Thursday, August 16, 2007

Zitto Kabwe asamehewa!


Na Luqman Maloto
Ikiwa ni siku mbili tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Zubeir Kabwe aliposimamishwa kuendelea na shughuli za bunge, Watanzania wameamua kumsamehe mwakilishi huyo kijana.

Msamaha huo wa Watanzania, unagusa katika makosa yote ambayo Kabwe amewahi kuyafanya ndani na nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwakuwa sasa mwakilishi huyo ni shujaa wa nchi.

Wakiongea na Ijumaa, Jumatano hii jijini Dar es Salaam, Watanzania hao walisema, wanamsamehe Kabwe kwa sababu ameonesha ujasiri kwenye kutetea ukweli na kwamba adhabu aliyopewa na bunge ilikuwa na lengo la kumdhoofisha kisiasa.

"Naamini kila Mtanzania amemsamehe Zitto na ameonesha yeye ni mtu wa namna gani mbele ya maslahi ya wananchi, ukitembea barabarani watu wanalia, tunaumizwa na adhabu aliyopewa kwa sababu haikuwa ya haki," alisema Rashid Kasesa, mfanyabiashara wa dagaa, Soko la Kariakoo.

Bi. Hamida Banzo wa Magomeni alisema, kusudio la bunge lilikuwa ni kummaliza Zitto kisiasa, lakini imeshindikana kwani wananchi walio wengi wanamchukulia mbunge huyo kama mwakilishi shujaa na mtetezi wa kweli wa haki za Watanzania.

"Kuna watu walimchukulia kama msaliti, wakati alipohusishwa na kashfa ya mapenzi na Marehemu Amina Chifupa, inawezekana ilikuwa ni kumchafua tu, lakini kwa adhabu aliyopewa hivi sasa, Watanzania tumeona ukweli uko wapi, Mungu atamsaidia ili arudi bungeni kututetea," alisema Sweetbert Kamau wa Ilala.

Jumanne wiki hii, Zitto alisimamishwa kuendelea na bunge hadi Januari mwakani baada ya wabunge wengi kupiga kura ya kumuadhibu mbunge huyo. Kufuatia adhabu hiyo atakuwa akilipwa nusu ya mshahara bila posho na hatoruhusiwa kuhudhuria vikao vya kamati katika kipindi chote hicho.

Hata hivyo, gazeti moja liliripoti jana kuwa wachimbaji wadogo wadogo wa Mgodi wa Mererani, Arusha wameahidi kumlipa mbunge huyo mshahara na marupurupu yake yote katika kipindi chote ambacho atakuwa akitumikia adhabu aliyopewa.

Adhabu hiyo ilimkuta Zitto baada ya kuwasilisha hoja binafsi bungeni ya kuomba kuundwa kwa Kamati Teule ya kuchunguza ukiukwaji wa kanuni na uvunjaji wa sheria uliofanywa na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi wakati wa kusaini mkataba na Kampuni ya Barrick Gold Corporation juu ya mgodi wa Buzwagi.

Katika hoja yake, Zitto alitaka uchunguzi ufanyike ili ukweli uwekwe wazi juu ya kwanini mkataba huo ulisainiwa London, England badala ya nchini na kulikuwa na sababu zipi za kuuharakisha kama ilivyofanyika? Ingawa kauli ya wabunge wengi ilidai amedanganya Mbali na Watanzania hao, viongozi mbalimbali wa kisiasa wameshatoa tamko la kupinga adhabu ya Zitto sambamba na kumuandalia mapokezi ya kishujaa kesho jijini Dar es Salaam mara atakapowasili akitokea Dodoma.

Aidha, Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila aliliambia Ijumaa jana kwamba anakusudia kuwasiliana na wanasheria wake ili kumshtaki Spika wa Bunge, Samuel Sitta na bunge zima kwa kumuadhibu Zitto.

Akiongea na gazeti hili jana, Zitto alisema, kanuni ya bunge namba 59 iliyotumika kumuadhibu ilipindishwa ili kumkomoa kwa sababu haihusiani na masuala ya adhabu bali huwepo kwa ajili ya usalama bungeni.

"Iliandaliwa kunikomoa, watu wasome hoja yangu, wapitie majibu ya Karamagi halafu wageukie katika hoja ya Hamad ( Kiongozi wa Upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohammed), watu watajua ukweli na kumbaini aliyesama uongo," alisema Zitto.

Aidha mbunge huyo aliongeza kuwa tayari amewasiliana na wanasheria wake ili kulifanyia kazi suala hilo kwani anaamini ameonewa.

"Kwa ujumla kuna juhudi za kuiomba mahakama ifuatilie kuona kama kuna kanuni ilikiukwa katika adhabu niliyopewa," alisema mbunge huyo jana.Alisema kuwa haogopi kutetea ukweli hata kama itakuwa ni kwa kuhatarisha maisha yake, kwavile anaamini yuko sahihi kwa kauli aliyoitoa bungeni.




Bwana harusi afumaniwa!

Na Dotto Mwaibale
Bwana harusi mtarajiwa aliyefahamika kwa jina la Kalebi Msanjila, amefumwa akifanya mapenzi na msichana mwingine aitwaye Lucy Damian (17) aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo cha ushonaji, kisha msichana huyo kujinyonga.

Tukio hilo la aibu lilitokea Agosti 9, mwaka huu Kimara Matangini, jijini Dar es Salaam. Akiongea na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita, Venance Mponzi ambaye ni mjomba wa msichana aliyefumaniwa alisema kuwa Lucy alikuwa akilala katika chumba cha uani kwenye nyumba anayoishi.

Alisema kuwa wakati wakiishi naye alipata taarifa kutoka kwa majirani zake kuwa mpwa wake alikuwa na tabia ya kuingiza wanaume katika nyumba yao jambo lililomfanya amkanye mara kwa mara.

"Kila nilipofika nyumbani kutoka katika biashara zangu, wapangaji wenzangu walikuwa wakinifahamisha Lucy alikuwa akiingiza wanaume ndani kwangu ndipo nilimkanya aache tabia hiyo," alisema Mponzi.

Aliongeza kuwa kutokana na kuchoshwa na tabia hiyo ndipo alipoamua kumpangia chumba cha uani na kumpatia kitanda na godoro.

Mponzi aliongeza kuwa, Lucy ambaye ni mtoto wa dada yake anayeishi mkoani Iringa, alimleta jijini kwa lengo la kumuendeleza kimaisha, hivyo kumpeleka Kozi ya Ushonaji nguo katika Chuo cha Ufundi cha Kijukuu, kilichopo Kimara Stop Over jijini Dar es Salaam.

Aidha, alisema mara baada ya Lucy kuanza kulala katika chumba hicho, alipata habari kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Msanjila na mara kwa mara walikuwa wakilala pamoja.

"Nilipopata taarifa hiyo nilimuonya na kumsihi azingatie masomo yake lakini alikasirika na kunieleza nikiendelea kumfuatafuata angejinyonga," alisema Mponzi.
Mponzi alisema, siku ya tukio alikuwa amerejea nyumbani saa 2.00 usiku ambapo alipokelewa na Lucy kutokana na mkewe kutokuwepo.

Aliongeza kuwa baada ya kupumzika kidogo, alimuona Lucy akiwa amebeba chakula na kuingia nacho chumbani kwake jambo ambalo halikuwa la kawaida, hivyo aliamua kumfuatilia.

Mponzi alisema ilipofika usiku wa manane alikwenda katika chumba cha mpwae na kugonga mlango lakini hakufungua. Baadaye alikubali kufungua, alipoingia hakuamini macho yake baada ya kuwafuma Lucy na Msanjila wakiwa kitandani.

Aliongeza kuwa baada ya kuwafuma Msanjila alichachamaa na kutaka kumpiga, lakini kwa kushirikiana na wapangaji wenzake walioamka kufuatia tukio hilo, walifanikiwa kumdhibiti.

Hata hivyo, Mponzi alisema kwa kuwa Msanjila na mpwae walikuwa wanaishi nyumba moja, alimwambia Lucy kuwa siku iliyofuata angempeleka hospitali kumpima apate kujua kama alikuwa mjamzito ama la ili aweze kuchukua hatua.

Alisema kuwa baada ya tukio hilo, wote walikwenda kulala, asubuhi alipoona Lucy amechelewa kuamka alikwenda kumgongea mlango, lakini hakufungua ndipo alichungulia dirishani na kumuona akiwa amejinyonga kwa kutumia khanga.

Mponzi alisema kufuatia tukio hilo, alitoa taarifa katika Kituo Kidogo cha Polisi Kimara, ambapo askari walifika na kukuta ujumbe aliouacha marehemu akikiri kufanya mapenzi na bwana harusi huyo mtarajiwa na kuomba msamaha.

Hata hivyo, polisi hawakuweza kumtia mkononi Msanjila kwani alitoweka mara baada ya taarifa ya kifo cha mpenzi wake. Habari zimedai kuwa kutoroka kwa Msanjila kulifanya mipango ya harusi yake kuharibika kwani alitarajia kufunga ndoa mkoani Dodoma siku chache zijazo.

Marehemu Lucy Damian alizikwa Jumatatu ya wiki hii katika Kijiji cha Kanikelele kilichopo Lupembe Wilayani Njombe.

No comments: