Monday, September 24, 2007

Street Version: NDOA YA RICHARD KUVUNJIAKA!

(Richard akiwa na kimwana wa Kiangola kwenye jakuzi pembei kuna mvinyo, kinachoendelea 'huko chini 'Big Brother alikijua?...jamaa hajakandamiza bado, lakini ataweza kuendelea kujizuiaa???)
Wiki hii, kupitia 'Street Version' tunapata maoni kutoka kwa baadhi ya Watanzania ambao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu Shindano la Big Brother Afrika (BBAII) linaloendelea hivi sasa huko Afrika ya Kusini, na kuneshwa Afrika nzima kupitia mtandao wa DSTV.

Ikiwa mtaani safu hii iliwauliza Wabongo hao kwamba, kufuatia mshiriki wa Tanzania, Richard kuwa karibu zaidi na binti wa Kiangola, Tatiana, wakionesha dalili zote za uhusiano wa kimapenzi, Je, upo uwezekano wa ndoa yake na mkewe aliyopo nchini kuvunjika? Swali la pili lilikuwa ni, Je, shindano hilo linaleta maana kwa Watanzania? Sasa twendeni tukaangalie watu wanasemaje.

Jina: Hawa Mohamed Anaishi: Sinza
Maoni: Mimi naona huyu mshiriki wetu ndoa yake itamshinda kutokana na vitendo anavyovifanya na yule dada wa Angola, Tatiana kwa sababu mambo ya mahaba yote wameshafanya wamebakisha kuibanjua amri ya sita tu. Pia mimi sioni kama shindano hilo linatufundisha chochote hasa sisi Watanzania, utamaduni wetu hairuhusiwi kuonyesha hadharani watu wakiwa uchi.

Jina: Khadija Maoti Anaishi: Kariakoo (Mtaa wa Livingstone)
Maoni: Mke wa Richard asipokuwa makini anaweza akavunja ndoa yake kwani kipindi hiki anaonekana amekuwa na wivu sana tofauti na pale mwanzo aliposema anamwamini mume wake sasa iweje imani imtoke? Yeye asubiri aone mwisho wake lakini avumilie tu. Hilo shindano halina maana yoyote kwetu zaidi ya kuvunja maadili ya Kitanzania na kuwafundisha watoto tabia mbaya.

Jina: Mwanaisha Fungo Anaishi: Kigogo Luhanga
Maoni: Mimi sioni kama ndoa yake itavunjika kwasababu mke wake alishaaongea nae na wakakubaliana, kwa hiyo mke atavumilia tu. Pia shindano hilo halileti maana yoyote kwa sisi watanzania, linazidi kuharibu maadili yetu.

Jina: Patrick Mwikile Anaishi: Temeke
Maoni: Kwa kweli haivutii hata kidogo kutuonyesha watu wako uchi au wakifanya vitendo vya ngono nje nje wakati watoto wadogo wanaona. Shindano hilo kwa ujumla halina maana kwetu.

Jina: Gwakisa Mwalukasa Anaishi: Yombo Kilakala
Maoni: Mtu ambaye amelelewa katika mazingira ya dini hawezi kwenda kushiriki mchezo kama ule kwani haufundishi chochote, ndio kwanza unakuharibu na kuonekana kituko katika jamii na pia unaweza kujutia mambo uliyoyafanya ukiwa dani ya jumba lile.

Jina: Juma Ngalihuja Anaishi: Keko Magulumbasi
Maoni: Richard kama yeye angekuwa anajua ameoa angejitunza, mambo ya kuwa na wasichana karibu angeacha ili ailinde ndoa yake. Shindano hilo halina maana kwetu zaidi ya kutufundisha uhuni na kutuharibia watoto.

No comments: