Mapigano makali baina ya waumini wa dini ya Kiislam yaliyosababisha kumwagika kwa damu yametokea katika Msikiti wa Masjid Hijra, uliopo Mtongani jijini Dar es Salaam baada ya pande mbili za waumini hao kurushiana silaha kali na kuumizana.
Kwa mujibu wa mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, mapigano hayo yaliyotokea saa 8.30 mwishoni mwa wiki iliyopita na kudumu kwa takriban dakika 30, yalifanya waumini kumi wajeruhiwe na kukimbizwa Hopitali ya Wilaya, Temeke kupata matibabu.
Mtoa habari huyo alisema kuwa kama si polisi wa doria na wale wa Kituo kidogo cha Mtongani kufika eneo hilo mapema na kutuliza ghasia hiyo hali ingekuwa mbaya kwani waumini hao walikuwa wakirushiana mawe, nondo na silaha nyingine kali.
Vurugu hizo zilisababisha Barabara ya Kilwa kutopitika kwa muda kutokana na waumini kujazana huku wakirusha mawe kuelekea msikiti huo mpya.
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, chanzo cha mapambano hayo ni baadhi ya waumini hao kutaka uitishwe uchaguzi wa viongozi na jina la msikiti huo ubadilishwe kutoka Masjid Hjira na kuwa Masjid Badri.
Habari zinasema kuwa msikiti huo awali ulikuwa ukiitwa Masjid Badri kabla kuhamishwa ili kupitisha ujenzi wa barabara mpya ya Kilwa inayoendelea kujengwa hivi sasa ambapo kwa sasa viongozi wanaosimamia wameupa jina jipya la Masjid Hijra.
Waandishi wetu ambao walifika katika eneo la tukio walishuhudia mawe na vipande vya nondo vilivyotumika katika mapambano hayo vikiwa karibu na msikiti huo huku baadhi ya watu wakiwa katika makundi kutafakari tukio hilo.
Aidha, waandishi hao walikwenda katika Hopitali ya Wilaya ya Temeke na kuwakuta baadhi ya waumini waliojeruhiwa wakiwa wanapatiwa matibabu.
Akiongea na mwandishi wetu mmoja kati ya viongozi wa msikiti huo aliyejitambulisha kwa jina la Shehe Mnondwa ambaye naye alipata kipigo kikali, alisema kuwa chanzo cha ugomvi huo ni tofauti ya msimamo kwani wakati wengine wanataka msikiti huo uandikwe jina jipya la Masjid Hijra, huku baadhi wanataka liandikwe jina la zamani la Masjid Badri.
Aidha, Shehe Mnondwa alisema kuwa baadhi ya waumini wanataka kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wapya kutokana na waliopo kumaliza muda wake.
Hata hivyo, kiongozi huyo alisema kuwa kilichosababaisha kushindwa kufanyika kwa uchaguzi huo ni kuchelewa kukamilika ujenzi wa msikiti huo mpya. "Tusingeweza kufanya uchaguzi wakati tuko katika harakati za kumalizia ujenzi msikiti mpya baada ya kuhamisha ule wa zamani," alisema Shehe Mnondwa.
Naye mmoja wa majeruhi hao aliyejitambulisha kwa jina la Issa Hussen alisema kuwa hii ni mara ya nne kutokea kwa vurugu katika msikiti huo, ambapo moja ya tukio kama hilo alisharipoti kwa Kituo cha Polisi Kilwa Road kwa jalada KLR/RB/5591/07 shambulio.
Baadhi wa wananchi walishuhudia tukio hilo walishangazwa na waumini hao kufikia hatua hiyo ya kutoana damu katika kipindi hiki cha mwezi wa Mtukufu wa Ramadhani, badala ya kumaliza tofauti zao kwa mazungumzo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Emmanuel Kandihabi alithibisha kutokea kwa tukio hilo, jana alisema upelelezi unaendelea kuwabaini waliosababisha vurugu na kuwajeruhi wenzao.
No comments:
Post a Comment