Saturday, August 18, 2007

MREMBO AFIA GESTI 'AKIKANDAMIZA' NA DOKTA!

Na Dotto Mwaibale
Mrembo aliyefahamika kwa jina la Fatuma Hassan Samata(31) ambaye ni mhudumu wa baa ya Maduka Matatu iliyopo Mwananyamala, jijini Dar es Salaam amekutwa amefariki ndani ya nyumba ya kulala wageni (gesti) ya Mahamo Inn iliyopo Mwananyamala akigandamiza raha na daktari aitwaye John Mtali.

Tukio hilo limetokea Jumatano wiki hii usiku ambapo mwanamke huyo alifika katika nyumba hiyo ya wageni akiwa na mwanaume mmoja aliyetajwa kuwa ni daktari wa zahanati moja ya binafsi iliyopo jirani na gesti hiyo.

Habari zaidi zinasema kuwa daktari huyo aliruka ukuta wa gesti hiyo na kukimbia baada ya kubaini kuwa mpenzi wake alikuwa amekufa.

Kufariki kwa mrembo huyo kulijulikana asubuhi baada ya mhudumu wa gesti hiyo, Onesmo Sigalla kufungua chumba hicho alipoona wateja wake hawatoki.

Akiongea na mwandishi wetu, kijana mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake aliyeingia ndani ya gesti hiyo kwa lengo la kuutambua mwili wa marehemu, alisema walikuta ukiwa hauna nguo na pembeni yake kukiwa na kondomu.

‘’Tulimkuta marehemu amelala kitandani huku akiwa hajavaa nguo yoyote, damu ikimtoka mdomoni, juu ya kitanda alichokuwa amelala kulikuwa na kondomu,” alisema kijana huyo.

Habari zaidi zinasema kuwa daktari anayedaiwa kuwa na Fatuma alifika katika gesti hiyo kushuhudia kilichokuwa kikiendelea, lakini baadhi ya watu waliomuona walimtambua, hivyo alitoweka kiaina baada ya kubaini kuwa alijulikana.

Polisi walifika eneo la tukio na kuchukuwa mwili wa marehemu kisha kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Mwananyamala ambapo hadi sasa askari hao wanamsaka daktari huyo.

Akielezea tukio hilo, wifi wa Fatuma aliyejitambulisha kwa jina la Zaituni Jalufu, aliyekuwa akiishi na marehemu alisema kwamba Jumatano wiki hii saa mbili usiku, akiwa nyumbani kwake na marehemu, alifika mhudumu mmoja wa baa ya Maduka Matatu.

Zaituni alisema, mhudumu huyo alimweleza kuwa kulikuwa na mtu aliyekuwa akimhitaji Fatuma ambapo alimjulisha na kuongozana naye hadi katika baa hiyo.

Alisema ilipotimu saa mbili na nusu usiku, Fatuma alirejea nyumbani hapo akiwa na daktari huyo ambapo alimuaga kuwa anaondoka kidogo angerudi baadaye, lakini hakumuona tena hadi alipopata taarifa ya kifo chake.

Aidha, baadhi ya watu waliokuwa wakinywa katika baa hiyo ambao walihojiwa na mwandishi wetu walisema kuwa walimuona Fatuma na daktari aliyetajwa kuwa naye wakipata ‘moja moto, moja baridi’, kisha waliondoka.

Mwandishi wetu alimpigia simu daktari, alipomuuliza kuhusu tukio hilo alimtaka waonane sehemu kwa ajili ya maongezi zaidi lakini hakwenda.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.


zitto kuuawa?

Na Makongoro Oging
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) Mhe. Zitto Kabwe anadaiwa kuwa maisha yake yako hatarini, hivyo wananchi wameomba awekewe ulinzi madhubuti ili asiuawe.

Kauli hiyo imetolewa jana na baadhi ya wananchi waliokuwepo katika maandamano ya ndani yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na kufanyika Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Wananchi hao walifanya maandamano kufuatia adhabu ya kusimamishwa kwa mbunge huyo kuhudhuria vikao vya bunge hadi mwakani kutokana na hoja yake kuwa kuna utata katika mkataba wa madini uliotiwa saini na Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi.

Wananchi hao ambao walipewa nafasi ya kuongea katika maandamano hayo na wengine kuhojiwa na mwandishi wetu, walisema kuwa hoja aliyotoa Kabwe ni nzito hali ambayo imeonyesha kuwa wabunge wengi hasa kutoka chama tawala hawakupendezewa nayo.

Katika maandamano hayo kulikuwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali kama vile ‘wabunge wekeni maslahi ya taifa mbele’, sheria, kanuni za Bunge zibadilishwe’, Nyerere angekuwepo mngefanya hayo?’ na Sitta acha ubabe Bungeni.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Bi. Usu Mallya alisema kuwa ajenda kubwa ya maandamano hayo ilikuwa ni pamoja na kupinga adhabu ya kusimamishwa kwa Zitto kuhudhuria vikao vya Bunge.

Hata hivyo, wananchi hao wamemhakikishia Zitto kuwa wako nyuma yake kwa lolote na kuwataka viongozi wa chama chake kumwekea ulinzi asiuawe.

“Nani amethibitisha kuwa Zitto amesema uongo na ni uongo upi wakati waziri amekubali amesaini mkataba huo huko London? Tunachokiuliza ni kuwa imekuwaje waziri asaini wakati Rais alizuia mkataba wowote kusainiwa hadi ya awali ipitiwe?” Alisema John Michael mkazi wa Masaki.

Zitto alipohojiwa na mwandishi wetu juu ya usalama wa maisha yake kufuatia hoja yake aliyotoa bungeni, alisema kuna wakati inalazimika kujitoa kafara katika kutetea maslahi ya taifa.

“Kuna wakati inalazimu ku-sacrifice katika kutetea maslahi ya taifa na hivyo ndivyo nilivyofanya,” alisema mbunge huyo.

Hata hivyo, mapokezi makubwa ya mbunge huyo yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam leo.




No comments: