Uwezo wa kupunguza unene unao mwenyewe - 2
Katika matumizi ya vyakula kama tiba mbadala ya kupunguza unene, tulianza kwa kuelezea jinsi ya kupunguza unene kwa kutumia mchanganyiko wa asali na juisi ya limau kutwa nzima bila kula kitu kingine. Leo tunaendelea na matumizi ya vyakula vingine kama tiba mbadala:
KUPUNGUZA UNENE KWA KULA KABEJI
Mboga aina ya kabeji kila mtu anaifahamu, lakini kitu ambacho hakifahamiki na wengi ni zile faida na uwezo wake wa kutumika kama dawa ya kupunguza unene na katika hili, kabeji inaaminiki kuwa bora zaidi.
Utafiti wa hivi karibuni umebaini kwamba, kabeji ina kemikali muhimu sana inayojulikana kitaalam kwa jina la tartaric acid ambayo ina uwezo wa hudhibiti mbadiliko wa sukari na wanga kuwa mafuta mwilini. Hivyo ni muhimu sana kwa suala la kupunguza unene.
Njia bora ya kuitumia kabeji ili ikusaidie kupunguza unene, ni kutengeneza salad mbichi kwa wingi, kisha kula badala ya chakula kwa siku kadhaa, pia unaweza kuwa unakula kila unapokula chakula chako cha mchana, jioni au usiku. Hiyo itakuwa ndiyo njia pekee ya kukufanya uwe mwembamba siku zote.
KUPUNGUZA UNENE KWA KUTUMIA NYANYA
Nyanya nayo ni kiungo kingine cha mboga ambacho kina faida kubwa katika suala la kupunguza unene. Wengi wetu tunaitumia nyanya kama kiungo cha kuongezea ladha kwenye mchuzi na mboga zingine, lakini faida zake ni zaidi ya hizo.
Nyanya pia inaweza kutumika kama dawa ya kusaidia kupunguza unene. Ili kupata faida za nyanya katika suala hilo, chukua nyanya moja au mbili zilizoiva vizuri, zioshe ili kuondoa bakteria na uchafu mwingine, kisha kula kila siku asubuhi kabla hujanywa chai wala kitu kingine. Baada ya mwezi mmoja au miwili, kutegemeana na unene wako, utaona mafanikio mazuri.
DAYATI YA MTU MNENE INAPASWA KUZINGATIA YAFUATAYO:
Kula matunda na mboga kwa wingi na kupunguza ulaji wa vyakula vyenye kalori nyingi.
Kula nyanya asubuhi na kwenye saladi, fanya kuwa sehemu ya mlo wako kila siku.
Kula kabichi mbichi au ya kuchemshwa, kwani hudhibiti ule mfumo wa wanga na sukari kujibadilisha kuwa mafuta.
Penda kula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha Vitamin B.
Pendelea mafuta ya kupikia aina ya Vegetable badala ya Butter au Margarine.
Pendelea kula vyakula vya kuchemsha, kuoka au kuchoma badala ya kukaanga kwenye mafuta.
Kula kiasi kidogo cha vyakula vyenye chumvi, sukari, mafuta, bidhaa zitokanazo na ngo'mbe na pombe.
Kunywa maziwa aina ya Skim Milk au Low Fat Milk badala ya Full Cream Milk.
Oka, chemsha au choma nyama na samaki ili kuua mafuta yote kwenye nyama hiyo, usipende kukaanga kwa mafuta.
Epuka kula wali na viazi vitamu ambavyo vina kiwango kikubwa cha wanga. Nafaka nzuri kula ni pamoja na ngano.
Epuka kula vyakula vyenye kalori nyingi, kama vile chocolate, ice cream, pipi na vyakula vilivyotayarishwa. Usipende kula wakati ukiwa na msongo wa mawazo au hasira.
Usipende kula mkate uliotengenezwa kwa ngano peke yake, mkate uliotengenezwa kwa mchanganyiko wa nafaka, kama soya na uwele ni mzuri zaidi.
Usiache kula mchana, hakikisha unakula milo yote mitatu kama kawaida ikienda sambamba na milo mingine midogo katikati.
Kunywa maji mengi kwa siku, lita moja mpaka mbili, bila kukosa.
Kunywa glasi ya maji yaliyochemshwa kila siku baada kila mlo.
NJIA ZINGINE ZA KUPUNGUZA UNENE
Mazoezi ya mwili pamoja na ya pumzi, ambayo ni muhimu sana katika programu ya kupunguza unene. Mazoezi ya dakika 30 hadi saa moja asubuhi yana faida kubwa.
Mazoezi ya kutembea ni mazuri kwa kuanzia. Mazoezi mengine yanayofaa ni pamoja na kuogelea, kuendesha baiskeli nk.
MWISHO: Badili tabia ya ulaji kwa ujumla. Kula chakula kwa kutafuna kwa muda mrefu, angalau mara 50 kabla ya kukimeza ili unapokimeza kiwe katika mfumo wa majimaji. Utafunaji wa namna hii umewasaidia wengi sana katika kupunguza unene. Zingatia hayo na bila shaka utafikia lengo lako.
UAMUZI UKO MIKONONI MWAKO!
No comments:
Post a Comment