Sunday, July 29, 2007

USWAHILINI KWA VITUKO! AIBU!


MARIAM MNDEME NA CHRISTOPHER LISSA

Ilikuwa ni aibu ya aina yake mwishoni mwa wiki iliyopita wakati warembo wawili walipozichapa kavukavu baada ya mmoja wapo kumfuma mwenzake akiwa anaponda raha na mpenzi wake, ambaye ni kigogo wa chama kimoja cha siasa.

Tukio hilo, lililojaza umati wa watu, lilitokea maeneo ya Buguruni katika baa maarufu ya Kimboka By Night. Varangati lilianza baada ya wapambe kumtonya msichana huyo kuwa mpenzi wake (kigogo, jina tunalihifadhi) ameonekana akiwa katika mikao ya kimahaba akiwa na rafiki yake kipenzi aliyejulikana kwa jina moja la Anna.

Hatua aliyoichukua msichana huyo, ni kutia timu kwenye baa hiyo ambako baada ya kufanya msako wa meza hadi meza, alimkuta kigogo huyo akiwa amekaa mkao wa kimahaba mazito na shoga yake na bila kuchelewa akaanza kutembeza kichapo.

Alianza kwa kumnyanyua Anna juu juu na kisha kumpa kipondo kikali mithili ya ‘mbwa mwizi’. Baada ya kuona siri imefichuka na watu wameanza kujaa, kigogo huyo aliamua kuingia mitini na kuacha zogo kubwa katika baa hiyo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari kilichokuwepo eneo la tukio, wasichana hao walikuwa ni marafiki wa muda mrefu na kibosile huyo alikuwa akiwala uroda kwa zamu, ingawa kila mmoja alikuwa akimficha mwenzake.

Hata hivyo msichana huyo aliepuka kipigo zaidi baada ya kuokolewa na walinzi wa baa hiyo wakisaidiwa na wasamaria wema, ingawa tayari alikwisha jeruhiwa vibaya usoni na kuchaniwa nguo zake na kuvuliwa wigi alilokuwa amevaa.

No comments: