UWEZO WA KUPUNGUZA UNENE UNAO MWENYEWE!
Leo tunaiandika kwa mara nyingine makala kuhusu unene wa kupindukia (obesity). Hili ni tatizo sugu duniani ambalo linawakabili watu wengi, mbaya zaidi watu wengi hujikuta kwenye tatizo hili bila kujua chanzo na wanapojaribu kujiondoa kwenye tatizo, hukwama na kushindwa kuelewa nini cha kufanya.
UNENE NI NINI?
Kitaalamu, unene unaelezewa kama hali ya kimwili inayosababishwa na kuwepo kwa hifadhi kubwa ya mafuta mwilini (excessive fat storage). Aidha unene umeelezewa kama ni ule uzito zaidi ya asilimia 20 ya uzito wa mtu anaopaswa kuwa nao kutokana na umri na urefu alionao au kwa kitaalamu inajulikana kama Body Mass Index (tulishaonesha jeduari hili katika makala zilizopita).
Kuwepo kwa tishu zenye mafuta mwilini ni muhimu, kwani ndiyo hifadhi ya nishati ya mwili iliko, lakini kuwepo kwa mafuta mengi zaidi husababisha unene wa kupindukia na huwa chanzo cha magonjwa mengi. Mtu mnene sana yu hatarini kupata ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu (Hypertension) na ugonjwa wa moyo.
DALILI ZA UNENE
Unene husababisha ongezeko la saizi na seli za mafuta mwili mzima na hali hii husababisha mrundikano wa mafuta mwilini. Sehemu ya mwili ambayo unaweza kuuona mrundikano huu kirahisi ni kiunoni.
Kipimo cha kiuno cha inchi 40 au zaidi kwa wanaume na 35 au zaidi kwa wanawake ni unene wa kupindukia na mtu huyo yupo kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yanayohusiana na unene.
Ingawa unene hauna magonjwa mahsusi, lakini huchangia kwa kiasi kikubwa matatizo mengi ya kiafya kwa watu wazima, yakiwemo;
Shinikizo la juu la damu
Kisukari (Type 2)
Magonjwa ya kibofu
Saratani
Kolestro
Kiharusi
Matatizo ya kupumua na kulala,
Mfadhaiko
Magonjwa ya ngozi
Kukoroma n.k
NINI HUSABABISHA UNENE?
Unene unaweza kutokea kutokana na sababu mbalimbali, moja ikiwa ni kula sana ambako hakuendani na mahitaji ya mwili. Unapokula sana kuliko mahitaji ya mwili wako, nishati inayobaki huhifadhiwa kwenye seli za mwili kwa njia ya mafuta na sukari na hivyo kumnenepesha mtu.
Sababu nyingine zinaweza kuwa zile za kibaiolojia au za kurithi kutoka tumboni kwa mama, staili ya kuishi kwa kula bila kujishughulisha na kazi yoyote, mwili kushindwa kusaga chakula na kuna baadhi ya dawa za tiba huchangia unene.
Ili kuepuka unene, mtu anapaswa kujiepusha na orodha ya vitu ifuatayo ambayo ina uhusiano wa karibu na maisha yetu ya kila siku kwa sasa:
-Kutokufanya mazoezi au kuwa na maisha ya kupenda kukaa tu.
-Kupenda kula vyakula vyenye mafuta mengi na sukari nyingi.
-Kukosa usingizi
-Kuishi maisha yenye msongo mkubwa wa mawazo
-Kuepuka dawa zinazochangia kuongeza unene.
UNAWEZA KUPUNGUZA UNENE KWA VYAKULA
Baada ya kukueleza unene ni nini, sababu na madhara yake kiafya, pia tutakueleza jinsi ya kupunguza unene kwa kutumia vyakula mbalimbali kwa mpangilio ambao utakuwa ndiyo dawa ya tatizo lako, pamoja na kuzingatia kanuni za ulaji sahihi.
Awali ya yote, ili upunguze unene unatakiwa uzingatie kanuni moja kubwa; KULA KIDOGO, FANYA MAZOEZI AU KAZI NYINGI. Kamwe usifanye mazoezi au kazi nyingi halafu ukala kwa wingi, huwezi kupungua. Unapofanya mazoezi au kazi nyingi unachoma mafuta au 'calories' kwa wingi na unapokula kidogo unaingiza calories kidogo. Hivyo kiwango kinachotoka kinapokuwa kikubwa kuliko kinachoingia, ndipo mwili unapopungua.
JUISI YA LIMAU NA ASALI
Mbali ya kuzingatia kanuni hiyo, fanya funga ya kutwa nzima kwa kunywa juisi ya limau iliyochanganywa na asali pamoja na maji. Kwa aina hii ya tiba mbadala, chukua kijiko kimoja cha chai cha asali mbichi, changanya na juisi ya limau (kipande kimoja cha limau) kisha changanya kwenye glasi moja yenye maji ya uvuguvugu kisha kunywa kiasi hicho kwa vipindi tofauti mchana kutwa.
ITAENDELEA WIKI IJAYO KUCHAMBUA DAWA MBADALA NYINGINE…
No comments:
Post a Comment