Tuesday, July 31, 2007

VIGOGO DAWA ZA KULEVYA WANASWA!


Makongoro Oging na Elvan Stambuli

Wafanyabiashara vigogo wa dawa za kulevya watano wamekamatwa katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kile kinachodaiwa kuwa wamekuwa wakijishughulisha na biashara hiyo haramu.

Akizungumza na Waandishi wetu ofisini kwake Kurasini Dar es Salaam juzi, Mkuu wa Kitengo cha Kuthibiti Dawa za Kulevya Nchini , Kamishna Msaidizi wa Polisi , Bw. Godfrey Nzowa alisema kuwa wafanyabiahsra hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti.

Aliwatajha wafanyabiahsa hao waliokamatwa na polisi kuwa ni Bi Zubeda Kassim (42) mkazi wa Mchikichini Ilala ambaye alidakwa Julai 22, mwaka huu saa 2:00 usiku maeneo ya Mtaa wa Mzizima Kariakoo akiwa na kete 5,000 ambazo alikuwa akizipeleka sokoni na kuongeza kuwa ndiye mwanamke anayeongoza kwa kukamatwa na kiasi kikubwa ya dawa hizo mwaka huu.

Alimtaja mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa kuwa ni Bw. Mbwana Mbaraka Mkanga, Mkazi wa Ukonga Wilaya ya Ilala ambaye alikuwa akitafutwa na jeshi lake , alitiwa mbaroni Julai 17 mwaka huu maeneo ya Uwanja wa ndege wa Mwalimu Jul;ius Nyerere akitokea Iran , ambapo aliondoka hapa nchini Mei 17,2007 kupitia Tanga na kupanda ndege uwanja wa Jomo Kinyatta nchini Kenya.

Kamishna Nzowa alisema kuwa Bw. Mkanga alitumwa na tajiri mmoja Mtanzania ambaye anaishi Hong Kong, hata hivyo alikataa kumtaja jina kwa madai kuwa anaweza kuvuuga mwenendo wa kazi zao wa kuwadaka vigogo wengine.

Alisema kuwa naye Bw. Godwin Vitus Chacha (25) Ambaye alikuwa akitafutwa kwa kuhusishwa na biashara hiyo alikamatwa Julai 17, mwaka huu maeneo ya Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius . Nyerere akitokea Irani kupitia Dubai.

Alisema kuwa mtu mwingine , Bw. Mkangana Chacha waliporejea nchini wakitokea Iran hawakuwa na dawa hizo baada ya kupata taarifa kuwa kumekuwa na udhibiti mkubwa, hivyo, walitumwa na mwaajiri wao kuja kuangalia hali ya hewa ndipo walipokamatwa.

Wafanyabiashara wengine haramu wa mihadharati waliokamatwa Tanga Julai 17 mwaka huu aliwataja kuwa ni Amiri Juma (29) aliyekutwa na misokoto 64 ya bangi, Julias Benard (26), kilo kumi za mirungi, Slivin John (28), misokoto 43 za bangi, Musa Maganga (42) kete 8 za Heoin.

Kamishna Nzowa alisema kuwa kuna wafanyabiahsra wengine wakubwa waliokamatwa ambao majina yao yatatajwa hivi karibuni katika mkutano na waandishi wa habari.

“Kwa sasa vijana wangu wamejizatiti katika kuhakikisha kuwa biashara hiyo inadhibitiwa kwa kiasi kikubwa, na ninawashukuru raia wema kwa kutoa taarifa polisi na kuwezesha kukamatwa kwa watu hao” alisema Nzowa.

Aliendelea kusema kuwa watu wanaojihusisha na biashara hizo wana mtandao mkubwa sana Duniani na vinara wao inashindikana kuwakamatwa kutokana na kuwa wao hawazishiki dawa hizo na kazi yao ni kutafuta hati ya kusafiria na viza ili kuwapa mawakala wao kusafirisha.

Alisema kuwa watu hao waliokamatwa wamefikishwa mahakamani na kuna wafanyabiashara wengine wa dawa hizo wanatafutwa ndani na nje ya nchi.

Aliongeza kusema kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali za kusafirisha madawa ya kulevya pale njia walizokuwa wamezizoea zinapogundulika.

Kamishna Nzowa alisema kuwa kwa sasa vijana wengi wanaojihusisha na biahsra hiyo wamekuwa wakirudi nchini mikono mitupu kufuatia udhibiti mkubwa unaofanywa na vijana wake kwa ushirikiano na wananchi, pia wamekuwa wakitoa elimu juu ya dawa za kulevya na madhara yake.

Wakati huo huo baadhi ya askari polisi wameilaumu serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa kushindwa kuboresha masilahi yao ingawa wamekuwa wakiahidiwa.

Aidha askari hao ambao hawakupenda kutaja majina yao kwa kile walichodai kuwa ni kwa usalama wao kikazi, walisema kuwa wamekuwa wakiishi maisha duni kutokan na mshara mdogo wanayopata.

Askari hao walisema walitegemea mishahara yao ya mwezi huu ingeongezwa lakini serikali haikufanya hivyo.

Naye Juma Mohamed mkazi wa Magomeni aliyehojiwa kuhusiana na malalamiko ya polisi alisema kuwa licha ya wizaa ya usalama wa raia kuboresha na kuongeza vitendea kazi kama vile pikipiki magari, Redio call, pia kukarabati ofisi na majengo ya vituo vya polisi na kuongeza wilaya, lakini kazi haiwezi kuwa nzuri kama maslahi ya askari ni duni.

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Kamishna Robert Manumba alikaririwa akisema maslahi ya askari polisi yataboreshwa, hivyo kuwataka kuondoa wasi wasi.




HUU NI UNYAMA
Na Dunstan Shekidele,Morogoro.

Mwanafunzi mmoja wa Shule ya Msingi ya Kaloleni, mjini Morogoro, Ally Ramadhani (16) na mkazi mwingine wa Kihonda, Hassani Nassoro Salehe (29) wameuawa kinyama na baadhi ya wakazi wa Kihonda kwa kudhaniwa kuwa ni wezi.

Marehemu hao siku ya tukio Julai 26 mwaka huu saa nne usiku walikuwa wanahamisha godoro na kitanda kutoka Kihonda kwa ndugu yao Nuhu Nassoro Salehe kuelekea maeneo ya mji mpya mkoani hapa ndipo walipokamatwa na wananchi wa eneo hilo na kasha kuwachoma moto mpaka kufa wakihisi kuwa walikuwa ni vibaka.

Akielezea tukio hilo Bw. Nuhu ambaye ni mdogo wa marehemu Hasani,alikuwa na haya ya kusema:

“Ndugu yangu (marehemu) alikuja kuomba kitanda kwangu kwa kuwa anajua niko peke yangu, nikampa na godoro, hivyo alimchukua kijana ambaye ni jirani yake ili amsaidie hadi kwenye kituo cha daladala, niliondoka kuelekea kazini na kumuagiza ndugu yangu kuwa funguo aache kwa fundi cherehani, lakini nilipofika asubuhi nikakuta mauaji,” alisema Nuhu huku akitokwa na machozi.

Aliongeza kuwa habari alizozikuta eneo hilo la tukio zilidai kwamba baada ya vijana hao kuonekana wamebeba kitanda na kisha hawafahamiki walianza kuitwa wezi ambapo walijitetea kwamba wao sio wezi na kwamba kitanda ni mali yao lakini baadhi ya wananchi hawakuwaelewa hivyo kuanza kuwapiga kisha kuwachoma moto mpaka wakafa na kisha wakatawanyika.

Mwenyekiti wa mtaa huo (wa Majengo Mapya) Bw Juma Yamo alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo alikiri kutokea na akasisitiza kuwa vijana hao waliouawa hawakuwa vibaka hata hivyo aliwashutumu kwa kusafirisha kitanda hicho nyakati za usiku wakati i wao ni wageni maeneo hayo licha ya kufahamika kuwa watu wasio na uwezo wa kupata usafiri wa gari huhama nyakati za usiku kwa tutumia miguu.

Akijitetea kwa tukio hilo mwenyekiti huyo wa mtaa alisema: "Usiku huo huo mimi nilitoka nikaelekea eneo la tukio baada ya kupewa taarifa na mjumbe mmoja ambapo nilipofika nilikuta miili ya vijana hao ikiendelea kuteketea kwa moto na kwamba sikukuta mtu yoyote hapo…,ninachotaka kusema ni kwamba siku za hivi karibuni katika mtaa wangu nimepokea malalamiko ya watu kuibiwa vitu vyao” alilalamika kiongozi huyo.

Baba mlezi wa mtoto Ally Bw . Nyenyembu ambaye ana mguu mmoja baada ya mguu wa pili kutwa,kufuatia kupatwa na ugonjwa wa kansa mguu wa pili,alisema kwamba kijana wake huyo ndiye akiyekuwa akimtegema katika mambo mengi kutokana na hali yake hiyo ya ulemavu na kwamba mwanae huyo hakuwa na tabia ya wizi.

Naye Mwalim Mkuu wa Shule ya Kaloleni aliyokuwa akisoma marehemu, Bi Blandina Mahai huku akitokwa na machozi alisema kwamba amesingitiswa sana na kifo cha mwanafunzi wake huyo ambaye alikuwa miongoni mwa watoto watiifu.

Awali Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Bw. Thobias Andengenye alipotoshwa na akatoa taarifa kwa waandishi wa habari kwamba vijana waliouawa walituhumiwa kuvunja nyumba ya Bw.Nuhu hata hivyo aliwalaani wananchi waliofanya kitendo hicho cha kujichukulia sheria mkononi na akaonya kuwa watakaobainika kufanya kitendo hicho watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Siku iliyofuata mwandishi wetu alimfuata tena kamanda huyo na kumueleza tukio zima lilivyo ambapo Andengenye alionekana kusikitiswa sana na aliahidi kuwasaka kwa udi na uvumba wote waliohusika na unyama huo.


No comments: