Tuesday, February 5, 2008

YOU ARE WHAT YOU EAT!




UWEZO WA NANASI KUWA KINGA NA TIBA
Msimu wa nanasi umeshawadia katika ukanda wote wa pwani. Katika msimu huu bei ya nanasi hushuka na kuwa katika bei ambayo mtu yeyote anaweza kuimudu bila shaka. Hivyo asiyekula mananasi ya kutosha mpaka msimu unaisha, huyo ana hasara kubwa katika afya yake. Ukiacha ukweli huo, tunda hili lina faida ambazo linashawishi kila mtu kulitumia.

Faida zinazoweza kupatikana kwenye nanasi ni nyingi ambazo zinaweza kuwa kama kinga na tiba kwa baadhi ya matatizo ya kiafya ambayo pengine yangehitaji mtu kwenda hospitali kupatiwa dawa, tena kwa gharama kubwa. Miongoni mwa faida hizo ni hizi zifuatazo:

USAGAJI WA CHAKULA
Nanasi lina virutubisho vinavyouwezesha mfumo wa usagaji chakula tumboni kufanya kazi yake ipasavyo, pindi mfumo huu unapowezeshwa kufanyakazi yake vizuri, mtu huweza kupata choo laini na kwa wakati kama inavyotakiwa. Hivyo wenye kula tunda hili kwa wingi hawawezi kusumbuliwa na tatizo la ukosefu wa choo. Aidha kwa mujibu wa tafiti nyingine, nanasi pia lina virutubisho vyenye uwezo wa kupunguza au kuzuia uvimbe tumboni.

KINGA YA MWILI
Nanasi linaaminika kuwa miongoni mwa matunda yenye chanzo kizuri cha vitamin C ambayo kazi yake mwilini ni kuupa mwili kinga dhidi ya ‘wavamizi’ mbalimbali (freee radicals), ambao wanapoingia mwilini, kazi yao huwa ni kuharibu chembembe hai za mwili. Vile vile ‘wavamizi’ hao wanapoweka makazi mwilini, huziba mishipa ya damu na hivyo kusababisha magonjwa ya moyo na mengine mengi, ikiwemo kansa ya tumbo.

Kwa kuongezea, vitamini C inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili, hivyo kuifanya kuwa kinga ya magonjwa madogo madogo kama vile mafua, kikohozi, homa na maambukizi mengine. Unapokuwa na kiwango cha kutosha cha vitamini hiyo, bila shaka kinga yako ya mwili itakuwa imeimarika na hivyo utakuwa umejiepusha na maambukizi mbalimbali.

CHANZO CHA MADINI
Mbali ya kuwa ni chanzo kizuri cha vitamin C, nanasi pia ni chanzo kizuri cha madini aina ya ‘manganese’ ambayo yanaaminika kuwa na uwezo wa kuboresha ufanisi wa vimeng’enyo mbalimbali vya mwili, vikiwemo vya kuzalisha nishati na kinga ya mwili. Halikadhalika tunda hili lina kiwango cha kutosha cha vitamin B1 (thiamin).

KUIMARISHA NURU YA MACHO
Inawezekana karoti ikawa ndiyo inayojulikana na watu wengi kuwa na uwezo wa kuimarisha nuru ya macho, lakini nanasi nalo lina uwezo mkubwa wa kuimarisha nuru ya macho. Utafiti unaonesha kuwa ulaji wa tunda hili na matunda mengine, kiasi cha milo mitatu kwa siku, kunaoindoa hatari ya kupungua kwa nuru ya macho kwa asilimia 36 kwa watu wazima.

NANASI LILILO BORA
Nanasi lililo bora ni lile kubwa na lililoiva vizuri. Wakati ni kweli kwamba nanasi kubwa lina nyama nyingi kuliko nanasi dogo, lakini hakuna tofauti ya ubora wa virutubisho kati ya nanasi dogo na kubwa, il mradi lisiwe limeoza au lenye michubuko mingi. Hivyo chagua nanasi lilioiva vizuri na lenye kunukia.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chuo Kikuu cha Innsbruck, nchini Austria, unasema kuwa tunda linapokuwa limeiva zaidi ndivyo ambavyo virutubisho vyake vinapokuwa bora. Kwa kula nanasi ambalo halijaiva vizuri, huenda ukajikosesha faida zinazopatikana kwenye tunda hilo kama inavyoelezwa.

Mara baada ya nanasi kumenywa na kukatwa vipande, linatakiwa kuliwa mara moja, iwapo litahifadhiwa kwenye jokofu kwa ajili ya kuliwa baadae, njia sahihi ya kuhifadhi ni kuliweka kwenye chombo chenye mfuniko (container) ili kuhifadhi virutubisho vyake kwa kipindi hadi cha siku tano bila kupoteza ubora wake, ikiwa pamoja na ladha.

Mwisho, unapokula tunda lolote, zingatia usafi. Osha tunda hadi litakate, nawa mikono yako kwa sabuni au maji moto kisha shika tunda lako, vinginevyo unaweza kujikuta unakula tunda na vijidudu vya maradhi ya kuharisha na hata Kipindupindu.

1 comment:

Anonymous said...

Best article, educational and helps.
Waiting for more educational article like this.
Nabila Ibrahim