Wednesday, May 13, 2009

Maalum kwa wagonjwa wa Kisukari


KWA kuwa ugonjwa wa Kisukari unatokana na upungufu wa virutubisho fulani mwilini, kuna miongozo imetolewa ya ulaji vyakula ambavyo vikifuatwa kwa ukamilifu huweza kudhibiti ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa na hata kuufanya usiwe tishio kwa maisha yako. Kama nilivyoahidi wiki iliyopita, wiki hii nimelazimika kurudia makala haya kwa faida ya wasomaji, hasa wale wanaosumbuliwa na ugonjwa huu.
Kitu cha msingi kuzingatia ni mtu kujitambua mapema kama una ugonjwa wa kisukari na kisha kuchukua hatua haraka ya kuudhibiti kwa chakula.

Mtu mwenye kisukari ambacho hakijakomaa sana, anaweza kukidhibiti kwa mlo tu bila kutumia dawa yoyote na akaweza kuishi bila matatizo. Lakini kisukari kilichokomaa kinahitaji mlo pamoja na dawa.

Hii ina maana kwamba kama kisukari chako hakijakomaa na kuwa tishio kwa afya yako, hali hiyo inaweza kubadilika na kuwa kisukari kilichokomaa iwapo hutazingatia ulaji wa mlo sahihi, hivyo hivyo kwa mgonjwa mwenye kisukari kilichokomaa anaweza kupoteza maisha haraka zaidi iwapo hatazingatia masharti ya vyakula.

Mtu mwenye ugonjwa wa kisukari anatakiwa kupunguza ulaji wa vyakula vyenye wanga (Carbohydrates), kama vile viazi, mihogo, mikate myeupe (White Bread), n.k. apunguze ulaji wa vyakula vya mafuta na kula vyakula vya protein kwa kiasi kidogo.

Badala yake mgonjwa huyu anapaswa kutumia kwa wingi vyakula vyenye kiasi kikubwa cha kirutubisho kiitwacho ufumwele (fibre) ambacho hupatikana kwenye vyakula kama vile matunda, nafaka zisizokobolewa (ugali sembe, dona, mtama, mikate myeusi, n.k) na aachane kabisa na kula vyakula vilivyosafishwa (refined foods).

Aidha, saladi (mchanganyiko wa wa mboga mbichi) inaweza kuliwa kwa kiwango chochote, lakini tahadhari ichukuliwe kwa saladi zilizowekewa mafuta mengi. Kwa kuwa matunda mengi yana kiasi fulani cha sukari, mgonjwa atapaswa kula matunda baada ya kupewa ushauri na daktari atakayejua kiasi cha sukari alichonacho. Juisi za matunda nazo ziepukwe na pale zinapotumiwa, ziandaliwe na maganda yake, kama vile apple na peasi.

Matunda yanapoliwa, hii ni kwa watu wote, hayapaswi kuliwa pamoja na chakula kwa wakati mmoja. Matunda huliwa saa 2 kabla ya kula au baada ya mlo ili kupata faida haswa za matunda.

Kwa ujumla mgonjwa wa kisukari, anapaswa kuogopa sana vyakula vyenye mafuta, hasa katika vyakula ambavyo mafuta yake hayaonekani moja kwa moja, kama vile maziwa (Full Cream Milk), kiini cha yai (Egg Yolk) na nyama nyekundu (Red Meats).
Unapokunywa maziwa, chagua maziwa yasiyokuwa na mafuta (Fat Free Milk au Skimed Milk), kama ni maziwa ya kuchemsha na kupoa, engua malai yake na yatupe, unapokula nyama ya kuku, usile na ngozi yake.

Ushauri mwingine unaotolewa kwa wagonjwa wa kisukari ni ufanyaji wa mazoezi mara kwa mara, ambayo huufanya mwili kuwa fiti na kuudhibiti ugonjwa huo. Mazoezi mepesi kama vile kukimbia taratibu (jogging), kuogelea na kutembea kwa mwendo wa haraka ni njia moja wapo ya kuuweka mwili wako imara dhidi ya kisukari.

Wagonjwa wa kisukari wanashauriwa kula milo yote, hasa baada ya kutumia dawa (insulin), kutokubadili dawa bila ushauri wa daktari na kuhakikisha wanapima mkojo mara kwa mara.

Pia mgonjwa azingaie haya yafuatayo:
1) Muda wa kula ni muhimu sana kwako. Kula mlo na vitafunwa vingine (snacks) muda ule ule kila siku kadri iwezekanvyo. Kula kitafunwa chochote wakati ufanyapo mazoezi au pale kiwango cha sukari kinaposhuka sana. Lakini hali ya kushuka sana kwa sukari inapokutokea mara kwa mara, wasiliana na daktari wako haraka.

2) Iwapo unatumia dawa, basi hakikisha kila wakati unapotaka kulala, unakula kitafunwa chochote. Kula mlo wako kwa kiwango kile kile bila kuzidisha, kwani kula kupita kiasi kunaweza kupandisha kiwango chako cha sukari.

Kila mgonjwa anapaswa kujua ni chakula gani akila kinaweza kumpa nafuu na kipi akikila kinaweza kumuongezea matatizo aliyonayo.

No comments: