Saturday, June 2, 2007

MAAJABU YA MAJI


Nimefurahi kuona ni kiasi gani watu wamefuatilia mada hii na kugundua siri hii ya siku nyingi katika ulimwengu wa afya bora. Nawashukuru wale wote walionipigia simu na kutaka ufafanuzi na wale walionitumia ujumbe mfupi wa maneno kwa njia ya simu, mnisamehe wale ambao sikuweza kuwajibu, kwani meseji zilikuwa nyingi sana!

Wiki iliyopiata tulisema kwamba ili upate faida ya maji kama tiba, ni lazima unywe maji mengi asubuhi kabla ya kuchomoza kwa jua na kabla hujapiga mswaki wala kula kitu chochote. Ujazo unaotakiwa kunywa ni kuanzia lita 1 na robo mpaka lita 1 na nusu, maji safi na salama na yasiwe ya baridi.

Adidha, tulisema kuwa ukisha kunywa maji hayo usile wala usinywe kitu kingine hadi baada ya dakika 45 au saa moja, baada ya kupita muda huo, unaruhusiwa kupiga mswaki na kunywa au kula chochote utakacho na kinachokubalika kiafya (rejea makala zetu zilizopita).

Kitu kingine cha kuzingatia ni kwamba baada ya kunywa hayo maji, ni lazima uyanywe ndani ya kipindi cha dakika 5 au 10 tu na usifanye mazoezi hadi baada ya nusu saa. Wakati unafuata tiba hii kwa siku nzima, basi sharti liwe ukisha kula chakula, unywe maji kila baada ya saa 2 na ukae muda huo kabla hujala kitu kingine.

Hata mtu asiye na maradhi yoyote, anashauriwa kunywa maji kwa mtindo huu ili kujikinga na maradhi katika maisha yake yote. Kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kunywa kiasi hicho kwa siku zao za mwanzo, wanashauriwa kuanza na kiasi kidogo cha angalau glasi 2 na hatimaye wafikie 4. Usiogope wala usifikirie kutapika wakati ukinywa maji hayo, maji hayatapishi, bali dhana yako ndiyo inayoweza kukufaya utapike!

Orodha ya magonjwa yanayoaminika kutibika, kuzuilika au kudhibitiwa kwa tiba hii ya maji ni pamoja na: Kisukari, shinikizo la damu, maumivu kwenye viungo (Joints Pain), matatizo ya moyo na kuzimia, homa ya uti wa mgongo (Meningitis), matatizo ya mkojo, kansa ya kizazi (Uterus Cancer), kikundu (hemorrhoid), matatizo ya tumbo, kuharisha, nyongo, kikohozi na chunusi.

Magonjwa mengine ni pamoja na kupooza mwili, athma, asidi tumboni, homa, kuumwa kichwa, upungufu wa damu (anemia), utipwatipwa (Obesity), kifua kikuu, magonjwa ya ini, matatizo ya hedhi, mataizo ya kukosa choo na magonjwa mengine mengi!

Iwapo watu wangeachana na unywaji wa pombe na soda, badala yake wakawa wanakunywa maji safi na salama kwa wingi, watafiti wa tiba ya maji wanaamini kwamba idadi ya wagonjwa hospitalini ingepungua kwa kiasi kikubwa sana duniani.


TIBA HII YA MAJI INAFANYA VIPI KAZI MWILINI?

MOSI: Unapokunywa lita moja na robo ya maji ndani ya dakika 5 au 10, baada ya kufunga kwa usiku mzima kwa muda usiopungua saa 8 hadi 10, shinikizo la maji yanayopita kwenye utumbo mdogo, huamsha seli (cells) kwa haraka kuliko kawaida.

PILI: Kutokana na shinikizo hilo la maji la ghafla, masalia na vipande vipande vya vyakula ambavyo huganda kwenye kuta za utumbo mdogo, husombwa na maji hayo pamoja na gesi na vitu vingine ambavyo havikusagwa na kutupwa kwenye utumbo mpana tayari kutolewa kama uchafu. Hali hii huuacha utumbo mdogo ukiwa safi na kuzipa seli uhai mpya!

TATU: Utumbo sio sehemu pekee inayonufaika na tiba hii ya maji, bali chembechembe hai (cells) zote za mwili huwa zimepewa uhai na nguvu mpya. Maji yanaponywewa baada ya mwili kutoingiza kitu chochote kwa kipindi cha saa 8 – 10, mwili huyapokea maji hayo kwa ‘kiu’ kubwa na kuyasambaza katika seli zote za mwili.

Vijidudu nyemelezi (free radicals) na vitu vyote vyenye sumu ambavyo huganda kwenye seli, kimsingi hushinikizwa kujiondoa vyenyewe kutoka kwenye seli hizo, hivyo kuurahisishia mfumo wa kusafisha mwili kuondoa mwilini sumu na vitu visivyotakiwa kwa urahisi.

TAHADHARI:
Kwa mgonjwa anayetumia tiba hii ya maji, kuna mabadiliko au usumbufu fulani anaoweza kuupata katika siku 3 au 7 za mwanzo. Anaweza kuumwa na kichwa au mwili na kuhisi kama kichwa chake ‘kinaogolea’. Vile vile anaweza kutokwa sana jasho, kusikia kichefuchefu au kama si hivyo, anaweza asijisikie vizuri tu.

Hayo yasikutie hofu, hayo SIYO MADHARA (side effects), bali hiyo ni dalili kwamba mwili umeanza kuondoa sumu zilizoganda kwenye seli zake. Kwa kuwa tiba ya maji haina madhara yoyote, unapoona dalili hiyo usiache, endelea kama kawaida, kama utashindwa basi punguza kidogo kiasi cha maji unachokunywa.

Baada ya siku kadhaa kupita, mgonjwa hurejea katika hali yake ya kawaida na hiyo huwa ni dalili kwamba mwili umeanza kutakasika. Hali ikirejea kama kawaida, mgonjwa hana budi kuendelea na kiasi kile kile cha maji kilichopendekezwa.

ZINGATIA
Ingawa tiba ya maji ni nzuri kwa wagonjwa wengi wa figo na moyo, lakini wenye matatizo MAKUBWA ya magonjwa hayo, wanashauriwa kujaribu tiba hii baada tu ya kupata mwongozo sahihi na ruhusa ya daktari.

Miongoni mwa watu ambao wamekiri kwa asilimia 100 kwamba nilichokiandika kuhusu tiba ya maji ni kweli, ni pamoja na msomaji wetu aliyenipigia simu kutoka Musoma aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Michael, ambaye alikuwa na tatizo la figo na hakuwahi kupata tiba mapema hositalini, lakini baada ya kupata habari za tiba ya maji na kutumia, tatizo liliondoka na sasa yu mzima wa afya.

Aidha Bw. Michael aliendelea kusema kwamba maji anayeheshimu sana na ameyafanya kuwa ndiyo tiba yake ya kwanza na ya msingi kila anapopatwa na tatizo la kiafya. Akasema kuwa alikuwa pia anakabiliwa na tatizo la kupoteza fahamu (kuzima), tatizo ambalo limekwisha kwa kutumia tiba ya maji, ambayo alielezwa hata kabla hajasoma kwenye gazeti hili, hivyo nawe anza kuchukua hatua sasa ya kujikomboa na adui maradhi.

2 comments:

Anonymous said...

Nashukuru kwa kutuekea blog kuhusu afya zetu hongera kwa kuanzisha kitu tofauti,mimi nina swali kuhusu matibabu ya maji,kuna siku nilikuwa nasikiliza Radiao One kipindi fulani mama Teri alisema matibabu ya maji siyo mazuri!!!kwani kunywa maji mengi kwa kipindi kifupi binaadamu unapoteza Culcium nyingi mwilini kwa njia ya mkojo kuanzia hapo mimi nikaacha na nikawa siamini matibabu haya.Je haya ni kweli naomba jibu pls.

Twaha Shekhe said...

Je nikinywa maji saa 10:30 alfajiri nitapata tatizo