Monday, June 18, 2007

UNAVIJUA VYAKULA HAI NA VISIVYO HAI?



Kuna mjadala mkali unaoendelea katika ulimwengu wa masuala ya vyakula na maisha ya binadamu. Katika mjadala huo kuna suala la vyakula hai na visivyo hai (Live and dead foods).

Wapo wanaosema vyakula vya kupika (visivyo hai) ndivyo vinavyochangia kwa kiasi fulani binadamu kupatwa na magonjwa mbalimbali, hivyo wanahimiza watu wapende kula vyakula hai, kama vile matunda, mboga na kadhalika, hebu tuangalie hoja zinazotolewa kuhusu dhana hii;

Inaelezwa kwamba kuna aina ya viumbe hai vipatavyo milioni 80 ardhini (kati ya hivyo karibu 700,000 ni wanyama) ambao wanaishi kwa kula vyakula visivyopikwa (raw food).

Aidha, ni binadamu pekee ndiye anayepika vyakula anavyokula. Kwa wastani, binadamu hufa wakiwa chini au nusu ya umri waliopaswa kuishi duniani kutokana na kusumbuliwa na magonjwa yaliyosababishwa na kuwa na staili mbovu ya maisha, hasa katika ulaji wa vyakula hivyo visivyo hai.

Halikadhalika wanyama wanaofugwa majumbani, nao kutokana na kuishi karibu na binadamu kula vyakula vilivyopikwa, hujikuta wakiugua magonjwa ya kibinadamu, kama vile kansa, magonjwa ya miguu, mafua, homa na mengine mengi.

Inaelezwa pia, wastani wa umri anaoweza kuishi binadamu ni kati ya miaka 120 hadi 140! Lakini umri huu haufikiwi kutokana na madhara ya kula zaidi vyakula vilivyopikwa (visivyo hai) na kutokujua mbinu za kukabiliana kwa ustadi na mfadhaiko wa maisha.

Kwa mujibu wa historia, binadamu amekuwepo duniani kwa mamilioni ya miaka. Kabla ya kuanza kutumia moto, miaka 10,000 iliyopita, binadamu huyu hakuwa akiishi kutokana na mlo zaidi ya vyakula vibichi, hai na visivyo chomwa moto, ambavyo vlikuwa halisi na asilia vikiwa na uhai wake wote.

Hali ilivyo hivi sasa ni tofauti, kabla ya kula kitu chochote, binadamu hutumia moto kwanza kukiandaa, hata maji ya kunywa lazima ‘yapigwe’ moto kwanza! Wanao tetea hoja hii wanadai kwamba ulaji wa vyakula visivyo hai ni sawa na kula majivu, kwa sababu virutubisho tunavyovila ambavyo vilishateketezwa na moto, vinapoingia mwilini hugeuka kuwa sumu.

Kibaiolojia binadamu anapaswa kula vyakula ‘fresh’ tu, kwani ulaji wa vyakula hivyo ni bora kuliko vya kupika na ndivyo vinavyoweza kuongeza umri wa mtu. Vyakula hai au freshi ndivyo vinavyomuweka binadmu katika hali na afya njema na kumkinga na maradhi yanayochangia kwa kiasi kikubwa kufupisha umri wake wa kuishi hapa duniani.

UTAFITI WA KISAYANSI WATHIBITISHA VYAKULA VISIVYOPIKWA HUTOA KINGA DHIDI YA KANSA NA MAGONJWA YA MOYO

Katika suala hili, ushahidi wa kisayansi unaonesha kwamba milo inayotokana na vyakula visivyopikwa, vina uwezo wa kupunguza sumu kwenye utumbo. Kwa mujibu wa wanasayansi Ling W.H na Hanninen O, kutoka Idara ya Elimu ya Mifupa ya Chuo Kikuu cha Kuopio, nchini Finland, vyakula visivyopikwa hupunguza madhara yatolewayo na vimeng’enyo (Enzymes) na aina fulani ya sumu mwilini, ambayo ndio huwa chanzo cha maradhi ya saratani ya utumbo.

Vilevile watafiti hao wamegundua kwamba milo yenye kiwango kikubwa cha mboga, hupunguza hatari ya mtu kupatwa na saratani ya matiti na ulaji wa matunda kwa kiasi kikubwa hupunguza hatari ya kupatwa na saratani ya utumbo, utafiti huo ni kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye jarida linalotoa elimu kuhusu magonjwa ya milipuko (Epidemiology), toleo la Mei 1998.

Aidha, taarifa ya jarida lingine linalotoa habari kuhusu masuala ya tiba linalochapishwa nchini Uingereza, toleo la Septemba, 1996, imesema kuwa ulaji wa matunda, kama sehemu ya mlo wa kila siku, hupunguza vifo vinavyotokana na mshituko wa moyo kwa asilimia 24.

JOTO JINGI HUONDOA UHAI WA VIRUTUBISHO

Moto unapounguza kidole chako, tishu za ngozi nazo hufa. Vivyo hivyo, vyakula na virutubisho vinapopikwa huwa vinaharibika kwa kiasi fulani. Kabla ya vyakula kuharibika au kupikwa, huwa vina uwezo wa kukaa kwa muda mrefu vikiwa safi. Vyakula vitokavyo shambani na kuliwa vingali freshi, hutoa mali ghafi ambazo huzipa uhai na kung’arisha seli na tishu zetu mwilini.

Vyakula vinavyopikwa kwa muda mrefu huwa vimeharibu uhai wake hivyo kutokuwa na uhusiano wowote na ustawi wa afya ya mwanadamu. Kwa maana nyingine, vyakula visivyopikwa huwa na uhai wake wote na mwanadamu anapovila, huwa amepata vile virutubisho vyote ambavyo vinapatikana kwenye chakula hicho.

Hebu tuangalie mchanganuo huu unaotokea kwenye kirutubisho pale chakula kinapopikwa kwa joto kali. Inaeleweka na kutambulika vyema katika fasihi nyingi za kisayansi kwamba joto huvunja vunja vitamini na virutubisho vingine na hutoa uhusiano usio sahihi wa protini, hasa kwenye nyama.

Chakula kinapopikwa, kwa zaidi ya nyuzi joto 117 tu kwa muda wa dakika 3 au zaidi, uharibifu mkubwa kwenye virutubisho hutokea na huongezeka kadri joto la kupikia linavyoongezeka. Katika mchakato huo wa kupika chakula, vitu vingi hutokea na kusababisha uharibifu mkubwa kwenye virutubisho vyote na kupunguza uwezo wake wa kufanya kazi yake ipasavyo kwa kati ya asilimia 30 hadi 50.

Aidha inaelezwa kwamba, kadri joto la kupikia linavyopanda, ndiyo virutubisho katika chakula vinavyotoweka. Njia nyingi za kisasa zinazotumiwa kuandaa chakula, huondoa viwakilishi vinavyotoa kinga dhidi ya saratani, lakini upikaji chakula huzalisha viwakilishi vya kansa na vitu vigeni hujitengeneza mwilini ambavyo baadae husababisha maradhi mengine.

Siyo jambo la ajabu kuona kwamba tangu mwaka 1950, matatizo ya kansa yameongezeka na kufikia kiwango cha juu kabisa nchini Marekani kutokana na watu kutawaliwa na ulaji wa vyakula visivyo hai vya aina mbalimbali. Ulaji wa vyakula vilivyopikwa sana husababisha upungufu wa lishe mwilini na matokeo yake kusababisha mwili kuvamia akiba ndogo iliyobaki mwilini na kubaki na njaa baada ya kukosa lishe hiyo.

Katika elimu ya mimea imethibitishwa kwamba upikaji chakula huharibu protini na hukifanya chakula hicho kuwa hakifai kabisa. Ili kujipatia protini ya kutosha mwilini, watu wameshauriwa kula matunda fresh, mboga, karanga, korosho mbichi kama chanzo cha uhakika cha protini.

Unavyotumia kwa wingi vyakula freshi kama mlo wako wa kila siku, mwili huzoea na kuufanya uhitaji chakula kingine kwa kiasi kidogo. Kadri unavyokula vyakula hai vyenye virutubisho zaidi, mwili huendelea kuwa na afya njema na uwezo wake wa kusaga na kukikubali kila unachokula, huongezeka. Protini itokanayo na mbegu kama karanga, korosho, ni bora kuliko ile inayopatikana kwenye bidhaa za wanyama.

TOFAUTI YA JOTO LA KUPIKIA NA LA KUSAGIA CHAKULA TUMBONI

Katika suala hili, wana saikolojia wanadai kwamba joto la kupikia chakula na joto lililo katika mfumo wa kusaga chakula tumboni ni karibu sawa. Wanadai kwamba upikaji ni utangulizi tu wa kukisaga chakula, kazi ambayo ingeweza kufanywa hata na joto la tumboni tu. Kwa maana nyingine, ukikipika chakula kinapoingia tumboni hupikwa tena, hivyo kukifanya kupikwa mara mbili.

Inaelezwa kwamba kuna njia mbili tu za kuondoa uhai katika chakula; mosi kwa njia ya vimeng’enyo (enzymes) ambayo kila mtu anayo na matumizi ya joto. Iwapo chakula kitaondolewa uhai wake kwa njia ya joto la kupikia, mwili hua hauna uwezo wa kurejesha virutubisho vyake (amino acids) pale chakula kinapoingia mwilini.

Tukiacha maelezo yote hayo ya kisayansi na kisaikolojia, ulaji wa vyakula hai ni hatua moja nzuri kuelekea kwenye afya njema. Ulaji wa kutosha wa matunda na mboga, huupa mwili wako nguvu imara bila kuacha maradhi yoyote au kutengeneza sumu mwilini mwako.

Hoja hizo ni changamoto kwa wale wakereketwa wa masuala ya afya, hatuna budi kutafakari na kupima hoja au dhana hii ya chakula hai na kisicho hai na kuendelea kuwa wachunguzi na wachaguzi kwa kila kitu tunachopitisha mdomoni kwenda tumboni.

Ni ukweli uliowazi kwamba vitu vingingine tunavila vikiwa vimepikwa kwa mazoea au ladha tu, lakini vinaweza kuliwa vikiwa vibichi. Mboga mboga kama vile nyanya, karoti, vitunguu, nakadhalika, ni mfano wa vitu vinavyoliwa baada ya kupikwa kwa ajili ya ladha tu.

Hata hivyo, katika hoja hii, bila shaka mtoa mada hakuwa na maana kwamba kila kitu kiliwe bila kupikwa na hakitakuwa na madhara. Suala la msingi kuzingatia, vyakula tunavyolazimika kuvipika basi tuvipike kwa choto la chini kadri iwezekanavyo na si kila chakula lazima kipikwe, tujifunze kula na vibichi kwa faida ya afya zetu.

Kwa mchango wa maoni na hoja zingine, nitumie maoni yako hapo chini....

No comments: