Thursday, February 7, 2008

RICHMOND:….’Usanii’ ulikuwa hivi

HAKUNA hapa nchini wala Marekani, kampuni iliyosajiliwa kwa jina la Richmond Development Company LLC. Bunge lilielezwa jana.


Mwenyekiti wa kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza mchakato wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura ulioipa ushindi kampuni hiyo, Dk, Harrison Mwakyembe alibainisha hayo bungeni mjini Dodoma jana.


Akiwasilisha muhtasari wa taarifa ya kamati hiyo, Dk. Mwakyembe alisema uchunguzi umeonyesha hakuna kampuni yenye jina hilo iliyosajiliwa katika jimbo la Texas nchini Marekani wakati wa kusaini mkataba huo.


“Kamati teule imejiridhisha kuwa hakuna kampuni yenye jina la Richmond Development Company LLC iliyokuwa imesajiliwa JImbo la Texas wakati wa kusaini mkataba huo hadi tunapowasilisha ripoti hii…” alisema.


Alisema hitimisho lilifikiwa na kamati hiyo, linashabihiana kwa vigezo na ushauri wa kitaalamu uliotolewa na kampuni mashuhuri ya mawakili wa Virginia, Marekani inayoitwa Hunton & Williams LLP kwa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Oktoba mwaka juzi “katika ripoti yake yenye kurasa 10, kampuni hiyo ya mawakili imetamka bayana kuwa hakuna kampuni yenye jina la Richmond Development.

Company LLC kwenye masijala ya katibu wa Jimbo la Texas ambaye moja ya majukumu yake ni sawa na ya Msajili wa kampuni Tanzania.


Dk. Mwakyembe alisema, Humton & Williams LLP wameituhumu Richmond Development Company LLC kwa upotoshaji wa hadhi yake kikampuni na kutoa tamko lisilo sahihi kuhusu hadhi yake chini ya sheria za Texas.


Alisema ukaguzi wa kumbukumbu za katibu wa jimbo la Texas uliofanywa na kampuni hiyo Oktoba 2006 ulionyesha hakuna kampuni yenye jina la Richmond Development Company LLC iliyokuwa imeanzishwa na kuendesha shughuli zake jimboni humo.


Dk. Mwakyembe alisema wajumbe wa kamati hiyo, waliokwenda Marekani Desemba 10 hadi 16 mwaka jana, waliambiwa na Mohamed Gire, kuwa Richmond Development Company LLC ni jina mbadala la biashara la kampuni yake iitwayo RDEVCO LLC.


“Bwana Gire ambaye aliamua mkutano wake na wajumbe wa kamati Teule ufanyike ofisini kwa wanasheria wake, Duane Morris LLP waliopo 3200 Southwest Freeway, suite 3150, jijini Houston, alisisitiza kuwa sheria na Texas zinawaruhusu wafanyabiashara na kampuni kutumia majina mbadala au tofauti na yale yaliyopo kisheria kwa sababu za kibiashara alisema Dk. Mwakyembe.


Alisema kamati yake iliyazingatia maelezo ya Gire kwa ajili ya kuyafanyia kazi, kwa sababu kuna, majimbo mengi Marekani, likiwemo la Texas yanaruhusu matumizi ya majina mbadala katika biashara au huduma.


Lakini, Dk. Mwakyembe alisema, sheria zinaweka taratibu za kuzingatia ili kuepusha vitendo vya kitapeli katika matumizi ya majina mbadala ya kibiashara.


“Katika jimbo la Texas ambako Gire anaishi ni kosa la jinai kutumia jina mbadala bila kulisajili. Usajili wa jina mbadala unadumu kwa miaka mitano ambapo mtumiaji lazima asajili jina hilo upya kati ya januari mosi na Desemba 31 ya mwaka wa tano,” alifafanua Dk. Mwakyembe ambaye pia ni mbunge wa Kyela.


Alisema, Gire aliwakabidhi wajumbe wa Kamati hiyo hati ya uthibitisho ya Harris County, Texas ambayo kwa maoni yake, ilikuwa inathibitisha kuwa Richmond Devilopment Company LLC ni jina mbadala la biashara.


“Kamati Teule imeikagua hati hiyo kwa kina na kuona kuwa badala ya kumsaidia Gire, inazidi kuthibitisha kuwa si mfanyabiashara mwadilifu ila tapeli kwa sababu kuu mbili:

Mosi, mbali na kwamba hati hiyo ya Gire ni kivuli tu au nakala ya “hati” halisi (kama ipo), nakala ambayo haina uthibitisho wowote wa uhalali na uhalisia wake, ilikuwa ina saini ya ofisa mmoja mbadala ya wawili walioainishwa katika hati hiyo pili, badala ya hati hiyo kutamka kuwa RDEVOCO LLC imesajili jina la Richmond Development Company LLC kama Gire alivyotaka Kamati Teule ielewe, hadithi mpya kabisa inaanzishwa kuwa Richmond Development Company ni jina mbadala lililosajiliwa na Richmond Development Company LLC! La kushangaza ni kuwa katika baadhi ya barua zake alizoiandikia TANESCO na wizara ya Nishati na Madini, Gire anatamka kuwa Richmond


Development Company ni jina mbadala la biashara la RDEVCO LLC.


“Mtu anaweza akadanganyika akifikiri kuwa kiwango hiki cha ubabaishaji hakithibitishi utapeli pekee, bali vilevile elimu duni ya mmiliki wa kampuni hizo, Gire, inayomfanya asione hatari kubwa anayojitwalia ya hata kumfikisha jela kwa udanganyifu,” alisema Mwakyembe, Kwa mfanyabisahara mzoefu aliyejizungushia mawakili wa kumtetea mambo yakimwendea mrama, anajua analolifanya, hivyo Richmond Development Company LLC ni kampuni ya kimakusudi ya kimkakati ambayo haikamatiki, haishitakiki, haipigiki faini na haiadhibiki kwa lolote lile itakalolifanya kwani haina uhai wa kikampuni,” alisema.

Dk. Mwakyembe alisema, Richmond Development Company LLC, kwa maneno mengine, si kampuni ya mchana bali ya usiku, kampuni ya mfukoni ambayo shirika la umma TANESCO liliingia nalo mkataba wa mabilioni ya fedha ya walipa kodi wa Tanzania.

No comments: