Thursday, January 31, 2008

YOU ARE WHAT YOU EAT

MATATIZO YA KUTOONA VIZURI NA UHUSIANO NA LISHE

Wataalamu waliposema ‘ulivyo kunatokana na unavyokula’, hawakukosea, kwani kila kasoro ya kiafya tunayoweza kuwanayo, inatokana na lishe; ama kwa kula kisichohitajika au kwa kukukosa kula kinahohitajika.


Leo tutaangalia tatizo la kutoona vizuri (Defective Vision) na kuona ni jinsi gani mtu anaweza kukabiliana au kujiepusha nako, au kupunguza athari ya kupatwa na upofu kabisa kwa kuzingatia lishe sahihi.

TATIZO LIKOJE

Tatizo la kutooana vizuri huanza kwa mtu kutoona vizuri vitu vya mbali, kama vile mwanafunzi kutoweza kusoma ubaoni akiwa mbali, au kutoweza kuona vizuri kwenye televisheni au jumba la sinema na anapojaribu kuangalia wakati mwingine macho huuma na hutoa machozi. Wakati mwingine tatizo la kutooana huambatana na kuumwa kichwa.


KITU GANI HUSABABISHA TATIZO HILI

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, mambo makuu matatu ndiyo husababisha tatizo hili. Kwanza ni tatizo la uchovu wa akili, pili ulaji wa vyakula usio sahihi na tatu ni matatizo ya mishipa ya damu kushindwa kusambaza damu ipasavyo. Uchovu wa akili una uhusiano na uchovu wa misuli na mishipa ya macho.


Sababu zingine zinazosababisha matatizo ya macho ni kupenda kusoma maandishi mahali penye mwanga hafifu au kukodolea macho mwanga kwa karibu, kupenda kusoma maandishi kwenye vitu vinavyotembea kama vile mabasi au treni, kuangalia televisheni au filamu na kusoma kwa muda mrefu sana.

VITAMINI A KAMA TIBA YA MACHO

Ulaji wa vitamini A ni muhimu sana katika suala zima la kuimarisha uwezo wa macho kuona. Vyakula vinavyoaminika kama vyanzo vikuu vya vitamini A ni spinachi, nyanya, karoti, kabichi, mchicha, soya, machungwa, tende, maziwa mabichi, siagi, jibini na krimu ya maziwa. Iwapo utaamua kula vidonge vya Vitamini A, dozi inayoshauriwa kwa siku ni ujazo wa 25,000 IU.

LISHE INAYOSHAURIWA KWA MWENYE MATATIZO YA MACHO

Tatizo la kutoona vizuri linaweza kudhibitiwa au kuepukwa kwa kula vyakula sahihi. Mtu mwenye matatizo haya anashauriwa kula vyakula vya asili, hasa vile visivyo pikwa ambavyo ndivyo vinavyoaminika na uwezo hata wa kutibu tatizo hili kwa wepesi zaidi kwa kuwa na vitamini asili nyingi.


Mwenye tatizo hili anashauriwa kula machungwa kwa wingi, epo (apples), zabibu mbichi, mboga za majani za kijani kama mchicha, spinachi, kabichi, karoti, vitunguu, nyanya na bidhaa za maziwa, bila kusahau vitu kama karanga na matunda ya kukaushwa. Halikadhalika vyakula vitokanavyo na nafaka halisi (whole grains) kama mkate na ugali.


Katika suala
hilo la lishe, ni vyema pia kuvijua vyakula ambavyo havitamsaidia mgonjwa katika kukabiliana na tatizo hilo. Vyakula vya kuviepuka kuvila ni pamoja na chai, kahawa, nyama, mayai, mikate myeupe pamoja na ‘jamu’.


Vyakula vilivyotajwa hapo juu si vya kupenda kula kwa wingi, kwani hutibua na kuleta ‘usumbufu’ kwenye mfumo wa usagaji chakula kwa kuchangia au kuchelewa mtu kupata choo
kama inavyotakiwa, kwa maana hiyo vinapaswa kuepukwa.


SULUHISHO MBADALA

Aidha, unaweza kupata suluhisho la tatizo la macho kwa kufanya mazoezi maalumu ya macho, ambayo hufanywa kwa kukaa kwenye dawati au kiti asubuhi. Elekeza uso wako jua linakochomoza, fumba macho na anza kutembeza macho yako kushoto na kulia kwa kiasi cha dakika 10. Baada ya hapo fungua macho, pepesa kwa dakika 10 na angalia sehemu yoyote tulivu.

Mazoezi mengine ni yale ya kusimama ukiwa umetanua miguu, mikono umeishusha chini bila kushika kitu chochote. Simama mbele ya picha au kioo, kisha zunguruka mfano wa saa huku ukiangalia hiyo picha au kioo bila kupepesa macho kwa dakika kadhaa hadi utakapoona unachokiangalia nacho kikizunguruka upande mwingine. Fanya hivyo kila asubuhi na utaona mabadiliko fulani. Mazoezi hayo husaidia kurekebisha mfumo wa misuli na mishipa ya macho.

No comments: