia ngoma hiyo ya Mtoto wa geti kali.

“Unajua wengi hawafahamu kama mimi ndiye niliandika ngoma ya Mtoto wa geti kali nikampa Inspector na siku zote huwa naamini hawezi kutoka tena mpaka nimuandikie,” alisema Cool Boy kwa kujiamini. Kauli hiyo ya mchizi tunaitupia hapa na kugeukia upande wa Inspector ambaye wakati tunaelekea mitamboni simu yake haikuweza kupatikana mara moja, tutaendele kumtafuta ili athibitishe hilo.
********************************

Z-ANTO: Mtoto wa kike aliniharibia malengo yangu
Hatimaye kijana aliyefanya vizuri na ngoma kadhaa miaka michache iliyopita, Ally Mohamed Ahmad a.k.a Z-Anto amefunguka na kupiga stori mbili tatu na ShowBiz zikiwemo ishu zinazohusu maisha yake ya ndani.

Akisema na safu hii kwa njia ya simu kutoka pande za Kigamboni, msanii huyo ambaye hivi sasa amerudi upya na ngoma yenye jina la Kisima cha malavidavi alitamka kwamba mipango mingi aliyokuwa nayo katika maisha yake ilivurugwa na msichana ambaye yeye humuita mtoto wa kike bila kumtaja jina lake.

“Kwa mfano hivi sasa baada ya kuwa peke yangu nimefanikiwa kufungua saluni huku kwetu Kigamboni iitwayo ‘Kwetu salon’ mipango ambayo nilikuwa nayo kitambo ila mtoto wa kike niliyekuwa naye akanivurugia malengo. Kwa sasa nina kila sababu ya kusema asante Mola kwani jina langu linarudi na biashara zangu zinakwenda kama nilivyotarajia, ‘i am back’,” alisema Z-Anto.
**********************************
DESTINY OF A MAN: kuleta changamoto Bongo muvi leo
Filamu ya kimataifa ya Destiny of man chini ya muongozaji na mcheza filamu mahiri kutoka Urusi, Sergei Bondarchuk inatarajiwa kuleta changamoto kubwa kwa wasanii wa Bongo jioni ya leo itakapooneshwa ndani ya Ukumbi wa filamu wa New World Cinema, Mwenge katika tamasha la filamu kutoka Ulaya (European Film Festival, EFF) ambapo kama kawa kiingilio ni bure.

Stori ya muvi hiyo ambayo inatoka katika kitabu cha mwandishi bora wa riwaya duniani, Mikhail Sholokov ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Nobel inamhusu mwanajeshi wa Kirusi, Andrei Sokolov ambaye anashuhudia mke na watoto wake wakiuawa kikatili na majeshi ya Ujerumani na baadaye na yeye ananusurika kufa baada ya kupewa mateso makali kwenye kambi ya mateso ya Ujerumani.

Msamaha maalum kutoka kwa kamanda wa Kijerumani Muller unamrudisha tena kwenye mapambano lakini mikosi bado inaendelea kumuandama pale anapopokea taarifa kuwa mwanae mwingine wa kiume ameuawa. Filamu hiyo ambayo imeshanyakua tuzo kama Grand Prize ya Moscow, Special Karlovy Vary Award na nyingine kibao inamalizika kwa Solokov kuamua kuwasamehe wote waliofanya ukatili dhidi ya familia yake.

Baada ya vita kwisha anabadilika na kuwa mtu mwema kwenye jamii na anajitolea kumlea mtoto yatima.

“Wote wanaotaka kuona viwango vya juu na changamoto katika filamu wafike New World Cinema kujionea wenyewe ambapo kiingilio ni bure,” alisema Tayana Tibenda, msemaji wa tamasha hilo.

imeandaliwa na mc
george/Ijumaa

No comments: