Hot Corner ndiyo jina la uga huu, na katika pitapita zake ndani ya Jiji la Dar es Salaam, wiki iliyopita, mtaalamu wetu Catherine Kassally a.k.a Mamaa wa Nyeupe alikutana uso kwa uso na Msanii wa Jumba la Dhahabu, Angela John a.k.a Winter na kumpiga maswali haya,
Hot corner: Hivi unavyoonekana sista duu, umeolewa kweli?
Winter: Nimeolewa ndiyo.
HOT Corner: Aisee hongera sana, sasa katika hiyo ndoa yako, matarajio ni kuwa na watoto wangapi?
Winter: Nikijaliwa, napenda niwe mama wa watoto wawili.
Hot corner: Umeshawahi kunywa pombe? Ukishaweka ‘glasi’ kadhaa kichwani, kitu gani huwa unatamani kufanya?
Winter: Katika maisha yangu sijawahi kunywa pombe na wala sitakuja kuinywa kwani binafsi naona ni ibilisi mbaya.
Hot corner: Ni msanii gani wa maigizo au filamu unayemfagilia hapa Bongo?
Winter: Simfagilii msanii yeyote Bongo, labda Nigeria namzimia Jean Viv Nanje ile kinoma!
Hot corner: Unapendelea kuvaa mavazi gani
Winter: Sina mavazi maalum, kila kivazi nitakachokitinga na kunitoa kiheshima hapo tunakwenda kazi.
Hot corner: Ushawahi kutumia kondomu katika maisha yako?
Winter: Kondomu kwangu ni kama sala ya baba yetu, ukiingia kanisani ni lazima uikute. Vivyo hivyo, nikiingia katika mapenzi ni lazima niizingatie.
Mtukutu wa verse kutoka Kundi la Nako 2 Nako, Isaac a.k.a Lloydize, amesema kuwa ukiachana na uvumi wa mitaani kwamba yeye siku hizi haziungi kwa sana na mwanadada kiuno bila mfupa, Rehema Chalamila ‘Ray C’, mrembo huyo bado ni mshkaji wake wa karibu.
Lloydize, alimtonya mdau wetu Mariam Mndeme kuwa hakuna utofauti wowote uliopo kati yao na kwamba wanaendelea kushirikiana kisanii kama ‘kawa’.
“Wanaosema tumegombana ni wanafiki tu, mimi na Ray C bado ni damu damu, halafu ukizingatia tumegundua kwamba tabia zetu zinaendana, labda washkaji fulani wanaona wivu, nitajuaje?” alisema Lloydize.
Kabla ya kauli hiyo ya Lloydize, kuna uvumi ulishazagaa mitaani kuwa mshkaji huyo wa Nako 2 Nako amemwaga kiuno bila mfupa, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa mrembo huyo kwa sasa mshiko siyo kivile.
Kuna msemo wa Kiswazi kuwa ‘jasiri hasahau asili’, basi Miss Singida 2003, Manka Mushi ameamua kuuenzi kwa kubuni na kuandaa shindano la urembo, Fatma Amri anakujuza kiundani zaidi.
Manka ambaye kabla ya kushiriki Miss Singida, alishiriki Miss Mwanza na kuingia tatu bora, alisema, ameamua kuja kivyake kwa shindano hilo ambalo dhumuni lake ni kuwasaka warembo wawili wa Wilaya za Ilemela na Nyamagana, mkoani Mwanza.
Aliongeza: “Nimeandaa mashindano hayo ili kuwapa nafasi warembo wenye sifa kuitumikia jamii. Na taji hili, litakuwa tofauti na yale ya masindano mengine yaliyozoeleka.
Alifafanua kuwa mchuano huo utachukua nafasi kwenye mkesha wa Pasaka katika ukumbi ambao atautaja hapo baadaye, kisha akagusia kwamba warembo wanaowania taji hilo kwa sasa wanafanya mazoezi ya kutisha ndani ya Klabu ya City Cabana, jijini Mwanza.
Prodyuza wa muziki, anayesadikika ni namba moja kwa sasa, Akwabi Akili ‘Dunga’, amesema kuwa kumpa tano mwanamuziki Nakaaya Sumari kama ishara ya kumpongeza haitoshi, hivyo anamkandimiza 10 mwana wane, Violet Mushi anadondoka nayo ado ado.
Dunga, anayeratibu shughuli za kupitia Studio ya 41 Record, ya jijini Dar es Salaam, alisema wiki iliyopita kwamba uwezo wa Nakaaya upo juu ile mbaya, hivyo yeye binafsi anaona ujiko kupiga mzigo na mdada huyo. “Namtabiria atafanya makubwa zaidi katika ulimwengu huu wa muziki.
Nakaaya hajaingia kwenye fani kubahatisha, uwezo na kipaji chake ni adimu kabisa,” alisema Dunga ambaye anasifika kwa kupika mapini yasiyo na kasoro za kiufundi.
Nakaaya kwa sasa anatamba na wimbo wake Mr. Politician.
No comments:
Post a Comment