Tuesday, September 25, 2007

YOU ARE WHAT YOU EAT!


FUNGA YA JUISI:

SULUHISHO LA MATATIZO YA KIAFYA, IKIWEMO UNENE!

Wiki iliyopita tuliandika makala kuhusu faida za kufunga kiafya, kwa kufuata taratibu za kidini, kama vile waislamu wanavyofunga hivi sasa kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani na tuliona kwamba ibada hii siyo tu ina faida kiroho, lakini pia kiafya.

Tukiwa bado kwenye mada hii ya funga na faida zake kiafya, wiki hii tutaangalia funga ya kutokula kitu isipokuwa juisi, mboga za majani na maji tu, ikiwa ni tiba mbadala na suluhisho la matatizo mengi ya kiafya mwilini, likiwemo tatizo sugu la unene.

Funga ya juisi ni aina ya funga ambayo huupa mwili lishe inayoondoa sumu mwilini. Funga hii ni ile ya mtu kuacha kula vyakula vingine na badala yake kunywa juisi au kula mboga za majana na kunywa maji kwa kipindi kisichozidi siku 3 mfulululizo. Wafuasi wa funga hii wanaipenda kwa sababu inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kuondoa sumu mwilini kuliko njia nyingine.

FUNGA YA JUISI NI NINI?

Ingawa funga hii hapo awali ilitumika kama tiba ya mtu kuachana na ulevi pamoja na uvutaji sigara, lakini hivi sasa inaeleweka kama ni lishe ya matunda, mboga au miti shamba, inayotumika kuondoa sumu mwilini zitokanazo na uchafuzi wa mazingira na baadhi ya vyakula tunavyokula.

SUMU HUINGIAJE MWILINI?

Tafiti nyingi za kisayansi zinaonesha kwamba kemikali nyingi tunazokula kwa njia ya chakula, maji na hewa tunayovuta, hungia mwilini na kuwamo kwenye seli za miili yetu. Vyakula vinavyokosa virutubisho, huchangia kuharibu mfumo wa asili wa mwili wa kuondoa sumu na matokeo yake sumu hizo hukusanyika mwilini.

Mkusanyiko huo huongezeka siku hadi siku na unaaminika kuwa ndiyo unaosababisha maradhi, kushusha kinga ya mwili na mwili kushindwa kusaga chakula vizuri. Dalili za mwili kuwa na sumu ni pamoja na ukosefu wa choo, kutoa harufu mbaya mdomoni, uchovu, ngozi mbaya na maumivu ya misuli na mgongo.

Ukiacha njia hii, sumu pia hujitengeneza mwilini yenyewe katika mchakato wake wa kawaida wa kuvunja protini na kemikali nyingine kama vile dawa za kuongeza uhai wa chakula (additives), dawa za kutibu maradhi, uchafuzi wa hewa na moshi wa sigara tunaoupata ama kwa kuvuta sigara au kwa kukaa karibu na mtu anayevuta sigara.

FAIDA ZA FUNGA YA JUISI

Faida za funga hii ni nyingi kwa wanaojali afya zao. Lakini mambo yaliyowazi kwa wanaotumia funga hii mara baada ya kumaliza ni pamoja na kuona mabadiliko bora kuanzia kwenye ngozi hadi ubongo. Watu wengi wanaotumia funga hii huondokewa na tatizo la uharara wa ngozi na akili huchangamka na kufanya kazi yake ipasavyo.

Mbali ya faida hizo, pia matatizo mengine ya uchovu, harufu mbaya mdomoni, mgongo kuuma huondoka na mtu mwenye unene huweza kupungua kwa kiwango cha kuridhisha na kwa muda mfupi.

WATU GANI HAWAPASWI KUJARIBU FUNGA HII

Kama ilivyo kwa kila jambo la kiafya, si kila mtu anaweza kutumia kila dawa yoyote. Katika suala la kufunga kwa juisi na maji tu, kina mama waja wazito na wanaonyonyesha pamoja na watoto, hawashauriwi kujaribu funga hii.

Aidha, watu wengine wasioshauriwa kujaribu funga hii ni wagonjwa wa kisukari, wenye matatizo ya kula, wenye ugonjwa wa figo, ini, utapiamlo, wenye uzito mdogo, ugonjwa wa kukauka damu mwilini, vidonda vya tumbo, kifafa, na magonjwa mengine sugu. Iwapo watajaribu funga hii basi ni lazima iwe chini ya ushauri na uangalizi wa karibu wa daktari.

Ili kupata faida ya funga ya aina hii, mfungaji hana budi kuhakikisha hana matatizo makubwa ya kiafya kama yalivyoainishwa hapo juu na wala asizidishe zaidi ya siku 3, kwa kufanya hivyo anaweza kupungukiwa na protini mwilini na hivyo kupatwa na matatizo mengine ya kiafya.

No comments: