Thursday, August 28, 2008

Zain yatangaza shule 19 zitakazopewa vitabu

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Bw. Samwel Kamote akibonyeza kompyuta wakati wa bahati nasibu ya kampuni ya simu za mkononi ya Zain kuchagua na kutangaza majina ya shule 19 kutoka mikoa mbalimbali Tanzania zitakazopokea vitabu vinavyotolewa katika programu ya Zain ya Build Our Nation (BON) jijini Mwanza, juzi. (Picha ya Zain Tanzania)
**************************************

ZAIN, kampuni ya simu za mkononi yenye mtandao katika nchi 22 barani Afrika na Mashariki ya Kati, imetangaza majina ya shule 19 kutoka mikoa mbalimbali Tanzania
zitakazopokea vitabu vinavyotolewa katika programu ya Zain ya Build Our Nation (BON) kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu nchini.

Shule hizo zilichaguliwa juzi (Jumatano Agosti 27, 2008) jijini Mwanza katika bahati nasibu iliyofanyika hoteli ya La Cairo ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Bw. Samwel Kamote kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. James Msekela na kuhudhuriwa pia na walimu na wanafunzi kutoka shule kadhaa za Mwanza.

Shule zilizochaguliwa na mikoa zinakotoka katika mabano ni Shule ya Sekondari Muyama (Kigoma), Shule ya Sekondari Mangio (Kilimanjaro), Shule ya Sekondari Mtama (Lindi), Shule ya Sekondari Quameyu (Manyara), Shule ya Sekondari Ndagala (Tabora), Shule ya Sekondari Shelui (Singida) na Shule ya Sekondari Maswa Girls (Shinyanga).

Nyingine ni Arusha Day (Arusha), Shule ya Sekondari Mongo (Dodoma), Shule ya Sekondari Mlolo (Iringa), Shule ya Sekondari Rwambaizi (Kagera), Shule ya Sekondari Semkiwa (Tanga), Shule ya Sekondari Nyandunga (Mara), Shule ya Sekondari Consolata (Mbeya), Ngerengere Day (Morogoro), Shule ya Sekondari Mwanu (Mtwara), Shule ya Sekondari Busolwa (Mwanza), Shule ya Sekondari Bagamoyo (Pwani) na Shule ya Sekondari Mpui (Rukwa).

Meneja wa Zain Kanda ya Ziwa, Bw. Ali Maswanya alisema bahati nasibu ya shule saba kutoka mikoa mingine iliyosalia itafanyika na kutangazwa wiki ijayo.

Build Our Nation ni programu ya Zain Tanzania yenye lengo la kusaidia na
kuwajibika kwa jamii ambayo imekuwa ikichangia vitabu kwenye shule za sekondari kwa mikoa yote 26 ya Tanzania, ili kuhakikisha kiwango cha elimu kinaongezeka Tanzania.

Bw. Maswanya alisema Zain imedhamiria kusaidia jamii na itaendelea kufanya hivyo ikiamini mchango huo katika sekta hii utasaidia kukuza kiwango cha elimu Tanzania na kuboresha maisha ya wanafunzi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Samwel Kamote aliipongeza Zain Tanzania kwa mchango huo na huduma inazotoa kwa jamii, hususan sekta ya elimu.

“Elimu bora ndio msingi wa familia na taifa imara na Serikali pia inaamini mchango wa Zain katika sekta hii muhimu utasaidia kukuza kiwango cha elimu Tanzania na kuboresha maisha ya wanafunzi wetu na kusaidia kuimarisha uchumi wetu, asanteni Zain kwa mchango huu,” alisema.

Zain Tanzania ilizindua programu ya ‘Build Our Nation’ Mei 10, 2004 na programu
hiyo inadhihirisha uwajibikaji wa kampuni hiyo katika kusaidia kuinua elimu nchini.

Mradi huo umegawanywa katika awamu kadhaa ambapo ya kwanza, shule moja
kutoka kila mkoa inachaguliwa katika bahati nasibu inayoendeshwa kwa kompyuta ili
kupata vitabu vyenye thamani ya sh. milioni 1. Hii inaiwezesha Zain kuepuka uteuzi
wa upendeleo kwa shule husika, na kutoa kipaumbele kwa shule zote.

Katika kila awamu, shule 26 zinachaguliwa kutoka mikoa yote Tanzania. Baada ya
kuchaguliwa, Zain inapata orodha ya vitabu vinavyohitajika zaidi katika kila shule, na
inachukua jukumu la kununua na kuvikabidhi.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu 2008, Zain itakuwa imetumia zaidi ya sh
milioni 500 katika kutekeleza programu hiyo na zaidi ya shule za sekondari 520
zitanufaika kutokana na mradi huo.

Katika mradi wa BON, pia Zain inatoa ofa ya kuwasomesha wanafunzi wanane bora
wa kike na kiume wanaopata ruhusa kutoka vyuo vikuu nchini. Kufikia mwishoni
mwa mwaka 2008, Zain itakuwa inasomesha wanafunzi 31 katika programu hiyo.

No comments: