Tuesday, June 10, 2008

GAUTI: UGONJWA UNAOWEZA KUDHIBITIWA KWA MATUNDA, MBOGA


You Are What You Eat!
Gauti (Gout) ni miongoni mwa magonjwa sugu yanayowasumbua watu wengi hivi sasa. Ugonjwa huu ambao kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, unajulikana pia kama Jongo, zamani uliitwa ‘ugonjwa wa kitajiri’, huwapata watu wazima zaidi na baadhi ya akina mama wanaofikia ukomo wa kipindi chao cha hedhi (menopause).

Gauti ni ugonjwa unaoleta maumivu katika baadhi ya viungo vya mwili, kikiwemo kidole gumba ambacho huvimba na kusababisha maumivu makali kwa mgonjwa. Kuvimba kwa kidole hicho husababisha maumivu sehemu nyingine za mwili za maungio, kama vile magoti, maungio ya viganja, n.k.

Maumivu ya Gauti mara nyingi hujitokeza usiku wa manane au asubuhi mapema mgonjwa anapoamka ghafla na maumivu yake huweza kuendelea kwa kiasi cha wiki moja au zaidi. Katika kipindi hiki, mgonjwa hupatwa na homa na huwa hana hamu ya kula.

NINI HUSABABISHA GAUTI
Inaelezwa na wataalamu wetu kuwa mtu hupatwa na ugonjwa huu pale chembechembe za asidi ya kwenye mkojo (Uric Acid) zinaporundikana kwenye maungio ya viungo, ngozi na kwenye figo. Asidi hii hujizalisha mwilini katika mchakato wa kawaida wa kimwili na hutolewa nje ya mwili kwa njia ya mkojo.

Watu wanaosumbuliwa na ugonjwa huu, damu yao huwa na kiwango kikubwa cha ‘uric acid’ ambacho hakikuweza kujichanganya chenyewe kwenye damu ama kutolewa nje kwa njia ya kawaida ya mkojo.

Sababu nyingine zinazosababisha mtu kupata Gauti ni pombe, ulaji wa mara kwa mara wa vyakula vyenye protini nyingi kama vile nyama, ulaji wa vyakula vyenye wanga kwa wingi, ukosefu wa mazoezi, kuwa na mfadhaiko wa akili (stress) na kurithi ugonjwa.

VYAKULA VIFUATAVYO VINAWEZA KUDHIBITI UGONJWA HUU:
Juisi za mboga na matunda
Mboga zina nafasi kubwa sana katika kupambana na maradhi yanayomkabili mwanadamu na huwa ndiyo kinga ya mwili wakati wote zinapotumiwa. Katika kutibu tatizo la Gauti, juisi ya mchanganyiko wa karoti, tango na Kiazisukari (Carrot, Cucumber & Beet) huweza kusaidia sana.

Tengeneza juisi ya tango na kiazisukari ya ujazo wa mililita 100 kila moja, kisha tengeneza juisi ya karoti ya ujazo wa mililita 300, halafu changanya juisi zote tatu ili upate mililita 500 (lita moja) ya juisi yeye mchanganyiko wa mboga hizo tatu na unywe kiasi kila siku.

Kwa upande wa matunda yanayoweza kukupa ahueni na kinga dhidi ya ugonjwa huu ni pamoja na maepo (apple). Tunda hili linajulikana kwa ubora wake katika kutibu Gauti kutokana na kuwa ‘malic acid’ ambayo ina uwezo wa kuiyeyusha ‘uric acid’ inayoleta madhara mwilini. Ili kupata faida ya tunda hili, mgonjwa anashauriwa kula epo moja kila baada ya mlo wake wa kila siku.

Ukiacha epo, ndizi nayo imo katika orodha ya matunda yanayoleta ahueni kwa wagonjwa wa Gauti. Dayati ya kula ndizi pekee kwa muda wa siku tatu ama nne, itaweza kumpa ahueni mgonjwa. Ili kupata ahueni kwa kutumia ndizi mbivu, mgonjwa anashauriwa kula ndizi pekee kati ya nane na tisa kila siku kwa siku hizo zilizotajwa hapo juu, na asile tunda lingine.

Limau nalo lina faida kubwa kwa wagonjwa wa Gauti. Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi, Vitamin C, ambayo inapatikana kwa wingi kwenye limau, ina uwezo wa kukinga na kutibu maumivu ya viungo kwa kuimarisha tishu za mwili. ‘Citric Acid’ iliyomo kwenye limau, ina uwezo wa kuyeyusha ‘Uric Acid’ ambayo ndiyo chanzo cha tatizo. Ili kutumia limau kama dawa, kamua nusu limau kwenye glasi na kunywa mara mbili kwa siku.

DAYATI YA MGONJWA WA GAUTI
Ukishajijua kwamba una Gauti, unashauriwa kuzingatia sana vitu unavyopaswa kula na vile ambavyo hupaswi kula. Kwa wagonjwa wenye hali mbaya, wanashauriwa kufanya funga ya kunywa juisi ya machungwa na maji tu kwa siku tatu ama nne, hii ina maana kwamba katika siku hizo, kitu pekee utakachokula kutwa nzima ni juisi ama maji tu.

Baada ya funga hiyo, utaona nafuu kwenye tatizo lako na unashauriwa kufanya funga nyingine ya kula matunda pekee kwa siku tatu ama nne mfululizo. Baada ya hapo, mgonjwa anashauriwa kupendelea kula vyakula vya asili huku akitilia mkazo matunda na mboga mboga.

Epuka ulaji wa nyama, mayai, samaki, chai, kahawa, sukari, vyakula vitokanavyo na unga mweupe (ukiwemo mkate mweupe), vyakula vya kwenye makopo na vya kukaanga.

Mwisho, mgonjwa anashauriwa kukaa sehemu za wazi ili kupata hewa safi na afanye mazoezi ya viungo mara kwa mara na kuacha kuwaza ili kuepuka mfadhaiko wa akili ambao tumeona kuwa unachangia ugonjwa huu.

No comments: