Tuesday, July 31, 2007

YOU ARE WHAT YOU EAT



HIZI NI DALILI KUWA MWILINI HAKUKO SAWA!
Awali ya yote naomba kusema kuwa wiki mbili zilizopita, nilikuwa na mfululizo wa makala isemayo Ukimwi siyo ugonjwa bali ni hali, makala ambayo ilizungumzia kwa kirefu tafsiri halisi ya ukimwi na jinsi ambavyo mtu anapatwa na hali hiyo.

Nafurahi kuona makala imeeleweka kwa wengi na nina washukuru wale wote waliofuatilia makala hayo na kutoa pongezi na maoni yao. Lakini napenda kutoa shukrani za pekee kwa Bw. Joseph katto ambaye amekuwa akiishi na virusi vya HIV kwa takribani miaka 20 sasa na ambaye nilimtolea mfano katika makala hayo.

Bw. Katto, kupitia kwa mhariri wa gazeti hili, ameomba tuendelee kueleimsha jamii kuhusu ugonjwa huu na kuwatoa hofu wale ambao wamepimwa na kukutwa na virusi vya HIV kwamba Ukimwi siyo ugonjwa bali ni hali ya kuwa na upungufu wa kinga mwilini, kinga ambayo unaweza kuiimarisha kwa kufuata staili ya maisha ambayo tumekuwa tukiieleza kila siku katika kona hii.

Baada ya kusema hayo, naomba kurudi kwenye mada yangu ya leo. Kama navyosema kila wakati, mwili wa binadamu umeumbwa katika hali ambayo unapaswa kujiendesha wenyewe iwapo utapewa mahitaji yake sahihi. Na pale unapokuwa haupati mahitaji hayo, huanza kutoa dalili fulani kuashiria kwamba hali haiko sawa.

Lakini kwa bahati mbaya sana wengi wetu huwa, ama hatuzijui dalili tunazooneshwa na miili yetu, ama huwa tunapuuzia kwa kudhani kwamba mwisho wa siku mambo yatakauwa shwari tu.

UPUNGUFU WA MAJI MWILINI

Hebu tuanze kwa kuangalia kwanza dalili ya mtu kuwa na upungufu au ukosefu wa maji mwilini. Kwa kawaida, mtu anapaswa kunywa maji kiasi kisichopungua glasi nane (kubwa) kila siku, hiki ni kiwango cha chini kabisa ambacho kinaongezeka kutokana na kazi unazozifanya, kama kazi zako ni nzito, basi utapaswa kunywa mara mbili au tatu ya idadi hiyo.

Katika suala hili la maji, ambalo kwa mtizamo wangu, ukiwa na nia na ukijua umuhimu wake, kila mtu analimudu bila tatizo lolote, lakini watu wengi hawafikishi kiwango hicho na hata wanapopatwa na dalili fulani fulani huwa hawazijali kutokana na kutotilia maanani afya zao.

Ukitaka kujijua kwamba mwili wako umepungukiwa maji, basi angalia rangi ya mkojo wakati unapokwenda haja. Unapoona mkojo wako ni wa rangi ya kahawia (brown) au njano, basi elewa kwamba mwili wako umepungukiwa maji. Kama lingekuwa gari, basi ‘injini’ tayari imeshachemsha, kuendelea kuliendesha hivyo hivyo ni sawa na kuiharibu kabisa injini.

Kwa kawaidi mtu unapaswa kukojoa mkojo mweupe kila wakati na hali hii utaiona pale unapokuwa umekunywa maji au matunda ya kutosha. Maji ndiyo msingi wa maisha ya kila siku ya binadamu, hakuna kitu au kiungo kinachoweza kufanyakazi mwilini bila maji, na ndiyo maana unapozidiwa na kukimbizwa hospitali, kitu cha kwanza ni kuchomwa ‘dripu’ ya maji na tiba nyingine ifuate baadae.

Hivyo ili kuuweka mwili wako katika hali inayotakiwa, hakikisha unakunywa maji ya kutosha kila siku na lisiwe jambo la kubahatisha. Unapokojoa mkojo wa njano au rangi ya kahawia, elewa mwili unakutaarifu kwamba umepungukiwa maji na usipotii, madhara yake utayaona baadae na wala hutaweza kujua chanzo chake.

UKOSEFU WA CHOO KWA SIKU KADHAA

Ni jambo la msingi sana binadamu kujielewa mwili wako unafanya vipi kazi, iwapo utakuwa hulijui hilo, basi uko hatarini kushambuliwa na magonjwa hatari bila kutarajia. Kwa kawaida binadamu anapaswa kupata choo kila siku, kama siyo mara mbili au tatu kwa siku, basi angalau mara moja, kutegemeana na ratiba ya ulaji wake wa kila siku.

Lakini baadhi ya watu hupata choo kwa taabu sana na wengine huweza kukaa hata wiki nzima bila kupata choo, hata hivyo hudhani kwamba kila kitu kiko sawa, hii ni hatari. Iwapo unakula kila siku na hupati choo cha kutosha au hupati kabisa kwa zaidi ya siku moja, elewa mfumo wako wa kusaga chakula hauko sawa na hilo ni tatizo, sawa na kutengeneza bomu ambalo siku moja litakulipukia.

Iwapo unapatwa na hali hiyo, unatakiwa kuanza kuchukua hatua za haraka kukabiliana nalo haraka, ikiwa ni pamoja na kunywa maji asubuhi mapema, kabala ya kula chochote au kula matunda ya kutosha, hasa papai bivu.

Lakini jambo lingine la msingi katika upataji wa choo bila matatizo ni kuzingatia ulaji wa vyakula vyenye virutubisho (rejea makala zetu zilizopita) na kujiepusha na ulaji wa vyakula vya kukaanga kwa mafuta na ulaji wa vyakula visivyo na virutubisho. Tuonane tena wiki ijayo kwa makala nyingine.


No comments: