Saturday, June 2, 2007

Mlo sahihi kwa wagonjwa wa kisukari


Kama ilivyo ada, leo tunakutana tena kuzungumzia jinsi ya kudhibiti tatizo lingine la kiafya kwa kutumia chakula, baada ya wiki iliyopita kuuzungumzia ugonjwa hatari wa ‘presha’, ambao unajulikana pia kama ‘muuaji wa kimya kimya’ (silinet Killer).

Leo tutazungumzia ugonjwa wa kisukari (Diabetes) ambao umeshajipatia umaarufu duniani na umekuwa kama fasheni, kwani idadi ya walionao inaongezeka kila mwaka, iwapo hatutabadili staili zetu za maisha bila shaka wengi tutapoteza maisha kwa tatizo hilo.

Kama ilivyo kwa maradhi mengine yanayomkabili binadamu katika karne hii, staili ya maisha ndiyo chanzo kikubwa. Ugonjwa wa kisukari hutokea pale mwili wa binadamu unaposhindwa kufanya kazi yake vizuri ya kujiendesha na kurekebisha mfumo mzima wa kupanda na kushuka kwa sukari kwenye damu.

Wataalamu wetu wanauelezea ugonjwa wa kisukari kuwa unatokana na kuvurugika kwa mfumo wa uvunjaji wa kemikali mwilini (metabolic disorder) ambao husababisha mwili kushindwa kutumia glukozi (sukari) kikamilifu, hivyo kusababisha mkusanyiko mkubwa wa sukari kwenye damu.

Hali hiyo hutokea baada ya kiungo kiitwacho Kongosho (pancreas) kushindwa kutoa homoni aina ya Insulin ambayo ndiyo hudhibiti kiwango cha sukari kinachotakiwa kubaki kwenye damu.

Kuielezea hali hiyo katika lugha nyepesi inayoeleweka kirahisi, tunaweza kusema kwamba hali hiyo ya kuvurugika kwa mfumo mzima wa kudhibiti sukari mwilini hutokea baada ya mwili kukosa chakula chenye kirutubisho muhimu katika kuliwezesha kongosho kufanya kazi yake ipasavyo, kwa maana hiyo ulaji wako wa chakula hauko sahihi ndiyo maana hali hiyo imetokea.

Kwa mujibu wa wataalamu wetu, kuna aina mbili za ugonjwa wa kisukari, ambazo ni Type1 na Type2. Type 1 huwapata zaidi watoto au vijana wadogo na hutibika zaidi kwa kutumia dawa (Insulin). Lakini aina ya pili ya kisukari (Type2) ambayo huwapata zaidi vijana kuanzia umri wa miaka 40, watu wanene na wazee, huweza kudhibitiwa kwa kufanya mazoezi na kula mlo uliokamili (balanced diet).

MLO WA WAGONJWA WA KISUKARI

Kwa kuwa ugonjwa huu unatokana na upungufu wa virutubisho fulani mwilini, kuna miongozo imetolewa ya ulaji vyakula ambavyo vikifuatwa kwa ukamilifu huweza kudhibiti ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa na hata kuufanya usiwe tishio kwa maisha yako.

Kitu cha msingi ni mtu kujitambua mapema kama una ugonjwa wa kisukari na kisha kuchukua hatua haraka ya kuudhibiti kwa chakula. Kutegemeana na hatua iliyofikia ugonjwa wako, kisukari kinaweza kudhibitiwa ama kwa mlo peke yake au mlo na dawa.

Mtu mwenye kisukari ambacho hakijakomaa sana, anaweza kukidhibiti kwa mlo tu bila kutumia dawa yoyote na akaweza kuishi bila matatizo. Lakini kisukari kilichokomaa kinahitaji mlo pamoja na dawa na ili muathirika ajiepushe na madhara makubwa ya ugonjwa huo yanayoweza kumpata, ni lazima ahakikishe anafuata masharti ya vyakula.

Hii ina maana kwamba kama kisukari chako hakijakomaa na kuwa tishio kwa afya yako, hali hiyo inaweza kubadilika na kuwa kisukari kilichokomaa iwapo hutazingati ya ulaji wa mlo sahihi, hivyo hivyo kwa mgonjwa mwenye kisukari kilichokomaa anaweza kupoteza maisha haraka zaidi iwapo hatazingatia masharti ya vyakula, na dawa anazotumia, haziwezi kumsaidia chochote.

Mtu mwenye ugonjwa wa kisukari anatakiwa kupunguza ulaji wa vyakula vyenye wanga (Carbohydrates), kama vile viazi, mihogo, mikate myeupe (White Bread), n.k. apunguze ulaji wa vyakula vya mafuta na kula vyakula vya protein kwa kiasi kidogo.

