Sunday, July 29, 2007

Mama Nanihii jamani!!


Mama mmoja, ambaye hakujulikana jina lake mara moja, alinaswa na kamera yetu usiku wa manane 'akibanjuka' huku akiwa na mtoto mgongoni katika tamasha la 'One Mike' lililofanyika usiku wa kuamkia jana katika Viwanja vya Leaders, jijini Dar es Salaam.

Katika tamasha hilo, ambalo liliwakutanisha wasanii wengi kutoka Uganda, Kenya na Tanzania, ‘mama nanihii’ alifikia hatua hiyo ya 'kubanjuka' bila kujali mtoto aliyembemba, baada ya kushindwa kujizuia wakati wasichana wanne wa kundi mahiri la Obsessions kutoka Uganda walipokuwa wakitumbuiza jukwaani.

Akifuatiliwa na kamera yetu, mama huyo alionekana mara kadhaa akihangaika kutafuta sehemu nzuri ya kufuatilia na kuburudika kwa karibu muziki uliokuwa ukipigwa na wasanii mbalimbali waliowatangulia wasichana hao. Hata hivyo, juhudi zake za kusogea mbele na kuwa karibu ya jukwaa, zilikuwa zikikwamishwa na vijana walinda usalama, maarufu kama 'mabaunsa'.

Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu, hatimaye mama huyo alipata upenyo na kukimbilia karibu na jukwaa la muziki ambako alianza kufuatilia muziki huku akirukaruka bila kujali mtoto aliyekuwa amembemba mgongoni mwake.

Katika tamasha hilo, wasanii kutoka Uganda na Kenya walioonekana kukonga nyoyo za mashabiki wao kuliko wasanii wa Tanzania. Alikuwa mwadada Nyota Ndogo kutoka Kenya ambaye alianza kufungua pazia la kushika mashabiki pale alipopanda jukwaani kuimba vibao vilivyompatia umaarufu Afrika Mashariki, kikiwemo kibao cha Watu na Viatu.

Kabla ya kuanza kuimba kibao hicho, msanii huyo aliomba kuimba na mume wa mtu, ombi ambalo lilikubaliwa kwa kujitokeza bwana mmoja aliyevalia bazee ambaye alipewa kiti na kukaa jukwaani huku akikatiwa mauno na kushikwashikwa kimahaba, hali iliyowaacha mashabiki wakipagawa kwa furaha.

Hata hivyo, baada ya mwanadada huyo kufungua pazia hilo, walifuatia wasanii wengine kutoka Kenya, Blu 3, ambao nao waliomba ajitokeze kijana mmoja wa kiume ili wampe raha na katika kufanikisha hilo walimchagua wenyewe kijana mmoja mtanashati kutoka katika kundi la mashabiki waliokuwa karibu na jukwaa.

Wasanii wengine waliotia fora na pengine kuacha historia katika tamasha hilo, ni pamoja na Nameless aliyewaimbisha na kuwapagawisha mashabiki kwa wimbo wake wa Sinzia, msanii DNA kutoka Kenya na wimbo wake maarufu wa Banjuka unaoshika vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini.

Aliyefunga kazi kwa kushika mashabiki alikuwa kijana anayejulikana kwa jina la Juacali ambaye naye alilazimika kurudia mara mbili wimbo wake wa Kwaheri ambao aliimba kwa kushirikiana na msichana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Josline ambaye alijitokeza na kupanda jukwaani kuimba kiitikio cha wimbo huo kwa umahiri mkubwa.

Tamasha hilo, liliopewa jina la One Mike Concert, liliandaliwa na Kituo cha Televisheni cha East Africa katika kusherehekea miaka 5 tangu kuanzishwa kwake. Kituo hicho kinarusha matangazo yake katika nchi za Afrika Mashariki na Kati. (picha zaidi ukurasa unaofuata)

No comments: