Thursday, May 8, 2008

IJUMAA SHOWBIZ!

Celtel Idols: Hii ndiyo Top 24
Hatimaye lile shindano la kumsaka kijana mwenye kipaji cha kuimba, maarufu kama Celtel Pop Idols limefanikiwa kuwapata wakali 24 (Top 24), Julius Kihampa anaanguka nayo.

Washiriki hao ambao walichaguliwa na majaji Angela Angwenyi, TK Siyandi na Scar, walipatikana juzi kupitia mchujo mkali uliofanyika nchini Kenya ambapo kati yao 19 ni wasichana na wavulana 5.

Waliotajwa kuingia Top 24 na nchi zao kwenye mabano ni pamoja na Adiona Maboreke (Zimbabwe), Alice Chinyimbe (Zambia), Alice Kalufyanya (Zambia), Ammara Brown (Zimbabwe), Chibwe Chapenuka (Zambia), Christine Apondiadda (Kenya), Cynthia Kuto (Kenya), Deborah Chansa (Zambia), Doris Onyango (Kenya), Eric Moyo (Zimbabwe), Faycal Birikunzira (Uganda) na Irenne Njunguna (Kenya).

Wengine ni Katungulu Mwenda (Kenya), Meeghan Galloway (Zimbabwe), Mkhululi Bhebhe (Zimbabwe), Mukuni Mulundika (Zambia), Nicollette Kiige (Uganda), Penjani Ng’uni (Zambia), Priscillah Mmbone (Kenya), Ruvimbo Mukorombindo (Zimbabwe), Samantha Mogwe (Botswana), Samantha Tirivacho (Zimbabwe), Samukeliso Eneya (Zimbabwe) na Trinah Chisanga (Zambia).

Bado zoezi linaendelea ili kumuwezesha mshiriki unayehisi anastahili kuwa mshindi unatakiwa umpigie kura kwa kuandika jina lake kisha unatuma kwenda namba 15727, mitandao inayotumika ni Celtel, Tigo na Vodacom.
Keisha azungumzia mauaji ya Maalbino
Msanii Khadija Shaban ‘Keisha’ amesema na safu hii kwamba amesikitishwa na uvumi ulionea mitaani kuwa, jamii ya Maalbino huuawa na baadhi ya watu kwa imani za kishirikina, Violet Mushi alicheki naye.

Akipiga stori zaidi muda mchache kabla ya kupanda basi kulelekea masomoni nchini Uganda mwanzoni mwa wiki hii, msanii huyo mwenye uwezo mkubwa wa kuimba alisema kuwa, kitendo hicho kinamuuma na kumchanganya sana, kitu kinachoweza kusababisha asifanye vizuri katika masomo yake.

“Naiomba jamii ielewe kwamba, sisi ni binadamu kama wengine, isitutenge au kudhani kuwa sisi tunatumika katika vitendo vya kishirikina, huu ni uonevu, itafikia kipindi nitalazimika kujificha kutokana na kuogopa hali hii. Pia naiomba serikali ilivalie njuga suala hili,” alisema Keisha.

Ishu ya 50 cent kuporwa cheni: Kina ‘Tatiana’ waitia aibu Afrika
Shabiki wa muziki wa Hip Hop aliyekwapua cheni ya msanii, Curtis Jackson ‘50 Cent’ alipokuwa kwenye shoo nchini Angola, anapotokea mshindi wa tatu wa shindano la BBA 2007, Tatiana amelitia aibu bara zima la Afrika.

Uchunguzi uliofanywa na ShowBiz kwa msaada wa mtandao wa internet, umebaini kwamba ishu hiyo imesambaa karibu ulimwengu mzima kupitia mitandao kadhaa, ikieleza kwamba “shabiki wa afrika ampora 50 Cent Cheni”.

Kutokana na ishu hiyo kuwa ‘hoti’ karibu ulimwengu mzima ambako mashabiki wa mwanamuziki huyo wameenea, imeifanya Afrika, hasa nchi ya Angola anakotokea Tatiana kuonekana kuwa na baadhi ya watu wenye tabia mbaya kama hizo, kitu ambacho ni cha aibu.

Safu hii inalaani vikali matukio kama hayo ya ajabu ambayo yanaweza kuishushia nchi heshima hasa kwa wageni ambao kwetu ni kama watalii ambao wanatakiwa wapeleke ujumbe mzuri wanakotoka. Pia inatoa Big Up kwa Wabongo ambao walijiachia na 50 Cent pamoja na kundi zima la G-Unit bila matatizo yotote.
General Deffao akidondoka Bongo, kutupwa Segerea?
Baada ya bendi ya muziki wa dansi, Akudo Impact ‘Vijana wa Masauti’ au ‘masauti ya ukweli’ kutangaza kumleta Bozi Boziana ‘Mzee Benz’ siku ya utambulisho wa albamu yao ya kwanza, ‘Impact’, FM Academia nao wameahidi kumleta General Defao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo siku hiyo, Richard Bukos anadondoka nayo.
Baadhi ya wadau wa muziki wa dansi nchini, waliopata nafasi ya kupiga stori na safu hii walisema kuwa, kitendo cha ‘Wazee wa Ngwasuma’ kutangaza kumleta Defao siku hiyo ya uzinduzi wa Akudo ni kutaka kuwavurugia, kitendo ambacho wamekiita si cha kiungwana.

“Kwanza Defao mwenyewe akifika nchini anaweza kupata matatizo ya kutupwa gerezani, mimi ninavyokumbuka jamaa alipokuja Bongo mara ya mwisho aliondoka na deni alilokuwa akidaiwa katika Hoteli ya Sea Cliff ambako alifikia, kwa hiyo inabidi jamaa wawe makini,” alisema mdau mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

Mdau huyo pia alitamka kwamba, wengine wanaomsubiri mwanamuziki huyo kwa hamu ni uongozi wa Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam ambayo anadaiwa kutibiwa na kuacha deni kabla ya kuondoka kurudi kwao.

Katika kujiandaa na uzinduzi huo, ‘Vijana wa Masauti’ wamejichimbia kambini Mkoani Lindi, ndani ya Hoteli ya Lindi Ocean wakijifua. Mbali na Mzee Benz, wapenzi wa rusharoho watarindimishwa na kundi la Jahazi Modern Taarab.

No comments: