Sunday, June 3, 2007

PAPAI ‘TUNDA LA MALAIKA:’ KINGA TOSHA DHIDI YA MSHITUKO WA MOYO, KIHARUSI, SARATANI YA UTUMBO NA KUVIMBA MAPAFU!Kama kuna tunda maarufu duniani na linalopendwa na watu wengi, basi bila shaka papai ni moja wapo. Licha ya kuwa ni tunda zuri lenye ladha tamu, lakini faida zake mwilini nazo ni kubwa na nyingi. Faida zake hazipo kwenye tunda pekee, bali hadi kwenye mbegu zake.

Inaelezwa kwamba, kutokana na uzuri wa tunda hili, mtafiti maarufu anayeaminika kulivumbua bara la Amerika, Christopher Columbus, alilipachika papai jina la ‘Tunda la Malaika’.

Mbegu za papai huliwa pia, ingawa zina ladha chungu, lakini hazina madhara bali zina faida kiafya. Tunda lenyewe na sehemu zake nyingine, zina aina pekee ya kimeng’enyo (enzymes) kiitwacho Papain, ambacho ni muhimu katika kusaidia usagaji wa protini mwilini.

Kimeng’enyo hicho hupatikana kwa wingi pale papai linapokuwa bado bichi. Kwa kawaida mapapai mabichi lakini yaliyokwisha komaa vizuri, ndiyo hutumika kupata virutubisho hivyo ambavyo hutengenezwa vidonge vya lishe (Food Suplements) na sehemu nyingine ya papai hutumika katika utengenezaji wa gamu za kutafuna (Chewing gum).

FAIDA KUBWA KIAFYA ZA PAPAI

Siyo tu kwamba papai lina ladha tamu na lina rangi nzuri ya kuvutia, lakini pia ndiyo chanzo kikuu cha virutubisho vinavyotoa kinga kubwa ya mwili (antioxidants) kama vile Carotenes, Vitamini C, Flavonoids na jamii zote za Vitamin B. Mbali ya kuwa na Vitamini, papai pia lina madini ya Potassium, Magnesium na Fiber.

Elewa kwamba virutubisho vyote hivyo vina kazi kubwa mwilini ya kuimarisha utendaji kazi mzuri wa mfumo mzima wa moyo (cardiovascular system) na kutoa kinga kubwa dhidi ya ugonjwa wa saratani ya utumbo (colon cancer). Hivyo ulaji wa tunda hili, ni tiketi ya uhakika ya kwenda mbali na matatizo ya moyo na saratani ya utumbo.

Zaidi ya hayo, papai hilo hilo lina vimeng’enyo muhimu (papain) vinavyosaidia sana usagaji na ulainishaji wa chakula tumboni. Vimeng’enyo hivyo pia hutumika kama dawa mwilini ya kutibu majereha kwenye utumbo na matatizo mengine ya mzio (allergies).

KINGA KUBWA YA MGONJWA YA MOYO

Vile vile papai linaweza kuwa na msaada mkubwa katika kuzuia magonjwa ya moyo na kisukari kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha vitamini C, E na A, vitamani ambazo zina nguvu na ni muhimu sana katika kutoa kinga dhidi ya magonjwa hayo.

Vitamini hizo ndizo zinazozuia ile hali ya kuganda mwilini kwa mafuta aina ya Cholestrol (Oxidation of Cholestrol). kwa mujibu wa wana sayansi wetu, ni pale tu cholestrol inapoganda, ndipo inapokuwa na uwezo wa kukwama na kujikusanya kwenye kuta za mishipa ya damu na kuanza kutengeneza uzio hatari ambao mwisho wa siku, ndio unaosababisha mshituko wa moyo au kiharusi.

Njia pekee ya kupamba na hali hiyo isitokee mwilini mwako ni kula kwa wingi matunda, kama papai, yenye kiwango kikubwa cha vitamin E na C za kutosha ambazo tunaelezwa ndizo zinazotoa mchango mkubwa wa kudhibiti kuganda kwa yale mafuta mabaya na mazuri ya Cholestrol (LDL & HDL Cholestrol).


Kama tulivyoona hapo juu, papai pia lina kirutubisho kingine muhimu aina ya Fiber (ufumwele) ambacho kimeonesha uwezo mkubwa wa kushusha kiwango cha Cholestrol mwilini. Wengi mnafahamu kwamba watu wenye kiwango kikubwa cha mafuta ya Cholestrol mwilini ndio wenye hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo au kiharusi, hali ambayo hutokana na kuwa na staili ya msiaha isiyo tilia maanani ulaji wa matunda na mboga mboga.

HUSAIDIA USAGAJI WA CHAKULA

Umuhimu wa kirutubisho aina ya Fiber, kilichomo kwenye papai, ni mkubwa sana. Miongoni mwa faida za kirutubisho hiki ni pamoja na kusaidia usagaji wa chakula tumboni hivyo kumuwezesha mtu kupata choo laini, na katika hilo kirutusho hiki kimeonesha uwezo wa kutoa kinga dhidi ya saratani ya utumbo ambayo huwa na uhusiano mkubwa wa mtu kukosa choo kwa muda mrefu au kupata kwa taabu kwa kipindi kirefu.

Virutubisho vyote vilivyomo kwenye papai hutoa kinga ya pamoja kwenye chembe hai za utumbo dhidi ya vijidudu nyemelezi. Hivyo kwa kuongeza ulaji wa tunda hili tamu, unakuwa unajipa kinga madhubuti dhidi ya magonjwa tuliyoyataja hapo juu.

HUTOA AHUENI KWA MAGONJWA YA MWASHO

Papai pia lina aina ya kipekee ya vimeng’enyo vya Protini vikiwemo vile maarufu vya Papain na Chymopapain. Vimeng’enyo hivi vimeonesha uwezo mkubwa wa kutoa ahueni katika magonjwa ya muwasho na kusaidia kuponyesha haraka majeraha ya moto.

Mbali ya hayo, virutubisho vinavyotoa kinga dhidi ya maradhi mwilini vilivyomo kwenye papai, vikiwemo Vitamin C, E na Beta-catene, husaidia sana kuwapa nafuu watu wenye magojwa ya muwasho kama vile pumu, vidonda vya koo, na kadhalika. Imethibitika kwamba wagonjwa hawa wanapopata virutubisho hivyo, haswa kwa njia ya vidonge, hupata nafuu ya haraka.

PAPAI HUTOA KINGA YA MWILI

Vitamini C na A pamoja na Beta-carotene, ambavyo vyote vinapatikana ndani ya papai, vinahitajika sana katika kuifanya kinga ya mwili ifanye kazi yake ipasavyo ya kukukinga na maradhi mbalimbali. Hivyo basi papai linaweza kuwa chaguo zuri sana la kukupa kinga dhidi ya maradhi madogo madogo, lakini yanayo sumbua mara kwa mara, kama vile mafua, kukohoa na maambukizi mengine.

KINGA DHIDI YA MARADHI YA VIUNGO

Katika utafiti mmoja uliofanywa kuhusu matatizo ya viungo, iligundulika kwamba vyakula vyenye kiwangao kikubwa cha Vitamin C, kama vile papai, hutoa kinga dhidi ya maradhi ya viungo, hasa magoti na sehemu nyingine za maungio. Hivyo kwa kula papai na kupata vitamini C, unaupa mwili wako kinga dhidi ya maradhi hayo, ambayo mara nyingi huambatana na umri mkubwa.

Katika utafiti wao juu ya suala hili la matatizo ya ugonjwa wa viungo (Rheumatic Diseases), ambao ulijumuisha zaidi ya watu 20,000, wanasayansi waligundua kuwa watu waliokuwa wakila kiasi kidogo sana cha vyakula vyenye vitamini C, walikuwa katika uwezekano wa kupatwa na ugonjwa wa viungo mara tatu zaidi ya wale waliokuwa wakila vyakula vyenye vitamini C kwa wingi. Hivyo utaona papai ni muhimu kiasi gani kwa afya yako.

HUBORESHA AFYA YA MAPAFU

Faida za papai zingali zikiendelea, na faida hii inawahusu sana wavutaji sigara au watu ambao hujikuta katika mazingira yenye moshi wa sigara, kama vile ndani ya kumbi za starehe.

Utafiti uliofanywa na chuo kikuu kimoja nchini Marekani unasema kwamba, iwapo utakula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha Vitamin A, kama papai, basi unaweza kuokoa maisha yako kwa kuimarisha afya ya mapafu yako kutokana na kuathiriwa na moshi wa sigara.

Wakati akitafiti uhusiano uliopo kati ya Vitamin A na ugonjwa wa mapafu, Richard Baybutt, ambaye ni profesa wa masuala ya lishe katika jimbo la Kansas nchini Marekani, aligundua kwamba siyo tu vitamin A huimarisha afya ya mapafu, bali pia huzuia athari zinazosababishwa na sumu aina ya Benzo(a)pyrene iliyomo kwenye moshi wa sigara ambayo husababisha ugonjwa wa kuvimba mapafu (Emphysema).

KWA NINI WAVUTA SIGARA WENGINE HAWANA MATATIZO YA MAPAFU NA WANA UMRI WA MIAKA 90?

Aidha profesa huyo anaamini kwamba uwezo wa kinga ilionao vitamin A, unaweza kusaidia kuelezea kwa nini baadhi ya wavuta sigara hawapatwi na ugonjwa wa mapafu.

“Kuna baadhi ya wavuta sigara ambao wanaishi hadi miaka 90 na ni wavutaji wazuri wa sigara, kwa nini? Bila shaka ni kutokana na lishe yao,” ansema prosesa na kuongeza kuelezea kwamba;

“kwa wale watu wanaoanza kuvuta sigara wangali wadogo, wana uwezekano mkubwa wa kupatwa na upungufu wa vitamin A na hivyo kupatwa na madhara yanayohusiana na kansa na ugonjwa wa kuvimba mapafu, na wakiwa na lishe duni ndiyo wasahau kabisa,” anasisitiza profesa huyo.

Ushauri anaoutoa profesa Richard ni kwamba iwapo wewe au mtu unayempenda anavuta sigara, au kazi na mazingira yako yanakufanya uvute moshi wa sigara bila wewe kupenda, jilinde dhidi ya maradhi ya kansa na kuvimba mapafu kwa kuhakikisha vyakula vyenye kiwangao kikubwa cha vitamini A, kama vile papai, vinakuwa sehemu ya chakula chako cha kila siku.

VIFUATAVYO NDIYO VIWANGO VYA VIRUTUBISHO VILIVYOMO KWENYE PAPAI

Vitamin C: 313.1mg
Folate (Vitamin B’s): 115.52 mcg
Potassium: 781.28 mg
Dietary fiber: 5.47 g
Vitamin A: 863.36 IU
Vitamin E: 3.40 mg
Vitamin K: 7.90 mcg

4 comments:

SIMON KITURURU said...

Mzee blogu yako bomba sana!

Miriam said...

Mrisho
Karibu sana sana, Nakuomba usiishie na matunda tuu, mboga pia na vyakula vingine. Mimi nitakuwa mgeni wako maarufu.

Anonymous said...

Nalipenda papai lakini nalila nikija huko home huku tuliko bei ya papai km unanunua gari!!!,mimi hupenda kulichanganya na matango,ndizi mbivu,chungwa na ndimu hulivuruga kwenye bakuli nikala km mlo kamili,je kwa kula hivi napata virutubisha au nauwa virutubisho?

Rodrick Alexander said...

hizo mbegu za malaika nitapata wapi maana nimetafuta kariakoo wamesema zimeisha na zinatengenezwa na kampuni toka Uganda.
Nimesikia pia SUA wanazalisha ila sijapata mawasiliano