Badala yake mgonjwa huyu anapaswa kutumia kwa wingi vyakula vyenye kiasi kikubwa cha kirutubisho kiitwacho ufumwele (fibre) ambacho hupatikana kwenye vyakula kama vile matunda, nafaka zisizokobolewa (ugali wa dona, ugali wa mtama, mikate myeusi, n.k) na aachane kabisa na kula vyakula vilivyosafishwa (refined foods) na kuondolewa virutubisho vyake (mikate myeupe, ugali mweupe, n.k).

Aidha, saladi (mchanganyiko wa wa mboga mbichi) inaweza kuliwa kwa kiwango chochote, lakini tahadhari ichukuliwe kwa saladi zilizowekewa mafuta mengi. Kwa kuwa matunda mengi yana kiasi fulani cha sukari, mgonjwa atapaswa kula matunda baada ya kupewa ushauri na daktari atakayejua kiasi cha sukari alichonacho. Juisi za matunda nazo ziepukwe na pale zinapotumiwa, ziandaliwe na maganda yake, kama vile apple na peasi.

Matunda yanapoliwa, hii ni kwa watu wote, hayapaswi kuliwa pamoja na chakula kwa wakati mmoja. Matunda huliwa saa 2 kabla ya au baada ya mlo ili kupata faida haswa za matunda. Watu wengi wanafanya makosa kula matunda, kama vile embe, papai wakati wa kula chakula cha mchana au jioni. Ulaji wa aina hii haufai na hauweze kuupa mwili wako faida za matunda.

Kwa ujumla mgonjwa wa kisukari, anapaswa kuogoba sana vyakula vyenye mafuta, hasa katika vyakula ambavyo mafuta yake hayaonekani moja kwa moja, kama vile maziwa (Full Cream Milk), kiini cha yai (Egg Yolk) na nyama nyekundu (Red Meats).

Unapokunywa maziwa, basi chagua maziwa yasiyokuwa na mafuta (Fat Free Milk au Skimed Milk), kama ni maziwa ya kuchemsha na kupoa, engua malai yake na yatupe, unapokula nyama ya kuku, usile na ngozi yake na tumia mafuta kiasi kidogo sana cha mafuta ya kupikia au siagi katika milo yako ya kila siku. Hata wewe ambaye huna kisukari, huu ndiyo ulaji unaotakiwa kuufuata.

Ushauri mwingine unaotolewa kwa wagonjwa wa kisukari ni ufanyaji wa mazoezi mara kwa mara, ambayo huufanya mwili kuwa fiti na kuudhibiti ugonjwa huo. Mazoezi mepesi kama vile kukimbia taratibu (jogging), kuogelea na kutembea kwa mwendo wa haraka ni njia moja wapo ya kuuweka mwili wako imara dhidi ya kisukari.

Wagonjwa wa kisukari wanashauriwa kula milo yote, hasa baada ya kutumia dawa (insulin), kutokubadili dawa bila ushauri wa daktari na kuhakikisha wanapima mkojo mara kwa mara. Wanashauriwa kutembea wakiwa wamejikinga ili wasiumie na kupata vidonda.

Likiwa lengo la kufuata lishe bora ni kuepuka kupanda na kushuka kwa sukari kwenye damu ili mtu uwe na afya imara, basi ni vizuri sana wewe uliyeathirika na kisukari kuzingatia haya yafuatayo:

1) Muda wa kula ni muhimu sana kwako. Kula mlo na vitafunwa vingine (snacks) muda ule ule kila siku kadri iwezekanvyo. Kula kitafunwa chochote wakati ufanyapo mazoezi au pale kiwango cha sukari kinaposhuka sana. Lakini hali ya kushuka sana kwa sukari inapokutokea mara kwa mara, wasiliana na daktari wako haraka.
2) Iwapo unatumia dawa, basi hakikisha kila wakati unapotaka kulala, unakula kitafunwa chochote. Kula mlo wako kwa kiwango kile kile bila kuzidisha, kwani kula kupita kiasi kunaweza kupandisha kiwango chako cha sukari.

Kwa ujumla, kila mgonjwa anapaswa kujua ni chakula gani akila kinaweza kumpa nafuu na kipi akikila kinaweza kumuongezea matatizo aliyonayo, kwa kujua hilo kuna mchoro (Food Pyramid), umeandaliwa maalumu kwa wagonjwa wa kisukari ambao unaonesha chakula kipi kinafaa kuliwa kwa wingi na kipi kiliwe kwa uchache sana. Usome kwa makini mchoro huo juu ili uelewe chakula kipi ukipende sana na kipi ukipene kidogo sana.

5 comments:

Anonymous said...

endelea kutupa elimu juu ya AFYA ZETU

Anonymous said...

Nimefurahia sana makala yako kuhusu mlo kwa wagonjwa wa kisukari umefanya utafiti mzuri sana hongera sana please keep it up

jovinarchard said...

Ongera sana kwa kutoamada nzito ya magonjwa na tiba ya matunda.

Jovin

Unknown said...

Je nawezaje kupata kitabu chenye muongozo kamili WA

Unknown said...

Mimi ninatatizo la figo na pia nasukari na presha ya kushuka na tatizo la moyo je ulaji wangu uweje???