Tuesday, May 20, 2008

HATUKUUMWA ILI TUUGUWE -2

You Are What You Eat!
Wiki iliyopita tulianza makala haya kuhusu ukweli kwamba binadamu ameumbwa ili aishi bila kuandamwa na maradhi. Tunaelezwa kwamba kuugua, ugonjwa wowote, huwa kunatokana na kukiuka kwa sheria za mwili (physical laws) zilizowekwa na Mungu mwenyewe….endelea..

UTAKAPOUGUA UFANYE NINI?

Naweza kusema kuwa tatizo kubwa tulilonalo ambalo linatusumbua ni kutokujua jinsi ya kutibu miili yetu pale tunapougua. Katika suala la ugonjwa, kabla ya kupata tiba, chanzo cha ugonjwa lazima kieleweke. Mazingira machafu yabadilishwe, ulaji usio sahihi uachwe kisha mwili usadiwe kujisafisha wenyewe kwa kuondoa sumu mwilini kwa kutumia dawa zisizo na madhara zikisaidiwa kwa kiasi kikubwa na vyakula sahihi.

Unapopatwa na ugonjwa, ikiwa ni matokeo ya ukiukwaji wa zile kanuni za mwili, swali la kwanza kujiuliza ni nini kimesababisha ugonjwa huo, kwa sababu hakuna ugonjwa usiokuwa na chanzo. Jiulize; ‘nimefanya nini mpaka nimeugua’? Mwanzoni swali hilo linaweza kuwa gumu na usipate jibu, lakini ukizoea na ukiwa makini na vitu unavyokula kila siku, jibu hupatikana kirahisi.

Baada ya kujua nini kimesababisha ugonjwa wako, ondoa sababau hiyo na acha kula au kufanya jambo hilo kisha anza kujitibu kwa kutumia dawa asilia ambazo zitakusaidia kuondoa sumu iliyoko mwilini na bila kukuletea madhara mengine. Jambo la kuzingatia hapa ni kuepuka matumizi ya dawa zisizo sahihi kutibu ugonjwa ulionao, kwani badala ya kutibu unaweza kuwa unajiongezea maradhi mengine zaidi.

Baada ya kuelezea kwa kirefu kanuni za mwili, tuangalie vitu muhimu vitatu anavyopaswa kuvitumia binadamu kila siku kutokana na umuhimu wake katika kufikia lengo la kuwa na afya bora:

1. MAJI

Sumu hurundikana mwilini tunapokuwa hatuna maji ya kutosha. Mtoto mchanga aliyezaliwa leo, asilimia 80 ya mwili wake huwa maji. Kiwango cha maji kwenye tishu hupungua kadri mwili unavyoongezeka hadi kufikia asilimia 60 kwa mtu mzima.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, binadamu aneweza kuishi hadi siku 81 bila kula, lakini hufa anapokosa maji kwa muda wa siku 5 tu! Mtu anapopoteza asilimia 5 ya maji mwilini, hubadilika na hueza kuanza kuweweseka, misuli kushikana na kukosa mwelekeo na akipoteza maji kwa asilimia hadi 15 maisha yake huwa hatarini na kupoteza maji kwa zaidi ya asilimia 15 mtu huweza kufa!

Katika suala hili la maji, naomba nisherehesha vya kutosha, kwani ni jambo muhimu na nyeti sana ambalo watu wengi hulipuuza na hawajui kuwa ndiyo chanzo cha matatizo mengi ya kiafya. Kwa kawaida mwili huwa hauweki akiba ya maji, hivyo huhitaji maji wakati wote na yanapokosekana athari zake huonekana upesi.

Watu wengi wamezoea kunywa maji pale wanaposikia kiu, hawana utaratibu wa kunywa kiwango cha maji kinachopendekezwa na wataalam wa afya cha lita moja na nusu hadi tatu kila siku. Unapofikia hatua ya kusikia kiu ni dadlili kwamba tayari mwili wako umepungukiwa maji. Mwili wa binadamu ni sawa na gari ambalo likiishiwa maji huweza kusababisha injini kufa!

Ili kujua umuhimu wa maji, unapaswa kuzijua dalili zinazojitokeza mwili unapopungukiwa maji. Sehemu za mwanzo kuathirika na upungufu huo ni zile zisizokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mzunguruko wa mishipa (Vascular circulation) kama vile magoti, viongio vya vidole na uti wa mgongo.

Maumivu yanayojitokeza sehemu hizo, ambayo huja na kuondoka, huwa ni matokeo ya mwili kuwa na upungufu sugu wa maji. Unapokabiliwa na hali kama hiyo, wazo la kwanza kukuingia akilini liwe “mwili wangu una tatizo sugu la maji”.

Kwa bahati mbaya sana, watu wanaokabiliwa na matatizo kama hayo katika hatua za awali huzipuuzia, ama kwa kutokujua au kwa kutojali, badala yake hukumbilia hospitali ambako huandikiwa dawa za kupunguza maumivu na kuacha tatizo la msingi likiendelea kujiiimarisha mwilini na hatimaye kuharibu mifupa ya sehemu hizo.

Kwa majibu wa Dk. Fereydoon Batmanghelidj, upungufu wa maji mwilini unaweza kusababisha maradhi mengine na kukauka kwa midomo siyo dalili pekee za kuishiwa maji mwilini, mtu kusubiri mpaka usikie kiu ndiyo unywe maji si sahihi.

Maumivu ya ndani ya viungo mara nyingi huwa ni kilio cha mwili ukiomba maji, mwili hujaribu kukufikishia ujumbe kuwa “nimeishiwa maji” na hupaswi kusikia kiu ndiyo unywe maji, bali kiu inapaswa kuzuiwa isitokee. Mwili unapokuwa haupokei maji ya kutosha lazima utasikia maumivu ya viungo.

“Maumivu ya mwili, ambayo hayawezi kuelezewa na mgonjwa kama yanatokana na kuumia au maambukizo ya ugonjwa, yaelezwe kama ni upungufu wa maji katika sehemu zenye maumivu, hivyo si vyeme mgonjwa kupewa dawa ambazo zitafanya tatizo kukua,” anaeleza zaidi Dk. Batmanghelidj.
ITAENDELEA WIKI IJAYO

No comments: